MWENYEKITI
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC),Zitto Kabwe, amesema
kamati yake itatoa hoja ya kuanza mchakato wa kikatiba wa kumvua ujaji,
Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, jaji Frederick Werema.
Mbali na
dhamira ya kutaka jaji Werema avuliwe ujaji pia, Zitto amesema kamati
yake itapendekeza watu wote waliohusika katika kashfa ya wizi wa akaunti
ya Tegeta Escrow, wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na
kufilisiwa mali zao.
Zitto, alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na Tanzania Daima Jumapili, kuhusu sakata la Escrow linaloendelea hivi sasa.
Majibu ya
Zitto yalitokana na maswali ya gazeti hili yaliyotaka kujua hatua
zitakazopendekezwa na kamati yake baada ya kukamilisha kazi ya kupitia
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG), juu ya akaunti ya
Tegeta Escrow.
Alisema
kimsingi kilichofanyika katika tukio hilo ni zaidi ya wizi wa kawaida na
kwamba wahusika ni vema wakafilisiwa mali zao kisha wachukuliwe hatua
nyingine za kisheria.
“Suala hili
sio wizi wa kawaida bali ni ‘money laundering’. Kwa hiyo kufilisiwa ili
kurejesha fedha hizo ni hatua nyingine itakayopendekezwa”alisema Zitto.
Alisema
hatua hiyo itakuwa ni fundisho kwa wengine huku akikumbushia matukio ya
wizi wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje(EPA) na sakata la
kampuni ya kufua umeme wa Richmond.
Alisema
kamati yake bado inaendelea na kazi na kwamba walichogundua ni kuwa
fedha zilizokuwa katika akaunti ya Tegeta Escrow zilikuwa za umma na
kwamba kampuni ya Pan Africa Power Resources (PAP) hawakuwa na uhalali
wa kuchukua fedha hizo.
“PAC bado
inaendelea na kazi. Watu wote ambao wamehusika katika wizi huu
tutapendekeza wawajibishwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.”alisema
Tishio kwa wabunge
Baadhi ya
wabunge wanaonekana vinara wa kusimamia suala hilo wanaelezwa kutishia
maisha ambapo mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, ameshatoa ripoti
polisi
Wasiwasi wa
usalama wa wabunge hao umeongezeka zaidi baada ya taarifa kuwa mbunge wa
Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM), kulishwa sumu akiwa safarini
nchini Uingereza
Mkono
inadaiwa ndiye anayejua sakata la IPTL kwakuwa kwa muda mrefu amekuwa
akishiriki kwenye kesi akisimamia Tanesco na wizara ya Nishati na Madini
Mbunge huyo
anadaiwa kuvujisha siri ya uchotwaji wa fedha hizo kwakuwa Wizara ya
Nishati na Madini mwanzoni mwa mwaka huu haikuingia makataba wa kuitumia
kampuni ya uwakili ya mbunge huyo
Hata hivyo
Mkono, mwenyewe mara kadhaa alishakanusha madai ya kushiriki kwenye
kuvujisha siri za ufisadi huo wala kuwa nyuma ya sakata hilo.
Na Abdallah Khamis, Mtanzania Daima
Post a Comment