JESHI la
Polisi mkoani Mwanza linamshikilia askari wake WP Fatuma wa Kituo cha
Polisi Igogo wilayani Nyamagana kwa kosa la kumjeruhi mtumishi wake wa
ndani kwa mkumkata vidole vyake vinne vya mkono wa kulia kwa panga,
akimtuhumu kumwibia Deki ya Video nyumbani kwake.
Tukio hilo
la kujeruhiwa kijana Steven Magessa (18), lilitokea Oktoba 20 mwaka huu
katika kijiji cha Magange Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara
nyumbani kwao kijana huyo aliyekuwa amekimbilia huko baada ya kudaiwa
kumwibia mwajili wake nyumbani eneo la Igogo.
Akizungumza
na G.SENGO BLOG kijana huyo alieleza kuwa kufanya kazi kwa askari huyo
kulikuja mara baada ya askari huyo kumfuata kijijini na kumuomba ridhaa
ya wazazi wa kijana huyo kuambatana naye jijini Mwanza ili kumsaidia
kazi za nyumbani ambapo walikubaliana malipo ya kiasi cha Sh 50,000/=
kila mwezi jambo ambalo askari huyo alilikiuka na kushindwa kulitekeleza
kwa muda wa miezi sita bila kumlipa mshahara.
“Nilipoona
hajanilipa mshahara wangu kwa muda wa miezi sita huku kila ni kimwambia
ananijia juu na kunitukana matusi basi nilimuomba ruhusa ya kwenda
kijijini Oktoba 15 mwaka huu kumuona mama yangu mzazi aliyekuwa anaumwa
ili kupata nafasi ya kurudi nyumbani” alisema.
Steven
alieleza kuwa wakati akiwa kijijini askari huyo (Mwajili wake) alikuwa
akimpigia simu kumtaka arudi Mwanza kuendelea na kazi na kudai kuwa
atamlipa malimbikizo ya mshahara wake kiasi cha Sh 300,000/= zilizokuwa
kama deni, Steven alikubali ombi hilo kwa kuomba atumiwe nauli na pesa
kidogo ya kumwachia mama yake, jambo ambalo askari huyo alikaa kimya
bila majibu.
“Siku ya
Oktoba 20 mwaka huu majira ya saa 4:00 asubuhi alifika kijijini akiwa na
askari watatu kwenye gari la Polisi (Difenda) wa Kituo cha Mugumu na
kudai kuwa nipo chini ya ulinzi kisha kunifunga pingu, akidai kuwa
nilimwibia Deki ya Video na kutoroka nyumbani kwake, walinipandisha
kwenye Difenda kunipeleka kituoni “ alisema.
Kijana huyo
alieleza kuwa baada ya kufikishwa kituoni Mugumu askari huyo na wenzake
walianza kumuhoji huku wakimpa maneno ya vitisho, kijana huyo alipokataa
kuwa hakuiba wala kutoroka, Sajenti Fatuma aliamuru kijana huyo
kuvulishwa shati alilovaa na kisha akafungwa usoni na kuombwa anyooshe
mkono mezani ili apewe 'Sapraizi'.
"Sekunde
chache nilihisi kitu kikali kimenipitia kwenye vidole vyangu vinne vya
mkono wa kulia na kufuatiwa na maumivu makali, niliusogeza mkono wangu
mdomoni kuupoza kwa kuupuliza ndipo nilipo gundua kuwa nimekatwa kabisa
vidole vyangu vinne vya mkono wangu wa kulia ikibakia dole gumba tu"
kijana Steven alisimulia kwa uchungu.
“Niliangua
kilio kutokana na maumizu na sijui vidole vyangu hadi sasa sijui
vikowapi, askari wenzake baada ya kuona nimetokwa na damu nyingi
walimshauri anipeleke hospitali ya Wilaya ya Mugumu ili nipatiwe
matibabu kabla ya kuondoka kuja Mwanza,”alisisitiza.
Steven
alisema baada ya kupatiwa matibabu, tulienda kupanda basi ili kuja
Mwanza kwa madai kuwa amenifungulia kesi ya wizi wa Deki ya Video na
tuliopfika alinipeleka kituo cha Polisi Kati Nyamagana na kuniweka
Mahabusu akinituhumu wizi, lakini nilipochukuliwa maelezo nilikana
tuhuma za wizi na kueleza ukweli wangu ili kupata msaada.
Huku taarifa
zingine kutoka ndani ya jeshi zilizopatikana zilidai kuwa askari huyo
alikusudia kufanya ukatili huo kutokana na udanganyifu ambao alifanya
kwa uongozi wake akiomba kupatiwa silaha (SMG) kwa ajili ya kuitumia
kwenye kazi za nje lakini lengo ikiwa ni kwenda na silaha hiyo kwa ajili
ya kumkamata na kumtishia kijana huyo, jambo ambalo uongozi ulimgomea.
JESHI LA POLISI LINASEMAJE
Kamanda wa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Valentino Mlowola, jana ofisini
kwake amethibitisha kuwepo kwa taarifa za tukio hilo na kueleza kuwa
tayari Jeshi hilo limechukuwa hatua madhubuti hatua ya awali ikiwa ni
kumshikilia askari huyo kwa kufanya ukatili huo kwa kuvunja sheria na
kujichukulia sheria mkononi kumjeruhi kijana huyo.
Mlowola
alisema pamoja na kijana huyo awali kufunguliwa jarada la kutuhumiwa
kufanya kosa la wizi (Jinai) na kudaiwa kutorokea kijijini kwao, bado
askari huyo alitakiwa kufuata mfumo wa kiutawala na kisheria uliopo
kushughulikia suala hilo badala ya kuamua kujichukulia maamuzi ya
kumwadhibu mtuhumiwa kabla ya uthibitisho wa mashitaka yaliyokuwa
yamefungulia.
“Nilipopokea
taarifa hizi kwa mashangao na masikitiko makubwa na zimenisitua sana,
si kitendo cha kiungwana hata kidogo kwa mtu ambaye anatakiwa kufuata
taratibu za mfumo wa utawala na sheria katika utekelezaji wa
kushughulikia kero na matatizo ya jamii, alitakiwa kutumia busara kwani
tayari aliishamfungulia jarada la kumtuhumu kumwibia ikizingatiwa naye
ni mzazi wa watoto watano ni lazima anaujua uchungu,”alisema.
Kamanda
Mlowola alieleza kufatia ukatili huo kufanywa na askari wake ameunda
timu ya kikosi cha askari kwenda hadi kijijini Magange wilayani
Serengeti mkoani Mara ili kufanya uchunguzi wa tukio hili ikiwa ni
pamoja na kufanya mahojiano na familia, wananchi wa kijiji hicho kisha
Hospitali ya Wilaya ya Serengeti alipopatiwa matibabu ya awali.
“Ili tupate
ukweli wa jambo hili tumeunda timu hiyo, kwani kijana Steven tumemhoji
ametueleza jinsi askari Fatuma alichomfanyia na kudai hakumwibia, lakini
askri wetu pia amehojiwa awali amedai hakufanya kitendo hicho bali
wananchi ndo walimfanyia ukatili huo hivyo ni mkanganyiko lakini ukweli
utapatikana tu japo kuwa tukio hili halikufanyika Mwanza”alisisitiza.
Mlowola
alisema kwamba tayari tunamshikiria askari huyu na kumfungulia jarada la
uchunguzi kwa taratibu za kijeshi na ikibainika kutenda kosa hilo
tutumfukuza kazi na kumfikisha katika vyombo vya sheria ili kuchukuliwa
hatua zaidi kulingana na kosa alilofanya, lakini pia kijana Steven naye
anashikiriwa kwa tuhuma alizonazo za wizi kufatia jarada lililopo.
“Hatuwezi
kuendelea kucheka na kufumbia macho kitendo hiki ni jambo ambalo
linamgusa kila mtu hata mimi ni mzazi ukiachana na utumishi wangu wa
umma, ntahakikisha jambo hili nalishughulikia kwa umakini na kutoa
taarifa kwa umma ili pia kueleza wananchi kuwa tukio hili limefanywa na
mtumishi kama mtu si Taasisi ya Jeshi la Polisi na ahidi kutenda haki
kwenye hili,”alisisitiza.
Wito wangu
kwa wananchi ni kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuwaadhibu
watuhumiwa mbalimbali kabla ya kuthibitika kwa makosa na tuhuma hizo,
lakini wazingatie kufuata taratibu za kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria ili kushughulikia matatizo yao nawaomba waendelee kutoa
ushirikiana na kufuata mfumo uliopo badala ya kujichukulia sheria
mkononi.
Post a Comment