0
                                                   KOROSHO
Limekuwa ni jambo la kawaida sasa kwamba kati ya Novemba na Mei, mamia ya wakulima katika Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara huyaacha makazi yao na kwenda kuishi mkoani Lindi kwa ajili kuendesha kilimo cha ufuta.


Kinachowafanya wakulima hawa kuhamia katika wilaya za Liwale na Kilwa, si kingine bali ni bei ya ufuta ikilinganishwa na ile ya zaomama la korosho ambalo wamekuwa nalo kwa miaka mingi.
Kwa kuwa korosho ni zao la kudumu, haliruhusu kilimo cha aina nyingine hivyo wakulima hawa wa Tandahimba wanaona ni vyema kwenda Lindi ambako kuna ardhi kwa ajili ya kilimo cha ufuta ambacho kwa maelezo yao, wanadai kuwa “kinalipa zaidi”.
Wilaya ya Tandahimba ina wakazi 227,514 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya 2012. Eneo hilo lina kilomita za mraba 2048.56 ambazo kati yake asilimia 90 zinafaa kwa kilimo.
Hata hivyo, asilimia 91 ya eneo linalofaa kwa kilimo limefunikwa na miti ya mikorosho ambayo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wake. Wilaya hiyo inayoongaza kwa uzalishaji wa korosho, ikiwa imezalisha tani 32,000 msimu wa mwaka 2013/14.
Mkulima wa Kijiji cha Mkwiti, Mohamed Kawanga anasema: “Ardhi yetu imefunikwa na mikorosho, ambayo ni zao la miaka mingi, haina tena rutuba ya kuzalisha ufuta ambao unahitaji ardhi ambayo haijachoka sana au utumie mbolea nyingi.

“Tunaenda Lindi kwa sababu kule unakuta eneo kubwa lenye ardhi nzuri, ni rahisi kuendesha kilimo hicho… Hapa kwetu ukilima, huwezi kupata chochote.”
Kawanga anasema yeye ni mmoja wa wakulima ambao msimu wa 2013/14 walikwenda wilayani Kilwa kulima ufuta na alirejea baada ya kuuvuna.
Anasema alilima ekari tatu na alivuna ufuta magunia manne.
“Bei yake kwa kila kilo niliuza Sh2500. Ziliniwezesha kupiga hatua moja mbele ya maisha kwa kuwa nilipata Sh1 milioni ambayo tangu nimeanza kulima korosho sikuwahi kushika hela nyingi kiasi hicho,” anaeleza mkulima huyo.
Naye Rashidi Liteleko (50) mkazi wa Mkwiti Juu anasema wakulima wengi wamehamasika kulima ufuta kutokana na uwapo wa bei nzuri na uhakika wa soko, hata hivyo nasema kukosekana kwa ardhi yenye rutuba katika eneo lake ni kikwazo kwake.
“Napenda kulima ufuta lakini hapa kwetu wanasema ardhi imechoka na sehemu kubwa imefunikwa na mikorosho na ndiyo maana wenzangu wanakwenda kulima mbali, mimi sina uwezo wa kwenda kulima huko mbali,” anasema Liteleko.

Bei ya korosho
Katika msimu huo, wakulima waliuza korosho kwa bei ya Sh1,000 kwa kilo moja, kiasi ambacho wanakilalamikia kuwa ni kidogo ukilinganisha na gharama za uzalishaji wanazokadria kuwa zinafikia Sh1,100.
Hata hivyo, takwimu za Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) zinaeleza kuwa gahrama za uzalishaji wa kilo moja ya korosho inakifia Sh650.

Kawanga anasema kuyumba kwa bei ya zao la korosho kunawalazimisha kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 300 hadi wilayani Kilwa, Lindi kulima ufuta zao ambalo anasema lina bei nzuri na uhakika wa soko.
“Kama korosho zingekuwa na bei nzuri, tusingekwenda mbali kulima ufuta. Haya yote ni baada ya kuyumba kwa zao la korosho. Sasa tunalazimika kuangalia zao mbadala litakalotuinua kiuchumi baada ya kushindwa kwa korosho,” anasema Kawanga.
Kaimu ofisa kilimo wa Wilaya ya Tandahimba, Willfred Kilali anathibitisha kuwapo kwa idadi kubwa ya watu wanaoyahama makazi yao kwa muda kwa ajili ya kwenda mkoani Lindi na kwamba idadi hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka.

“Kila mmoja anahamasika kutokana na mafanikio aliyoyapata mwenzake. Kwa sasa hili ni tatizo kwa sababu linasababisha athari nyingine za kijamii na kiuchumi,” anasema Kilali.
Hata hivyo, anasema anaamini hakuna sababu ya wakulima wake kwenda kulima ufuta nje ya wilaya hiyo na anasisitiza kuwa bado kuna uwezekano wa zao hilo kulimwa wilayani Tandahimba iwapo wakulima wataelimishwa juu ya kilimo bora cha zao hilo.
“Iwapo Ufuta ungelimwa hapa, wangeuza hapa hapa na hivyo halmashauri ingepata fedha kutokana na ushuru. Ni suala ambalo sisi wataalamu tumeliona na tunajipanga kuwapa elimu ya kilimo bora cha zao hilo,” anasema Kilali.

“Ni kweli ufuta unahitaji ardhi yenye rutuba, hata hivyo wakulima wanaweza kuelimishwa kuhusu matumizi ya mbolea ili kurutubisha ardhi iliyochoka na wakapata mavuno mengi bila ya kuhama makazi kwa muda.”
Naye ofisa kilimo wa Wilaya ya Kilwa, John Mkinga anathibitisha wilaya yake kupokea wakulima kutoka Wilaya za Tandahimba, Newala na maeneo mengine ya Mkoa wa Mtwara wanaolima ufuta.
“Wilaya imepokea wakulima kutoka wilaya za Tandahimba na Newala wanaokuja kulima ufuta... Siwezi kutoa takwimu ni wangapi kwa sababu tulikuwa hatujaweka mfumo rasmi wa kuwatambua. Sasa tumeagiza viongozi wa vijiji kuwatambua wageni wote,” anasema Mkinga.“Msimu wa kilimo 2013/14 Wilaya yangu ilikadiria kulima hekta 29,652 za ufuta, kwa sasa tumevuka lengo hilo baada ya hekta 30,100 kulimwa. Makisio yetu ya mavuno ni tani 20,756.4 kwa wastani wa kilo 700 kwa hekta.’’MWANANCHI

Post a Comment

 
Top