- Imezingatia asilimia 20 tu ya maudhui ya Tume
- Masharti ya mgombea binafsi hayatekelezeki
- Kura ya maoni kabla ya uchaguzi mkuu haiwezekani
- Muundo wa Muungano umeiweka Zanzibar pabaya zaidi
- Ni vigumu Rais wa Muungano kutoka Zanzibar
- Madaraka ya Bunge kuisimamia Serikali yamemomonyolewa
- Hakuna anakoenziwa Nyerere, maadili yametupwa
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amesema
muundo wa Muungano uliopendekezwa kwenye Katiba pendekezwa ‘una utata
mkubwa’ hasa baada ya kupunguza mambo ya Muungano na kwamba kunaipa
nguvu Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwa Serikali ya Tanganyika.
Alisema
muundo wa serikali mbili hauwezi kuendelea kwa sababu haiwezekani kuwa
na serikali ya Jamhuri ya Muungano, isiyovuka bahari.
Akizungumza
na NIPASHE ofisini kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam jana, Jaji
Warioba alisema pia kwamba haoni kama Wazanzibari watakubali kuipitisha
Katiba pendekezwa kwa kuwa Ibara ya 294 inataka Katiba ya Zanzibar
ifanyiwe marekebisho ili iwiane na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Alisema
wananchi wa pande zote walieleza namna kero za Muungano kwa kina na
ndiyo maana Tume yake ikapendekeza muundo wa Serikali tatu kama
mwarobaini wa matatizo hayo.
MALALAMIKO YA ZANZIBAR
Alisema
malalamiko makubwa kutoka Zanzibar ilikuwa kwamba; la kwanza, wanaona
Tanganyika imevaa koti la Muungano kwamba kwa hali ilivyo, wanaofaidi
Muungano ni Tanganyika.
Pili,
walisema kuongezeka kwa mambo ya Muungano kunapunguza mamlaka ya
Zanzibar kusimamia mambo yake.Tatu, kufuatana na makubaliano ya hati ya
Muungano, rais wa Zanzibar awe makamu wa rais.
“Katika
haya, Bunge Maalum limekubali kupunguza mambo ya Muungano; kwa hiyo
katika orodha mpya mambo yote ya uchumi yameondolewa kwenye orodha ikiwa
ni pamoja na biashara, mikopo ya nje, takwimu, utafiti na kwamba hata
sensa haitakuwa mambo ya Muungano.”
Jaji Warioba
alisema sensa ndiyo msingi wa mipango ya maendeleo, lakini sasa baada
ya kuondolewa kwenye Muungano, kila upande utashughulikia sensa yake na
pia Zanzibar wameridhika na sasa watasimamia uchumi wake kikamilifu na
pili imekubalika rais wa Zanzibar atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
“Mimi
naamini, mabadiliko haya hayataisaidia Zanzibar kwa sababu kwa kuondoa
mambo yote ya uchumi, Zanzibar ikasimamia mambo yake maana yake ni
kwamba serikali ya Muungano itakuwa inasimamia mambo ya Tanganyika tu
ndiyo hapo Tanganyika itakuwa imevaa koti la muungano,” alisema Jaji
Warioba.
Aliongeza:
“Haiwezekani ukasema una serikali ya muungano ambayo haivuki bahari na
ndivyo ilivyo sasa na ndiyo yalikuwa malalamiko kwa sababu Serikali ya
Muungano haivuki bahari.”
Alisema
wananchi wa Bara wanajua kwamba mambo yote yanayowahusu yanashughulikiwa
na serikali ya Muungano ikiwamo elimu, afya, maji, barabara na mambo
mengine wakati sivyo ilivyo kwa wananchi wa Zanzibar.
“Kwa wananchi wa Zanzibar hakuna hata moja kati ya haya linashughulikiwa na Serikali ya Muungano.”
Alitoa mfano
kwamba ndio maana hata kama Waziri wa Ujenzi au wa Uchukuzi wa Bara,
hata kama angekuwa ni mtendaji mzuri kiasi gani, hawezi kwenda Zanzibar.
“Hujaona
Waziri anavuka kwenda Zanzibar kufanya kazi. Utawaona kwa mfano Magufuli
anafanya kazi sana huwezi kumsikia amevuka kwenda Zanzibar. Mwakyembe
atatembelea bandari ya Dar es Salaam, lakini hujamsikia amevuka kwenda
Zanzibar; kwa sababu Serikali ya Muungano haina madaraka Zanzibar.”
Alisema:
“Kwa hiyo huwezi kusema una serikali ya Muungano ambayo haina madaraka
upande wa Zanzibar.”Pili, hii serikali ndiyo inayo hodhi sovereignty,
sovereignty ya nchi iko chini ya serikali ya Muungano, ndiyo
inayojulikana duniani kwamba serikali ya Tanzania ni Serikali ya
Muungano.
Alisema
rasilimali za Bara ndizo rasilimali za Serikali ya Muungano, hivyo hata
inapotaka kukopa hutumia rasilimali hizo na kwamba itakopa kwa ajili ya
Bara na kutafuta rasilimali kwa ajili ya Bara pia bila kuhitaji kibali
chochote.
Alisema kwa upande wa Zanzibar ni kinyume chake, kwa kuwa haina haki ya kukopa bila kupitia Serikali ya Muungano.
Alisema hiyo
ni kwa sababu rasilimali za Zanzibar haziko chini ya serikali ya
Muungano hivyo ili ikubali kukopa kwa ajili ya Zanzibar lazima itake
dhamana na kwamba hata katika Katiba pendekezwa, Zanzibar itaendelea
kuwa na tatizo hilo.
Kuhusu Rais
wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, alisema wakati
waasisi wa Taifa walipokuwa wanaunganisha vyama vya Afro-Shiraz na Tanu,
waliunganisha mambo mengi yaliyolenga kuunda Serikali ya Muungano.
“Kabla ya
hapo kulikuwa na rais na makamu wawili; Makamu mmoja ambaye alikuwa
makamu wa kwanza alikuwa Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu. Tukasema
ukifanya hivi hutaunganisha nchi, ni lazima anayemsaidia rais amsaidie
kwa nchi nzima.”
Alisema
baada ya kubaini ugumu huo, marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
ya mwaka 1977, yaliondoa nafasi za makamu wawili wa rais na kuweka
sharti kwamba rais akitoka upande mmoja wa muungano, makamu wake atoke
upande wa pili.
Alitoa mfano
kwamba wakati ule, rais wa Jamhuri alikuwa Hayati Mwalimu Julius
Nyerere (Bara) na Makamu wake akawa Rais wa Zanzibar na wakafuta Waziri
Mkuu asiwe makamu wa rais.
Alisema
mwaka 1984, upande wa Bara ulidhani Waziri Mkuu atakuwa ni nafasi ya
Bara peke yao na wakaamua kuirudisha kwamba naye awe Makamu wa Rais.
Alisema
alipoteuliwa kushika wadhifa huo nafasi hiyo mwaka 1985 ilikuwa
imerudishwa, lakini mwaka 1992, walibaini kwamba maamuzi hayo
yalirudisha nyuma azma ya Muungano, hivyo wakaamua kumwondoa Waziri Mkuu
kwenye wadhifa wa Makamu wa Rais kwa nia ya kutoa fursa kwa viongozi
hao watoke upande wowote wa Muungano.
Alisema
kurudisha makamu wa rais watatu kunafanya wakati wote Rais wa Jamhuri ya
Muungano atoke Bara.Ibara ya 99 ya Katiba pendekezwa inaeleza kuwa
kutakuwa na Makamu wa Rais watatu ambao watakuwa:
(a) Makamu wa Kwanza wa Rais;
(b) Rais wa Zanzibar ambaye atakuwa Makamu wa Pili wa Rais; na (c) Waziri Mkuu ambaye atakuwa Makamu wa Tatu wa Rais.
“Kwa sababu
haiwezekani kwamba ukawa na marais wawili; Rais wa Zanzibar na Rais wa
Jamhuri wote wanatoka upande mmoja na hasa kwa kuwa huyu Rais wa
Muungano anashughulikia zaidi mambo ya Bara; kwa utaratibu huu ni kwamba
utafanya haitawezekana tena kupata rais kutoka Zanzibar.”
Alisema
Zanzibar pia haitaweza kutoa Waziri Mkuu kwa kuwa makamu watatu
wanaliopendekezwa mmojawapo ni mgombea mwenza ambaye lazima atoke
Zanzibar kwa kuwa rais atatoka Bara, mwingine ni Rais wa Zanzibar na
mwingine ni Waziri Mkuu ambaye haitawezekana naye akatoka Zanzibar.
Alisema kwa
utaratibu huo, kama taifa tunarudi nyuma kwa kuwa ile dhana ya kiongozi
atoke upande wowote ule kiuhalisia haitawezekana.
“Kwa hiyo kwa kufanya hivi mimi sioni kama Zanzibar wamepata faida yoyote.”
Alisema
katika mambo ya Muungano, suala la kodi ya mapato yanayolipwa na watu
binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa amabzo
zimekuwa za Muungano.
Alisema mgogoro wa kwanza kuhusu Muungano ulitokana na masuala ya mapato na sababu zake zinaeleweka.
“Zanzibar
imepewa mamlaka kuendesha uchumi wake, kwa hiyo ni lazima iwe na mapato.
Vyanzo vikubwa vya mapato ni hivi vilivyotajwa; kodi ya mapato, ushuru
wa bidhaa na ushuru wa forodha. Huwezi kuipa madaraka kisha
ukainyang’anya uwezo wa kifedha hiyo ndiyo inayoleta mgogoro.”
Alisema
mwaka 1977 iliamuliwa kwamba kodi hizo zinazopatikana Zanzibar zisiletwe
kwenye serikali ya Muungano na kwamba ndivyo ilivyo hadi sasa.
Alisema
Zanzibar haitaweza kujiendesha bila kodi kwa kuwa nusu ya mapato yao
yanatokana na kodi hizo na kwamba mapendekezo yaliyopo kwenye Katiba
hayatatekelezeka.
“Na Zanzibar
watalikataa. Mimi nadhani hapa wamekosea (BMK). Tume ilipendekeza
ushuru wa bidhaa ndiyo iwe kodi ya Muungano kwa sababu kwa upande wa
Bara ndio chanzo cha pili kwa ukubwa.”
Alisema
mwaka 2012/13; ushuru wa bidhaa uliingizia Bara mapato ya Sh. trilioni
1.3 lakini Zanzibar ilikusanya Sh. bilioni 11 na kwamba fedha hiyo ni
kidogo ambayo Zanzibar ingeweza kuchangia kwa kuzingatia kuwa masuala
mengi ya Muungano yapo zaidi Bara kama jeshi.
“Matatizo ya
Zanzibar hasa kuhusu mikopo na misaada yatakuwa makubwa zaidi. Uhuru wa
mahusiano wa mahusiano ya kikanda na kimataifa nao utakuwa mdogo;
Zanzibar haiwezi kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Umoja
wa Afrika, Sadc, OIC, UN na mashirika yake, kwani uanachama unahitaji
sovereignty,” alisema.
MALALAMIKO YA BARA
Alisema
wakati wa kukusanya maoni, wananchi wengi wa Bara walilalamikia
mabadiliko makubwa ya Katiba ya Zanzibar kwamba imeingilia Katiba ya
Muungano kwa kuwa sheria zinazopitishwa na Bunge la Jamhuri haziwezi
kutumika Zanzibar bila kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi.
Pili,
alisema wananchi wa Bara hawana haki ya kumiliki ardhi Zanzibar na pia
hawana haki ya kuchaguliwa au kupiga kura; wakati ni kinyume chake kwa
wananchi wanaotoka Zanzibar ambao wanaishi Bara.
Kadhalika,
Mahakama ya Rufani haina madaraka Zanzibar, mashauri yanayotokana na
haki za binadamu na Mahakama za Kadhi. Pia Katiba ya Zanzibar
inavitambua visiwa hivyo kama nchi kamili.
Hata hivyo,
alisema inawezekana wajumbe wa BMK walikubaliana ndani ya Bunge mambo
kadhaa ambayo hawakutaka kuyaweka hadharani hasa suala la kuirekebisha
Katiba ya Zanzibar.
Ibara ya 294 ya Katiba pendekezwa inaeleza kuhusu mambo ya mpito ikiwamo:
(a)
kurekebisha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 ili kuwiana na masharti ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 2014;
(b) kutunga
na kurekebisha sheria mbalimbali za Jamhuri ya Muungano, sheria ambazo
si za Muungano zinazohusu Tanzania Bara na sheria za Zanzibar ili
kuwiana na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
Mwaka 2014.
“Kwa kuwa
ardhi imeingizwa kwenye Katiba basi Zanzibar italazimika kubadili sheria
yake ili raia wote wawe na haki sawa. Pia sheria za uchaguzi nazo
zitabadilika ili raia wote wawe na haki za kiraia. Kama mabadiliko hayo
yamekubalika Zanzibar basi wananchi wa Tanzania Bara hawatakuwa na
malalamiko yoyote ya msingi,” alisema.
Jaji Warioba
aliongeza: “Tatizo ninaloliona mimi ni ugumu wa kufanya mabadiliko
haya. Katika taarifa ya Tume tulisema kama kuna jambo ambalo tuliona
Wanzanibari wameungana ni Zanzibar kuwa nchi. Ili mabadiliko yafanyike
kwenye Katiba ya Zanzibar ni lazima yapatikane maridhiano, pasipo na
maridhiano Baraza la Wawakilishi halitapata kura za kutosha kupitisha
marekebisho.”
“Hali
itakuwa ngumu zaidi kwenye kura ya maoni kama Katiba ya Zanzibar
inavyotaka. Kazi kubwa ipo katikakusuluhisha makundi ya Zanzibar kwa
suala hili. Uhasama unaoonyeshwa hadi sasa unatia wasiwasi, kama
marekebisho hayatafanywa, Katiba inayopendekezwa itabaki ni Katiba ya
Tanganyika; Zanzibar itabaki ni nchi yenye mamlaka na madaraka makubwa
na Tanganyika ndiyo itakuwa Muungano.”
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment