0
Mbunge akanusha kufanya vurugu kwenye ndege
MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki Tanzania (EALA) Shy-Rose Bhanji amesema tuhuma dhidi yake zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii na magazeti mengine katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo, zimelenga kuchafua sifa yake, sababu kubwa akisema ni chuki dhidi ya watu wasioipenda misimamo yake ndani ya bunge hilo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, amesema baadhi ya misimamo hiyo ni kutetea ardhi ya Tanzania ibaki kuwa mali ya Watanzania ;na pia msimamo wake wa kumtetea Spika wa EALA, Dk Margaret Zziwa wa Uganda asiondolewe katika nafasi yake, kama baadhi ya wabunge wanavyotaka.

Alisema kutokana na misimamo hiyo, amekuwa akikwaruzana mara kwa mara na baadhi ya wabunge wa bunge hilo, hivyo sasa wameamua kumtafuatia mkakati mwingine wa kumchafua, akitolea mfano kile kinachodaiwa kulewa na kufanya vurugu katika ndege wakati wabunge hao wakiwa safarini kwenda Ubelgiji.

“Ni uzushi wa hali ya juu na hakuna mwenye kuthibitisha hilo…Kitendo chochote cha kuhatarisha usalama ndani ya ndege ni kosa ambalo Mbunge kama mimi siwezi kuwa na kinga nalo. Jambo kubwa na la hatari kama hilo maana yake ningeishia mikononi mwa polisi baada ya kutua Ubelgiji, na pengine nisingeshiriki shughuli iliyonipeleka kule.

“Lakini pia lingeripotiwa katika vyombo husika nchini mwangu, lakini kote huko hakuna kitu kama hicho kwa sababu ni uzushi unaoenezwa kwa lengo la kunichafua na kunivunja nguvu.

“Iweje wamesubiri wiki mbili baada ya madai hayo ya kuwapo tukio la kutunga ndipo wajitokeze wakati wa kikao kinachoendelea mjini Kigali, Rwanda?..madai mengine ni kwamba nimewakashifu au kuwatolea lugha mbaya viongozi wakuu wa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, haya nayo ni uzushi mwingine. Ni uzushi kwa sababu sijawahi kutoa maneno ya aina hiyo, iwe ndani Bunge au nje. Nitaendelea kuwaheshimu marais wa nchi hizi tano na wananchi wake,” alisema.

Alielezea kushangazwa kwake na baadhi ya wabunge kushinikiza madai hayo yajadiliwe bungeni, hali iliyosababisha kukwama kwa kikao cha katikati ya wiki iliyopita jijini Kigali kwa sababu ya kutotimia kwa akidi.

Kutokana na hayo yanayoendelea dhidi yake, aliwataka Watanzania kuelewa ukweli wa mambo yanayozushwa, huku akisema atasimama kidete kuona Tanzania haiburuzwi katika bunge hilo, hasa kwa mambo yasiyo na maslahi kwa nchi.HABARILEO

Post a Comment

 
Top