Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Ludovick Utouh.
Na Mwandishi wetu
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali inapenda kuujulisha Umma kuwa Ukaguzi Maalum wa
akaunti ya Tegeta Escrow ambao unafahamika kama Ukaguzi wa IPTL
unaendelea na unaongozwa na Hadidu za Rejea (ToR) zilizotolewa na kisha
kuridhiwa na Ofisi ya Bunge na Wizara ya Nishati na Madini.
Ukaguzi wa akaunti ya Tegeta Escrow
uliombwa na Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini.
Ukaguzi huu unalenga kufanya uchunguzi wa kina ambao utatoa taarifa
kamili yenye kuonesha hali halisi kuhusu miamala (transactions) kwenye
akaunti maalum ya Tegeta Escrow kisha kutoa taarifa kuhusiana na ukaguzi
huo.
Kwa kuwa Hadidu za Rejea pekee
haziwezi kuonesha ukubwa wa kazi bali utekelezaji wa kazi yenyewe ndio
unaoweza kutoa taswira halisi, ni vyema umma wa watanzania ukatambua
kuwa Ukaguzi huu haujaweza kukamilika kwa kipindi kilichokadiriwa awali
hivyo ukaguzi unaendelea kwa kuzingatia Hadidu za Rejea na kifungu cha
29 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008.
Aidha, ongezeko la muda wa
kukamilisha ukaguzi huu limetokana na uhitaji wa kukusanya maelezo
yanayoendana na vielelezo vinavyojitosheleza ili kumsaidia mkaguzi
kufikia malengo ya ukaguzi huo.
Ukusanyaji wa taarifa hizo
unategemea wahusika kutoka Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na
taasisi na Watu binafsi waliopo nchini na nje ya nchi ambao ni wadau
katika suala hili.
Hata hivyo licha ya changamoto
zilizoainishwa hapo juu, ukaguzi wa IPTL unaendelea na muelekeo ni mzuri
kwa sababu ni maeneo machache tu yaliyobakia ambapo yatakapo kamilika
tutawasilisha ripoti kwa taasisi zilizouomba ukaguzi huu kwa mujibu wa
Sheria.
Aidha, tunaendelea kupata
ushirikiano mzuri kutoka kwa wadau wa ukaguzi huo. Ifahamike kuwa
ukaguzi bado unaendelea hivyo itakuwa ni kinyume na utaratibu kwa Ofisi
hii kuzungumzia kwa kina taarifa ya ukaguzi wa IPTL kwa sasa.
Ofisi hii itaendelea kutekeleza
majukumu yake yote kwa kuzingatia misingi ya uwazi na uwajibikaji
usiokiuka taratibu za kisheria katika kukusanya na kutumia rasilimali za
umma.
Post a Comment