Maambukizi Katika Njia ya Mkojo (UTI) ni moja kati
ya magonjwa ambayo hayapewi msisitizo wa kutosha katika jamii licha ya
kuwa wengi huathirika kwa ugonjwa huu bila kujua chanzo, tiba na kinga
yake.
Ugonjwa huu huanza kuathiri mirija inayopitisha
mkojo, baadaye huenea katika kibofu na figo. Mgonjwa anaweza kupata
ugonjwa sugu wa figo na kupoteza maisha kama ugonjwa huu hautatibiwa
mapema.
Wataalamu wa afya wanasema UTI husababishwa na
vimelea ambao huingia kupitia mirija inayosafirisha mkojo na kuutoa nje.
Vimelea hawa wanashambulia kibofu na baadaye huendelea mpaka kwenye
figo. Hii ndiyo hatua kubwa ya ugonjwa ambayo inaweza kusababisha kifo
au tatizo la kudumu.
Hawa ni vimelea wa jamii ya bakteria walio wanajulikana kwa jina la escherichia coli (E.coli).
Bakteria hawa wanapatikana katika utumbo mpana
lakini husafiri kupitia njia ya haja kubwa kwenda katika njia ya mkojo
na kusababisha maambukizi katika kibofu na figo.
UTI inavyoenea
Dk Veronika Kaniki kutoka hospitali ya Sekou
Toure, anabainisha tabia na mazingira yanayoweza kusababisha maambukizi
katika njia ya mkojo kuwa ni kushiriki ngono mara kwa mara na watu
tofauti bila kutumia kinga.
Anasema hii inamfanya mtu kuchukua bakteria wa UTI kutoka kwa mwenzi wake ambaye tayari ana maambukizi hayo.
Dk Kaniki anaongeza kuwa kujitawaza kutoka nyuma kuja mbele baada ya haja kubwa kunapelekea maambukizi hasa kwa wanawake.
Hii ni kwa sababu vimelea hao hupatikana kwa wingi katika utumbo mpana.
Hivyo, kitendo cha kujisafisha kwa njia hiyo,
anasema huwasafirisha bakteria hao kutoka sehemu ya haja kubwa kuja
katika njia ya haja ndogo.
Anasema mazingira haya husababisha UTI kwa wanawake kwa sababu njia ya haja kubwa na ndogo zipo karibu sana.
“Mama wajawazito pia wako hatarini zaidi kwa
sababu mimba kukandamiza kibofu na kusababisha kukosekana kwa uwazi
katika njia ya mkojo ambayo kitaalamu inajulikana kama incomplete
emptying,” anafafanua Dk Kaniki.
Mtaalamu wa magonjwa ya figo kutoka Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, Dk Fransis Fredrick anasema takwimu zinaonyesha kuwa
kwa kila wanawake watano, mmoja amewahi kupata ugonjwa huo.
Hali hiyo anaielezea kuwa huweza kuwa ni ya
kujirudia mara kwa mara kwa baadhi ya wanawake, hasa kinamama wajawazito
na watu wenye umri mkubwa.
Mbali na wanawake kupata maambukizi zaidi, Dk Fredrick anaeleza kuwa watoto wa jinsi zote pia wako hatarini.
Anasema ni vema mazingira ya chooni na bafuni yawe safi ili kuwalinda watoto dhidi ya maambukizi haya.
Dk Fredrick anabainisha kuwa maambukizi katika
njia ya mkojo yanaweza kusababishwa na bacteria, fangasi au virusi.
Anasema matibabu yake hutolewa kulingana na aina ya vimelea
waliosababisha maambukizi hayo.
Kisukari huathiri zaidi
Maambukizi haya yanaweza pia kuwaathiri watu wenye kisukari kirahisi zaidi kwa sababu ya sukari nyingi iliyopo katika mkojo.
Sukari hiyo huchochea kuzaliana kwa bacteria wanaosababisha maambukizi.
Kwa mujibu wa ripoti iliyofanywa na Chama cha
Kisukari cha Marekani (ADA), asilimia 9.4 ya watu wanaokutwa na kisukari
wanaugua pia UTI wakati asilimia 5.7 ni wenye maambukizi lakini hawana
kisukari.
Wenye kisukari wanaathirika zaidi kwa sababu pia
bakteria kuzaliana kwa wingi na baadhi ya mishipa inaharibika na
kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.
Hata hivyo, ripoti hiyo imebainisha kuwa sukari nyingi iliyopo
kwenye damu ya mgonjwa wa kisukari inaua seli nyeupe za damu, hivyo
mwili unakosa kinga ya kupambana na bakteria hatarishi walioingia
mwilini.
Athari, dalili, tiba
Dk Kaniki anafafanua kuwa endapo mtu hatatibiwa
mapema au kumaliza dozi, ugonjwa huu unaweza kuwa sugu na kusababisha
kuharibika kwa figo na kibofu.
Anasema maambukizi yanayotokea chini ya kibofu huathiri kibofu na mirija inayotoa mkojo nje.
Maambukizi yanayotokea katika figo ni hatua ya juu
na athari zake ni kubwa zaidi kuliko athari zitokeazo katika mirija na
kibofu.
Alibainisha athari nyingine kuwa mwanamke mjamzito anaweza kuzaa mtoto kabla ya wakati au mtoto kuzaliwa akiwa na uzito pungufu.
Anasema wagonjwa wanashauriwa kupata tiba mapema
na kumaliza dozi na kwamba watoto wadogo na wazee pia wanaweza kupata
maambukizi hayo kirahisi.
Ripoti ya ADA inabainisha dalili za awali kwa mtu
mwenye maambukizi katika njia ya mkojo ni maumivu wakati wa kukojoa,
kuhisi kukojoa laini ukienda chooni mkojo unatoka kidogo sana, kukojoa
mkojo wenye damu na maumivu ya tumbo na mgongo.
Dalili kwa maambukizi yaliyokomaa, zinaelezwa kuwa ni homa kali, kutetemeka, kutapika, kuharisha na maumivu ya mgongo.
Hata hivyo, kinga ya ugonjwa huu inaelezwa kuwa ni
kuzingatia kanuni za usafi hasa baada ya haja kubwa na kujisafisha
kuanzia sehemu ya mbele kwenda nyuma ili kutoruhusu vimelea kuingia
katika njia ya mkojo kwa urahisi.
Inashauriwa kumwona daktari baada ya kuona dalili hizi na kutumia kikamilifu dawa itakayopendekezwa na daktari.
Ni muhimu kwa mgonjwa kumaliza dawa ili kuzuia kujirudia kwa ugonjwa huo mara kwa mara na kusababisha madhara au usugu.MWANANCHI
Post a Comment