Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba sasa lipo katika hati hati ya kuendelea kutokana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kutangaza kuwa hawatakuwa tayari kujadili rasimu tofauti na iliyowasilishwa na Jaji Joseph Warioba bungeni.
Wakizungumza katika mkutano na waandishi wa habari
jana katika Ukumbi wa Pius Msekwa bungeni, viongozi wa Ukawa, Profesa
Ibrahim Lipumba, James Mbatia, Freeman Mbowe na Tundu Lissu, walisema
wataitetea rasimu hiyo, ndani ya Bunge na kwenye Kamati.
“Rais Jakaya Kikwete amekuja bungeni siyo kufungua
Bunge la Katiba bali kaja na mapendekezo ya rasimu ya CCM, sisi
tutajadili rasimu ya wananchi ya Jaji Joseph Warioba ambayo inazungumzia
muundo wa Muungano wa Serikali tatu,” alisema Profesa Lipumba.
Kutokana na msimamo huu wa Ukawa huenda Bunge
litakwama kwani kwa mapendekezo ya CCM yenye Muundo wa Muungano wa
Serikali mbili ni lazima kuandikwa upya Rasimu ya Katiba au kufanyika
mabadiliko makubwa.
Profesa Lipumba alisema katika majadiliano juu ya
rasimu, Ukawa watajikita kutumia Rasimu ya Katiba waliyopewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ambayo imeeleza mapendekezo kwa nini yamefikiwa
katika kila hoja,” alisema.
Hata hivyo, alisema wamesikitishwa sana na Rais
Jakaya Kikwete, badala ya kufungua Bunge alijikita katika kuchambua
rasimu na kuikosoa tume aliyoiunda mwenyewe.
“Rais Jakaya Kikwete siyo tu amemdhalilisha Jaji
Warioba pamoja na wajumbe wa Tume, bali amewadhalilisha wananchi
waliotoa maoni kwani hata takwimu alizotoa za kupinga rasimu siyo za
kweli,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema muundo wa Serikali tatu ndio mawazo ya
wananchi ambayo yamekusanywa na watu wenye heshma wakiwapo Jaji Warioba
aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais na Jaji Augustino Ramadhani
ambaye pia amewahi kuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Alisema kauli za Rais badala ya kuimarisha umoja
zimewagawa Watanzania kwani ametoa vitisho ambavyo havina sababu hasa
kwa Wapemba bila kujua kuna Wanyamwezi wanaoishi Zanzibar.
Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye
pia ni mjumbe wa Bunge hilo, alisema kwa kauli ya juzi ya Rais Kikwete,
kutangaza kuwapatia Zanzibar; watu, ardhi, mamlaka kamili na kusimamia
uhusiano wa kimataifa ni kuvunja rasmi Muungano,
Mbatia alisema Rais Kikwete pia amewagawa
Watanzania katika kauli zake ikiwa ni pamoja na ile ya Wapemba kwa
kulima vitunguu katika Jimbo la Kibakwe kana kwamba ni makosa.
Alisema wamesikitishwa na Rais kuacha kufungua Bunge badala yake
katumia taarifa potofu za mitaani kuligawa Bunge na kuwadhalilisha
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hakuna asiyejua sasa tupo katika mgogoro mkubwa
wa kikatiba, Zanzibar tayari ni nchi kamili kutokana na mabadiliko ya 10
ya katiba yao waliyoyafanya mwaka 2010 baada ya kupitisha dhana ya kuwa
Zanzibar ni nchi,” alisema.
Mbowe
Mbowe alisema Rais amevunja maridhiano na hata
kushindwa kusikiliza maoni ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya,
Seneta Amos Wako kuwa maoni ya wananchi yaheshimiwe.
Alisema Serikali ya Kenya ilichakachua maoni,
ilichakachua rasimu na kusababisha vurugu kubwa jambo ambalo linaweza
kutokea kwa Tanzania.
“CCM wasijidanganye kwa wingi wao bungeni hakika katika hili tutatetea madai na maoni ya wananchi hadi mwisho,” alisema.MWANANCHI
Post a Comment