0
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta amedhihirisha wazi kuwa hapendi na hathamini kazi kubwa inayofanywa na vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusu mchakato wa Katiba mpya.
Mapema wiki hii, Sitta alionesha dhamira hiyo pale alipowaeleza wajumbe wa Bunge hilo liwa kuna chombo kimoja cha televisheni kimekuwa maarufu ya kurusha midahalo na makongano huku kikiwaalika waliyokuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kana kwamba hakina habari nyingine za kutangaza.
Sitta alikwenda mbali zaidi akimtaka Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kuangalia uwezekanu wa kukithibiti chombo hicho.
Tunalaani kwa nguvu zote kauli ya kipuuzi ya Sitta. Na kwa maoni yetu kufumbia macho jambo hili ni sawa na kukubali kuizika tasnia ya habari pamoja na kuzika uhuru wa vyombo vya habari na vile vile kuwanyima wananchi haki yao ya kikatiba ya kupata habari.
Pamoja na kwamba Sitta hakukitaja moja kwa moja chombo lengwa lakini ni dhahiri alikilenga kituo cha ITV ambacho mmiliki wake, Reginald Mengi ametumia uzalendo kutoa nafisi ya kurusha matangazo ya midahalo na makongano ili wananchi wapate kufuatilia mchakato wa katiba.
Mbali na midahalo na makongamano, pia ITV imekuwa ikitoa fursa ya viongozi waandamizi wa CCM husuasani mawaziri akiwemo Sitta kueleza maoni yao kuhusu mapendekezo ya rasimu ya Katiba mpya.
Ukilinganisha nafasi waliyopata katika ITV wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na viongozi wa serikali ya CCM kama Sitta na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uaratibu), Stephen Wassira, ni wazi kwamba kiongozi huyo hana shukrani zaidi ya kujawa na ubinafsi.
Lakini tunajiliza hili litakuwa Bunge la aina gani ambalo Sitta na wenzake wanataka wasikosolewe kwa lolote wakati wao sio miungu na kila mara wamekuwa mabingwa na kuvunja kanuni na taratibu?
Sitta anataka Jaji Joseph Warioba na  wenzake wasipewe nafasi ya kuzungumzi upotoshwaji wa wazi unaofanywa na viongozi wa serikali ya CCM dhidi ya rasimu yake, lakini yeye anona ni haki yake ya msingi kuiponda rasimu inayopendekezwa bila hata kupata ufafanuzi kutoka kwa wale walioiandaa.
Tunachelea kuamini kwamba Sitta aliteleza kwa kauli ile, ila bado tunamsihi atumie fursa hii kuviomba radhi vyombo vya habari kabla havijamharibia safari yake ya kusaka urais kama inavyodaiwa.
Kama Sitta hataki kukosolewa ni vyema akaacha kuvunja kanuni za Bunge hilo na badala yake ajitenge na ushabiki wa maslahi ya chama chake asimamie ukweli wa kulinda matakwa ya wananchi ili asije kulaaniwa na historia ya taifa hili.TANZANIA DAIMA

Post a Comment

 
Top