Dar es Salaam. Serikali imepoteza zaidi ya Sh362.9 bilioni kutokana na baadhi ya kashfa kubwa za ufisadi na operesheni mbalimbali zilizoligharimu taifa tangu uhuru.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini taifa kukumbwa
na kashfa mbalimbali za upotevu wa fedha au kuanzisha mipango ambayo
utekelezaji wake ulisababisha maumivu kwa wananchi na hakuna awamu ya
uongozi wa Serikali iliyokwepa hali hiyo.
Kuanzia awamu ya kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere
aliyeiongoza nchi toka mwaka 1961 ilipopata uhuru hadi 1986, Rais Ali
Hassan Mwinyi (1986-1995), Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) na Rais
Jakaya Kikwete (2005-hadi sasa), kumeibuka kashfa mbalimbali, saba
zikiwa kubwa na kulitikisa taifa.
Kashfa na operesheni saba kubwa zilizotikisa taifa
ni pamoja na Operesheni Uhujumu Uchumi, ufisadi katika Mfuko wa
Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import Support –
CIS) na Kashfa ya Rada.
Nyingine ni ufisadi Akaunti ya EPA, kashfa ya
Richmond, Operesheni Tokomeza Ujangili na ile ya uchotaji mabilioni
katika akaunti ya Escrow.
Operesheni Uhujumu Uchumi
Mwaka 1984 Serikali ilianzisha Operesheni Uhujumu
Uchumi, iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Sokoine ili
kutaifisha mali ambazo baadhi ya watu walidaiwa kujipatia kwa njia isiyo
halali.
Operesheni hiyo ilishuhudia baadhi ya watuhumiwa
wakimwaga fedha mitaani na majalalani, huku wengine wakitupa mali
kuhofia kutiwa kwenye mkono wa sheria.
Hata hivyo, katika operesheni hiyo baadhi ya
watendaji wa Serikali ambao hawakuwa waaminifu, waliitumia nafasi hiyo
vibaya kutaifisha mali za baadhi ya watu, ambao hawakuwa wahujumu
uchumi.
Zoezi hilo lilisababisha wananchi kadhaa hasa
vijijini kuwekwa ndani na wengine kuachwa maskini baada ya kunyang’anywa
mali zao ikiwamo mifugo na mashine za kusaga nafaka, kwa kudaiwa kuwa
walizipata kwa njia isiyo halali.
Mfuko wa Commodity Import Support (CIS)
Miaka 24 baadaye yaani mwaka 2008, liliibuka
sakata jingine lililokuwa na harufu kubwa ya ufisadi wa mabilioni katika
Mfuko wa Kuwezesha Uagizaji Bidhaa kutoka Nje ya Nchi (Commodity Import
Support – CIS).
Mwaka 2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la ufisadi kwa mara nyingine. Safari hii uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada kuukuu kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada hiyo unatajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu taifa Sh29.5 bilioni, wakati gharama halisi ilikuwa Sh21 bilioni.
Sakata hilo liliwahusisha baadhi ya wanasiasa, wafanyabiashara
maarufu nchini na wizara kadhaa za Serikali ya Muungano na ile ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Kupitia mfuko huo, vigogo hao walichota zaidi ya Sh200 bilioni kwa kivuli cha uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi.
Mfuko huo wa CIS, ulianzishwa katika miaka ya
1980, ambapo baadhi ya nchi wafadhili ikiwamo Japan, zililenga kuipatia
Tanzania fedha za kigeni za kununulia malighafi, vyombo vya usafiri wa
barabara, vifaa vya kilimo, ujenzi na vingine mbalimbali. Mpango huo
ulioanzishwa na Serikali uliendelea hadi mwanzoni mwa miaka 2000, ambapo
nchi hizo wahisani ikiwamo Japan, Uingereza, Uholanzi, Saudi Arabia,
Norway, Uswisi, Ubelgiji, Sweden na Denmark zilikuwa zikiipatia Serikali
fedha za kigeni ili kuimarisha sekta za biashara.
Wizara zilizotajwa katika orodha ya wadeni wa CIS
ni pamoja na iliyokuwa ya Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Kazi,
Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maji na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa
Tanzania Bara, wakati Zanzibar zinatajwa Wizara ya Mawasiliano na
Uchukuzi na Wizara ya Maji.
Rada
Mwaka 2011 Serikali ilikumbwa na jinamizi la ufisadi kwa mara nyingine. Safari hii uliibuka ufisadi wa mabilioni ya shilingi kupitia ununuzi wa rada kuukuu kutoka Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza. Ununuzi wa rada hiyo unatajwa kutofuata taratibu sahihi, uliligharimu taifa Sh29.5 bilioni, wakati gharama halisi ilikuwa Sh21 bilioni.
Serikali ya Uingereza iliamua kurudisha fedha hizo
kama chenji, huku ikisisitiza kuwa watuhumiwa wote wa hapa nchini
waliohusika na ununuzi wa rada hiyo mtumba, washitakiwe Tanzania au
Uingereza kutokana na kubainika dosari kwenye ununuzi huo.
Wakati Uingereza ikitaka watuhumiwa hao wafikishwe
mahakamani, mtandao wa Wikileaks unaosifika kwa kufichua siri za ndani
ya mataifa mbalimbali duniani, ulibaini kuwepo kwa harakati nchini za
kutowafikisha mahakamani wahusika wa ufisadi huo.
EPA
Mwaka 2008 iliibuka kashfa nyingine ya wizi wa
mabilioni katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki
Kuu (BoT), ambapo vigogo kadhaa walitumia mbinu chafu kuchota zaidi ya
Sh133 bilioni katika akaunti hiyo.
Katika wizi huo ulioitikisa nchi, wahusika
walitajwa kutumia vivuli vya siasa katika kupitisha nyaraka bila
kufanyiwa uhakiki wa nyaraka hizo.
Richmond
Operesheni Tokomeza Ujangili
Mwaka 2006 baada ya Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani kulitokea tatizo kubwa la uhaba wa umeme.
Hapo ndipo Serikali ilipoanza kufanya mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafuta njia za dharura za kutatua tatizo hilo.
Waziri Mkuu wa wakati huo Edward Lowassa alikuwa
mstari wa mbele katika mikakati hiyo ndipo Kampuni ya Richmond
Development (LLC) ilipewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura na
kuliuzia Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Tanesco.
Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa kampuni hiyo
haikuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kama ilivyodhaniwa, badala yake
kulikuwa na michezo michafu iliyofanyika kwa masilahi ya wafanyabiashara
na baadhi ya viongozi wa Serikali.
Mwaka 2007, sakata hilo lilifika bungeni na
aliyekuwa Spika wakati huo, Samuel Sitta aliunda kamati iliyokuwa chini
ya mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ili kuchunguza suala hilo.
Kamati hiyo ilichunguza sakata hilo na kutoa
taarifa ilionyesha kuhusika kwa viongozi wa juu wa Serikali akiwemo
aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa na kusababisha kiongozi huyo,
kujiuzulu pamoja na mawaziri wawili kung’oka madarakani.
Waliong’oka madarakani ni mawaziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti, ambao ni Naziri Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha.
Operesheni Tokomeza Ujangili
Operesheni Tokomeza Ujangili iliyoanzishwa na
Serikali kupambana na ujangili wa wanyama nchini mwaka jana iliwang’oa
madarakani mawaziri wanne ambao wizara zao zilielezwa kushindwa
kusimamia vizuri utekelezaji wa operesheni hiyo.
Kung’oka kwa mawaziri hao kulitangazwa bungeni na
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyeeleza kuwa Rais Jakaya Kikwete ametengua
uteuzi wao baada ya kuwasiliana naye kwa mashauriano akiwa nchini
Marekani.
Mawaziri waliong’olewa kutokana na ripoti ya
kamati hiyo iliyoongezewa shinikizo na michango ya wabunge wengi ni
Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamisi Kagasheki na Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi. Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi, Dk Mathayo David Mathayo.
Operesheni hiyo inadaiwa kukiuka haki za binadamu
ikiwamo watu 13 na askari sita kuuawa, utesaji wa kutisha wa watuhumiwa,
ubakaji, rushwa na uporaji wa mali za wananchi.
Akaunti ya Esrow
Akaunti ya Esrow
Wakati kashfa ya Richmond haijasahaulika, mapema
mwaka huu imeibuka kashfa ya upotevu wa mamilioni ya fedha kwenye
Akaunti ya Esrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kashfa hiyo inayolitikisa Bunge na Serikali sasa,
imetajwa kuwa ni mwendelezo wa jinamizi la kashfa ikiwa ya saba kubwa
kulikumba taifa hadi sasa.
Akaunti hiyo iliyokuwa na zaidi ya Sh200 bilioni,
ilifunguliwa wakati kukiwa kuna mgogoro wa kisheria baini ya wabia wa
zamani wa IPTL (VIP Engeneering and Marketing na Mechmar Corporation ya
Malaysia) kwa upande mmoja, Tanesco na Independent Power Tanzania, IPT,
kwa upande mwingine.
Wadau kwenye akaunti hiyo hawakupaswa kuchukua
kitu chochote hadi pale mgogoro utakapotatuliwa. Hata hivyo, kitita
hicho cha fedha kilichotwa.
Wazungumza
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),
Emmanuel Mallya alisema matukio ya ufisadi yanaongezeka nchini kutokana
na Serikali kushindwa kuweka bayana hatua zinazopaswa kuchukuliwa watu
wanapatikana na makosa hayo, ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema kila mara wizi wa fedha za umma
unapotokea, Serikali hupata kigugumizi kuwawajibisha wahusika, hatua
inayowafanya watu wengi kuamini kushindwa kwao kunatokana na woga wa
kutekeleza azma zao.
“Hakuna uwajibikaji kama mtu kafanya jambo fulani,
kuna kulindana sana, lakini kama wote wangechukuliwa hatua za wazi
pengine ufisadi usingekuwa wa kiwango cha juu namna hii,” alisema.
Mhadhiri
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM)
Faraji Christoms, alishauri wenye dhamana ya kusimamia masilahi ya taifa
wanatakiwa kujitathmini upya.
Alitaja maeneo yanayohitajika kufanyiwa tathmini
kuwa ni uzalendo kwa taifa, elimu kwa maana ya uelewa wa mambo ya
kisheria, lugha za kimataifa na umakini wakati wa majadiliano ya
kimataifa na wanaposoma mikataba ya aina hiyo.
“Unakuta mtu badala ya kutuliza akili akasoma kwa makini mkataba
kabla ya kuusaini, anaupeleka kwa msaidizi wake ukisindikizwa na memo
(agizo la maandishi) “Please read carefully for advice,” (tafadhali soma
kwa makini, shauri),” alieleza Christoms.
Alisema katika mazingira hayo, hatima ya usalama wa mkataba huo unakuwa mikononi mwa mwingine, tofauti na aliyepewa dhamana.
Christoms alisema mazingira yanaonyesha kuwa
wanasheria serikalini wanashindwa na walioajiriwa kwenye kampuni za
uwakili, hivyo kusababisha Serikali kupata hasara kwa kuingia katika
mikataba isiyo na masilahi kwa taifa.
Profesa Gaudence Mpangala, wa Chuo Kikuu cha Ruaha
(RUCO) alisema historia ya ufisadi nchini inamnyima mtu yeyote makini,
ujasiri wa kuishauri Serikali mbinu za kudhibiti vitendo hivyo vya
rushwa.
Profesa Mpangala alisema vitendo vya rushwa
haviepukiki katika jamii, lakini Serikali inapochukua hatua
zinazothibitisha kuwa inavipiga vita, hali inakuwa shwari tofauti na
ilivyo nchini ambapo rushwa ndogo na ufisadi vimeota mizizi huku hatua
zinazochukuliwa zikiacha maswali mengi bila majibu.
Alitoa mfano wa serikali ya awamu ya kwanza,
ilivyoshughulikia rushwa iliyokuwa inaelekea kwenye ufisadi kwa kuchukua
hatua kali, chini ya hayati Edward Sokoine na Mwalimu Nyerere ambapo
waliothibitika kuhusika pamoja na adhabu ya kifungo jela, walitakiwa
kuchapwa viboko wakati wa kuingia na kutoka gerezani.MWANANCHI
Post a Comment