0

KUANZIA sasa, shule yoyote mpya isiyokuwa na maabara ya sayansi na maktaba haitasajiliwa na wala kuruhusiwa kutoa huduma; Serikali imeagiza. Wakati agizo hilo linagusa shule za Serikali pamoja na za binafsi zinazojengwa, kwa upande wa shule zilizopo ambazo hazina mahitaji hayo, unaandaliwa mkakati hatimaye zote ziwe na maabara na maktaba.

Akizungumza na mwandishi katika mahojiano maalumu, Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bharalusesa alisema hakuna usajili utakaotolewa kwa shule yoyote mpya bila kutimiza masharti hayo.

Hatua hiyo ya Serikali ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya elimu kuwezesha upatikanaji elimu bora na yenye viwango.

Kamishna huyo wa Elimu alisisitiza, “hii inatokana na agizo la Rais Jakaya Kikwete kwa shule zote mpya zinazojengwa kuhakikisha masharti haya yanatekelezwa, vinginevyo, shule husika hazitapewa usajili hata kidogo.”

Kwa mujibu wa Profesa Bharalusesa, maabara zinapaswa ziwe zimekamilika kwa kuwa na vifaa vyote vinavyohusu masomo ya Fizikia, Kemia na Bayolojia.

Vile vile kwa upande wa maktaba, maelekezo ya wizara ni kwamba lazima ziwe zimekamilika kwa ajili ya kuwezesha utoaji elimu yenye viwango.

Hivi karibuni, vyombo mbalimbali vya habari, viliripotiwa juu ya baadhi ya shule za serikali mkoani Arusha kushindwa kuanza muhula mpya wa masomo kutokana kutokidhi masharti ya kuwa na maabara na maktaba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, hivi karibuni aliliambia gazeti hili kwamba yako mabadiliko mengi yanayotarajiwa kufanyika katika sekta ya elimu.

Alisema mipango mbalimbali pamoja na sera zitaundwa kukidhi mahitaji hayo. Alisema mabadiliko hayo yatajitokeza kupitia Sera ya Elimu na Mfunzo inayopitiwa.

Kwa mujibu wa Profesa Mchome, kama mambo yatakwenda vizuri, sera hiyo itakuwa tayari mwakani na itatumika kutatua kasoro mbalimbali katika sekta ya elimu.HABARILEO

Post a Comment

 
Top