Freddy Macha
Majuma mawili yaliyopita, habari za mwanamke wa London aliyeoana na mbwa wake aitwaye Sheba zilitangazwa na gazeti la Metro.Metro
hutolewa bure, kila siku, kwa wasafiri miji mbalimbali ya Uingereza.
Baadaye mwanamke huyo Amanda Rodgers, alipohojiwa na ITV mjini London
alidai : “Nafahamu ndoa yangu na Sheba haitambuliki kisheria. Lakini
ilikuwa njia nzuri ya kuonyesha ninavyomthamini Sheba. Sheba amekuwa
nami miaka mingi, hunichekesha na kunifariji ninaposononeka. Sikuweza
kumpata mwenzi mwingine wa maisha kama huyu.”Sheba ni mbwa anayeongelewa na Amanda.Mwenzenu
alishachoka, baada ya kuishi na wanaume wawili, kuyeyushwa na uhusiano
pamoja na kero akaamua kufunga ndoa na mbwa wake.Mila
ya wafuga mbwa wa ndani tofauti na wale walindao nyumba hata
wanaosaidiana na polisi. Mbwa wa ndani hutunzwa kama sehemu ya familia,
hutunzwa na kupewa majina kama ndugu yeyote wa damu.
Hivyo, Sheba ambaye ni mbwa jike, alitimiza kanuni za mapenzi ambazo mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 47 alizihitaji.
Wanasaikolojia huuliza: Siri ya mapenzi ni nini?
Niambie wewe msomaji.
Siri ya fenesi la moyo nini?
Wimbo mmoja wa taarabu uliwahi kushauri zamani : “Ukipenda Pendeka...”
Amanda Rodgers ameshaishi miaka 47.
Miaka
arobaini na kitu kwa mwanadamu huitwa umri wa makamo kwa Kiswahili. Bado
uzee kushtadi hakika, bali kukomaa kimaisha; kupitia mengi hata ikibidi
kujaaliwa kajukuu. Lakini siyo wote tunaojaaliwa haya.
Hapa
uzunguni, ndoa zimefikia kilele cha ugumu siku hizi. Ugumu kiasi ambacho
ndoa za jinsia moja zinapigiwa madebe kukidhi haja.
Kihistoria
miaka 50 sasa uhuru na ukombozi wa akina mama umeleta maendeleo katika
uchaguzi wa kazi na taaluma, uhusiano na wanaume, malezi ya watoto,
kujiamini, kujituma na kadhalika. Hapo hapo maendeleo haya yameporomoka
kiuwiano.
Wanawake
wamekuwa wahitaji na wakali zaidi. Matokeo yake ndoa hazidumu. Wanaume
wanakimbia nyumba zao. Habari za baadhi ya midume kuzaa kisha kuua
watoto, mke na wao wenyewe zinazidi kuenea. Wanaoumia ni watoto.
Katika hali hii ngumu, unawakuta wachache wanaoamua bora kuoana na viumbe wengine kuliko wanadamu.
Kuna
habari za waliooana na nyoka, samaki, hata waliofunga ndoa na vitu
walivyovihusudu, mathalan madaraja hata viwanja vya kuchezea.
Yanachekesha, yanastaajabisha, yanakondesha, yanasikitisha.
Ila uhusiano mzuri kati ya mtu na mbwa ndiyo mbingu.
Mbwa ni
kiumbe anayethaminiwa sana Uzunguni. Nakumbuka mara yangu ya kwanza
kuzozana na utamaduni huu nilikuwa nikiishi Ujerumani mwaka 1985. Ongeza
sasa hizo nafasi ndogo za kufungiwa ndani, mbwa hukosa jaha.
Wanaojiweza huajiri watembeza mbwa, wanaotoza fedha kwa waliokwenda
kazini na kukosa nafasi kuwatembeza na kuwafanyisha mazoezi.
Hilo, moja.
Pili,
mbwa huyo wa jirani aliacha kinyesi chake pale mlangoni kwangu. Kila
nilipolalamika nilionekana eti nimejaza chuki. Ilitokea hata siku moja
mgeni wangu akakanyaga kinyesi cha mbwa. Zingatia harufu iliyokithiri na
matusi yaliyotutoka.
Nilipogomba nikaambiwa; “Ah nyinyi Waafrika mnachukia wanyama, mnatesa wanyama, hamna utamaduni wa elimu viumbe.”
Baada ya
malalamiko ya majuma kadhaa, kutosikilizwa na kupuuzwa, nikaamua sasa
kumvizia yule mbwa. Asubuhi moja wakati akijisetiri mlangoni nikamvizia
na tofali dogo (maana mawe hayapatikani ovyo miji ya Ulaya, nikambabua
vizuri. Kilio alichokitoa kilizagaa eneo lote lile. Magari yalisimama.
Wapita njia wakaduwaa.
Utadhani
nimeua. Pamoja na yale mavi kuwa ushahidi nikaandamwa. Simu ikapigwa
polisi, dakika kumi hazikupita, king’ora hicho. Askari watatu wakaja;
pingu mkononi, vigongo. Nikazolewa mkuku hadi kituoni.
“Akili zako ziko sawasawa?”
Nikaelezea hali mbaya ya kinyesi na kadhalika.
“Kwa nini hukuja kituoni kushtaki?”
Nikasema sikujua kama unatakiwa kumshtaki mbwa kwa kwenda haja kubwa.
“Unatakiwa ndiyo. Huo ni uchafu wa mazingira.”
Yote yalikuwa mapya kwangu. Nilizoea mengine, Afrika.
“Umefanya kosa la jinai. Umemdhuru kiumbe na mali ya mtu.”
Maneno
yalikuwa mengi. Lakini pamoja na ukali wao, sheria za nchi hizi zina
haki. Ukishtakiwa unapewa pia wakili. Wakili akatetea sijaishi sana
nchini. Nimezoea mazingira na utaratibu mwingine wa Bara la Afrika.
Sifahamu utaratibu.
Nikaonywa. Lakini ilibidi kuhama; kila nilipopita nilinyoshewa vidole kitongojini. Kampiga mbwa. Mtesa wanyama.
Mbwa,
paka na wanyama kwa jumla huheshimiwa zaidi. Siyo ajabu kwamba huyu
Amanda Rodgers akaamua kufunga nao pingu za maisha. Ukitazama video au
sinema zinazoonyeshwa katika mtandao wa You Tube utathibisha uhusiano
huo. Taswira za wanaume kwa wanawake wakipigana mabusu (midomoni) na
mbwa ni nyingi .
Kijana wa
miaka 19, Wayne Bryson alifikishwa mahakamani mapema mwezi huu kwa
kufanya ngono na mbwa wa mke wake. Mke anasema asingefahamu kilichokuwa
kikiendelea kama siyo jamaa kujipiga picha ya video katika simu yake.
Kisa
kilichojulikana zaidi duniani ni cha dada wa Kimarekani, Alyssa Rosales
aliyefanya ngono na mbwa kwa takriban dakika moja halafu akasambaza
video Facebook na You Tube. Baada ya malalamishi iliondolewa. Leo Alyssa
katajirika kutokana na tendo hili. Ukitaka kuitazama filamu kuna
malipo.
Lakini siyo Wazungu tu.
Video za Wakongo, Wakorea na Wachina wakichinja mbwa, kuwauza au kuwala kama kuku zimejazana You Tube.
Yote haya yanatueleza nini kuhusu maisha yetu ?
Je, mapya?
Sidhani.
Tangu zamani wanadamu tulikuwa na tabia ya kufanya vitendo viovu na
wanyama. Leo vyaonekana zaidi kutokana na uwazi na usambazaji haraka wa
habari. Vilevile siku hizi wanadamu hatuoni aibu kuelezea mambo yetu ya
undani, hadharani. Ni sura halisi ya maendeleo tuliyoyafikia.
Mwananchi
Post a Comment