Wiki hii
Bunge Maalumu la Katiba limeahirishwa, kupisha Bunge la Bajeti kuanza
vikao vyake vya bajeti kwa mwaka mpya wa fedha wa 2014/15.
Hata
hivyo, Bunge hilo limeahirishwa likiwa limegawanyika vipande, baada ya
wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje ya
Bunge hilo Aprili 16, wakipinga kejeli, matusi na mambo mengine ya
ukiukwaji wa taratibu yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya mawaziri nje ya
Bunge.
Kutoka
kwa Ukawa nje unaojumuisha vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, DP na
wajumbe 25 kutoka kundi la 201 hakukuzuia Bunge hilo kuendelea na vikao
vyake. Bunge hilo limeahirishwa Agosti 5, litakapokutana tena mjini
Dodoma kuendelea na majadala wa kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya
Katiba.
Kundi la
Tanzania Kwanza linalojumuisha wajumbe wengi wa CCM, wamekuwa wakiwapiga
vijembe kuwa warudi bungeni kuendelea na mjadala huo kwani Katiba
haitengenezwi nje ya Bunge.
Jukata yasaka suluhu
Kutokana
na mgawanyiko huo kuonyesha kuligawa taifa na kuwaacha wananchi wakiwa
njiapanda juu ya hatima ya kupata Katiba Mpya, Jukwaa la Katiba Tanzania
(Jukata) linajipambanua kutaka kusaka suluhu ya mvutano huo.
Mwenyekiti
wa Jukata, Deus Kibamba anasema, Jukwaa hilo linajitolea kusaka suluhu
kwa kuratibu maridhiano ya makundi yanayovutana ya Ukawa na la Tanzania
Kwanza.
Anasema
lengo la kusaka maridhiano hayo ni kuhakikisha kabla ya Bunge hilo
kuanza Agosti 5, kunakuwapo maridhiano, yatakayowezesha wajumbe wote
wanakuwa kitu kimoja katika kujadili maudhui ya rasimu, licha ya tofauti
zao za kiitikadi na kimisimamo.
Kibamba
anasema wameamua kuwaalika wataalamu ambao wana uzoefu wa siku nyingi
katika masuala ya sheria kusimamia maridhiano hayo, yatakayojenga umoja
na mshikamano katika taifa.
Wataalamu
hao kwa mujibu wa Kibamba ni Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Barnabas
Samatta anayekuwa mwenyekiti, Profesa Patrice Lumumba kutoka nchini
Kenya ambaye atakuwa msuluhishi mwenza sambamba na uwepo wa makundi ya
viongozi kutoka Ukawa, Tanzania Kwanza, vyama vya siasa, asasi za
wananchi na taasisi zote muhimu zilizoguswa na mchakato huu.
"Katika
kujenga Katiba yenye kuwajali wananchi, tunaomba kila upande kuridhia
kukutana na kutokuwa na misimamo mikali ili kuhakikisha tunawaunganisha
na kuendelea na mchakato huo kama kawaida," anasema Kimbamba.
Kuhusu
uhalali wa Bunge hilo kuendelea na mijadala licha ya Ukawa kutoka nje,
anasema sheria za Jumuiya ya Madola kwa mabunge ya Katiba kundi moja
linapotoka nje kwa tamko, Bunge hilo hutakiwa kusitishwa."Ukawa wametoka
nje tena wakiwa zaidi ya 190, Bunge lilitakiwa kusitishwa na kupata
maridhiano kwanza si kama wanavyotumia akidi vibaya kuliendesha Bunge
hilo," anasema Kibamba.
Aliongeza:
"Jukata bado inaamini kwamba mwaka 2014 Katiba Mpya haitapatikana,
hivyo kunahitajika kufanyiwa marekebisho makubwa Katiba ya sasa hasa
vifungu vinavyohusu uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika
kwa amani."
Maoni ya wadau
Katibu
Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania, Felician
Mkude anasema, maridhiano yanahitajika ili kuweza kupata uwakilishi
ndani ya Bunge hilo kwa ufasaha.
Anasema,
kuendelea na mvutano kuhusu aina gani ya Muungano, si jambo la maana na
kinachotakiwa kufanyika ni wananchi kupiga kura ya muundo gani
unaostahili.
"Huwezi
kuwalazimisha watu kuamua jambo ambalo hawalitaki kama ni muundo wa
Muungano tunaomba wananchi ndiyo waamue, lakini yote hayo Katiba yetu
inatakiwa kubainisha mambo mbalimbali yanayohusu watu wenye ulemavu na
haki zao zote," anasema Mkude.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Idd Makombe anasema mvutano uliokuwa
ukiendelea bungeni kuhusu muundo wa Muungano haukuuimarisha bali
unauvuruga.
Dk Makombe anasema, uwazi na maridhiano ndio utakaowezesha kuipata Katiba Mpya yenye kuwajali Watanzania wote.
"Kunahitajika
kufanyika kwa kura ya maoni kuhusiana aina gani ya Muungano wananchi
wanataka, kwani hivi sasa watu hatuaminiani na huwezi kumlazimisha mtu
jambo ambalo halitaki, hivyo pande zote mbili zifikie maridhiano kwa
amani," anasema Dk Makombe.
Mhadhiri
wa Chuo Kiuu cha Dar es Salaam, Idara ya Sayansi na Utawala, Richard
Mbunda anasema nchi inapitia katika kipindi kigumu kutokana na kauli na
mienendo mbalimbali inayoendelea kujitokeza.
Mbunda
anasema viongozi wa kidini na Serikali wanapotoa kauli wanatakiwa kuwa
makini, kwani zinaweza kuliingiza taifa katika vurugu za kidini au za
kisiasa.
Kauli ya
Rais KikweteAkizungumza na Vijana na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi kutoka
Tanzania Bara na Visiwani juzi kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba, Dar es
Salaam, Rais Jakaya Kikwete amewataka Ukawa kurejea bungeni kuendelea na
mjadala wa kutunga Katiba.
Jukwaa la
Katiba Tanzania (Jukata), limeingilia kati mpasuko uliojitokeza katika
Bunge Maalumu la Katiba kwa kusaka wasuluhishi watakaorejesha maridhiano
ya pande mbili zinazokinzana.
Rais
Kikwete anasema, katika kuandika Katiba ya Watanzania kunahitajika
kufanya maridhiano ili kuhakikisha mchakato huo unamalizika salama kwa
wananchi kupata Katiba yenye kujali masilahi yao.
CHANZO MWANANCHI
Post a Comment