Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli leo anatarajiwa kuwakabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Simba SC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kabla ya mchezo wao na Kagera Sugar ya Bukoba.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Mario Ndimbo, Rais Magufuli atawasili Uwanja wa Taifa Saa 8:00 na kukagua timu kabla ya mchezo kuanza Saa 8:15 na baada ya hapo atakabidhi Kombe kwa mabingwa, Simba SC.
Awali ya hapo, Rais Magufuli atapokea Kombe la ubingwa wa michuano ya Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 (CECAFA U17), ambalo Tanzania ilitwaa mapema mwezi huu nchini Burundi.
Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli leo anatarajiwa kuwakabidhi Kombe Simba SC Uwanja wa Taifa
Uwanja wa Taifa leo, unatarajiwa kusheheni pande zote mashabiki wa Simba wakijitokeza kushuhudia timu yao inakabidhiwa taji la kwanza la ubingwa wa ligi tangu mwaka 2012.
Simba SC inataka kuendeleza rekodi yake ya kutopoteza mechi leo ikimenyana na Kagera Sugar katika mchezo wake wa 29 wa Ligi Kuu, wakitoka kushinda mechi 20 na kutoa sare nane.
Simba walitambulika kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Mei 10 baada ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC kufungwa 2-0 na Tanzania Prisons mjini Mbeya kabla ya Wekundu hao wa Msimbazi kwenda kujiridhisha kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Singida United Jumamosi iliyopita Uwanja wa Namfua mjini Singida.
Simba SC wenye pointi 68 za mechi 28, baada ya mchezo wa leo watakwenda kukamilisha msimu wa Ligi Kuu kwa mchezo dhidi ya Maji Maji mjini Songea mkoani Ruvuma.
Post a Comment