0
Waziri wa Kilimo, Eng Charles Tizeba akizindua msimu wa ununuzi pamba mwaka 2018/19 wilayani Igunga. 

Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba ametangaza bei elekezi ya kununulia pamba msimu huu wa 2018/19 kuwa shilingi 1,100/= kwa kilo moja ya pamba mbegu. Akiongea katika siku ya ufunguzi wa msimu wa ununuzi wilayani Igunga tarehe 1/5/2018 Mhe. 

Tizeba amesema, “Msimu huu bei ya pamba itakuwa shilingi 1,100/= kwa kilo moja kutokana na bei katika soko la dunia kuwa haziridhishi, na kwamba bado pamba yetu nyingi inauzwa nje ikiwa ghafi hali inayotufanya tuwe tegemezi kwenye suala la bei, lakini Serikali iko katika mchakato wa kuhamasisha maendeleo ya Viwanda vya nguo nchini hali hii itaboresha bei ya pamba nchini” Aliongeza kusema kwamba, ili kumpunguzia mkulima mzigo wa madeni ya pembejeo na makali ya bei kushuka kwa shilingi mia kutoka ile ya msimu uliopita, Serikali imeamua kulibeba deni la zaidi ya shilini bilioni 30 la viuadudu ambavyo wakulima walikopeshwa msimu huu ili kuwafanya wakulima waweze kunufaika na kilimo chao. 

Aidha kuanzia msimu ujao wa kilimo, wakulima watapatiwa pembejeo zote ambazo ni mbegu za kupanda, kamba za kupandia na viuadudu bure bila kulipia gharama yoyote. Akifafanua kuhusu mchakato wa bei, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Marco Mtunga alisema; bei elekezi ya pamba inasimamiwa kwa sheria ya Pamba Na.2 ya mwaka 2001, ambayo inaelekeza kwamba kabla ya msimu wa ununuzi wa pamba kuanza lazima wadau wa msingi wa zao la pamba wakutane na kukubaliana juu ya bei. Hili limewekwa ili kuwa na mazingira ya ushindani wa haki katika biashara ya pamba na kulinda maslahi ya wakulima.

 “Kwa mujibu wa sheria ya Pamba Na. 2 ya mwaka 2001, Bodi ya Pamba ambayo ndiyo msimamizi wa tasnia ya pamba inaitisha kikao cha kujadili na kukubaliana kuhusu bei elekezi ya kununulia pamba kabla ya kuanza kwa msimu. Wadau wa msingi katika kikao cha bei ni wakulima wanaowakilishwa na Vyama vya Ushirika, Wanunuzi wa Pamba, Wizara ya Kilimo, Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Pamba na Bodi ya Pamba inayosimamia mchakato mzima. Vigezo vya msingi vinavyozingatiwa katika mchakato wa kupata bei elekezi ni pamoja na bei ya pamba nyuzi katika soko la dunia, gharama za ununuzi na uchambuaji wa pamba, ushuru wa Serikali na bei ya mbegu za kukamua mafuta”. 

Alisema Mtunga Pamoja na bei elekezi ya msimu huu kushuka kwa kiasi cha shilingi 100 ikilinganishwa na msimu uliopita, lakini ukweli ni kwamba msimu uliopita wafanyabiashara wengi walishindwa kufanyabiashara ya pamba kutokana na gharama kuwa kubwa hali ambayo ilifanya wakulima kukaa na pamba yao kwa muda mrefu sana bila kupata soko. Kwa makisio ya uzalishaji wa tani 600,000 msimu huu ambao ni ongezeko la zaidi ya asilimia 400 kutoka tani 132,000 za msimu uliopita, hatua za makusudi lazima ziangaliwe ili kuhakikisha mkulima hakosi soko; hii ni pamoja na kuwa na bei ambayo ni rafiki kwa pande zote za mnunuzi na mkulima.

 “kumekuwa na ongezeko kubwa sana la eno la uzalishaji wa pamba msimu huu kutoka ekari 650,000 msimu uliopita hadi ekari 3,000,000 msimu huu ambazo zimepandwa tani 26,500 za mbegu. Ongezeko hili linamaanisha onezeko pia la pato la mkulima mmoja mmoja” alisema Mtunga. Akifafanua kuhusu mfumo wa ununuzi wa pamba, Mtunga alisema, pamba yote ya wakulima itanunuliwa kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS). 

Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Vyama vya Ushirika na Mrajisi wa Ushirika wanawajibika kusimamia zoezi la ununuzi na kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati. Fedha za wakulima baada ya kuuza pamba zitalipwa kupitia akaunti za benki za wakulima ndani ya siku tatu baada ya mkulima kuuza pamba yake kwenye Chama cha Msingi. Wanunuzi wote wanawajika kununua pamba kutoka kwenye Vyama vya Msingi na siyo kwa wakulima.

 Aidha mnunuzi atalipa chama cha msingi asilimia tatu (3%) ya ushuru kama gharama ya ununuzi wa pamba. Mchakato wa kuanzisha vituo vya ununuzi chini ya AMCOS sanjari na kutoa elimu ya ushirika na matumizi sahihi ya mizani ya digiti unaendelea katika maeneo yote inakozalishwa pamba. Wakala wa Vipimo (WMA) watasimamia suala la mizani kuhakikisha inafanya kazi inavyostahili. 

 “Bodi ya Pamba itaendelea kusimamia ununuzi katika AMCOS kuhakikisha biashara inafanyika kwa uwazi na haki, wakulima wanalipwa kwa wakati na uzingatiaji wa sheria za ununuzi wa pamba pamoja na usafi na ubora wa pamba” alisema Mtunga na kuongeza kwamba; usafi na ubora wa pamba ni suala ambalo linapewa kipaumbele kikubwa kwa sababu uchafu kwenye pamba unaathiri ubora na sifa ya pamba katika soko la dunia. 

Wakulima na wanunuzi wanajibu wa kutunza ubora wa pamba. Utafiti unaonesha kwamba kuongezeka kwa tija katika kilimo cha pamba kutamuongezea mkulima kipato zaidi kuliko ongezeko la bei, hali ambayo iliifanya Bodi ya Pamba kuwekeza katika utoaji wa elimu ya Kanuni Kumi za Kilimo Bora cha Pamba hasa upandaji wa pamba kwa mistari. Msimu uliopita wilaya zaidi ya 13 zilipatiwa kamba za kupandia pamba zilizowekewa vipimo ambazo ziligawiwa bure kwa wakulima; msimu ujao Bodi ya Pamba inatarajia kugawa kamba katika maeneo yote yanayolimwa pamba. 

Katika msimu ujao wa kilimo 2018/19, wakulima wote watapanda mbegu aina ya UKM08 ambayo imeidhinishwa; mbegu hii kwa mujibu wa utafiti itamwongezea mkulima tija kwa zaidi ya asilimia 25 kwa sababu inaukinzani na magonjwa ya pamba ambayo ni Mnyauko Fuzari na Bakabakteria, pia ina uwiano mkubwa wa nyuzi ikilinganishwa na aina nyingine za mbegu hususan UK91. 

Ili kufikia uchumi wa kati na viwanda, Serikali inahamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda vya nguo nchini ili pamba yetu iwezekuongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi na kuongeza bei ya pamba kwa mkulima. Pamba inazalishwa katika mikoa 17 nchini ambayo ni Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Mara, Kagera, Tabora, Singida, Kigoma, Katavi, Dodoma, Morogoro, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Iringa.

Post a Comment

 
Top