Abiria 54 waliokuwa wakisafiri kwa mashua kutoka Shimoni, Mombasa nchini Kenya kuelekea Kisiwa cha Pemba wanadai kutelekezwa jijini Tanga baada ya kukamatwa na watu waliokuwa kwenye meli kubwa katika Bahari ya Hindi.
Abiria hao waliachwa nje ya jengo la Kikosi cha Majini cha Jeshi la Polisi (Polisi Marine) kilichopo jijini hapa, jana.
Wakizungumza na Mwananchi, walisema ‘walitekwa’ juzi na watu waliokuwa katika meli kubwa ya kijeshi ambayo ilikuwa na askari Waafrika na Wazungu.
“Baada ya kukamilisha ugongaji wa paspoti zetu za kusafiria tulianza safari katika Bandari ya Shimoni, Kenya kuelekea Wete Pemba, lakini wakati tukikaribia kufika Bandari ya Wete ilitufuata meli kubwa ya kijeshi na waliokuwamo melini humo walimwamuru nahodha ateremshe bendera na atii amri yao,” alisema Hamad Said Nassoro (37), mmoja wa abiria aliyekuwa katika mashua hiyo.
Alisema askari hao waliiamuru boti waliyokuwa wakisafiria kugeuza kuelekea Tanga kwa madai kwamba huko walikokuwa wanakwenda hakuna Serikali ni bora wapelekwe Tanga.
“Tukiwa na watoto wetu, tulipokaribia kufika Tanga meli ile kubwa ya kijeshi ilitia nanga na ikaja boti ndogo kutuchukua na kutuweka hapa nje ya Kituo cha Polisi Marine bila kutueleza kama ni wakosaji au vipi,” alilalamika Time Ramadhani Bakari (37).
Time alisema walifikishwa katika jengo hilo la polisi wa majini juzi saa saba mchana na hadi jana hawakuelezwa chochote.
“Hapa tulipo tumelala hapahapa na tuna njaa kali, watoto wanahangaika, tunaiomba Serikali iturejeshe kwetu Pemba kama inaona hatuna makosa na kama tuna makosa ni vyema tufunguliwe mashtaka kuliko tunavyofanyiwa,” alisema Habiba Salim (17).
Abiria hao walisema hawajui hasa kama meli ‘iliyowateka ni ya Tanzania au ya nchi gani kwa sababu ndani yake walikuwemo Waafrika na Wazungu.
Abiria hao walisema wao hufanya shughuli zao Mombasa na kila mwaka unapokaribia mwezi wa Ramadhani hurejea nyumbani Pemba kwa ajili ya maandalizi ya ibada ya kufunga.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema jeshi hilo linafuatilia tukio hilo ili kujua waliowakamata watu hao na ni kwa sababu zipi.
“Niseme tu kwamba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola tunafuatilia suala hili ili kujua kama ukamatwaji wao ulikuwaje na nani walihusika kuwakamata, kisha nitatolea maelezo lakini kwa sasa subirini kwanza,” Kamanda Bukombe aliwaambia wanahabari jana.
Mpaka jana jioni abiria hao walikuwa katika kituo hicho cha polisi wakiwa hawajui iwapo watasafirishwa kurudi Pemba au la. Pia walilalamika kukosa chakula tangu siku waliyotekwa na kwamba, hali za watoto ni mbaya.
Na Burhani Yakub, Mwananchi
Post a Comment