0
Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi imezinduliwa rasmi mjini Dar es Salaam, ikishuhudiwa na wadau mbalimbali wa sekta ya Ardhi.

Akizindua Mfuko huo kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe. William Lukuvi; Naibu Katibu Mkuu; Dkt. Moses Kusiluka alisema, Mfuko wa Fidia ya Ardhi umeanzishwa kwa mujibu wa Kanuni zilizoundwa chini ya Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 kwa lengo la kuondoa kero za ulipaji wa fidia katika utwaaji wa Ardhi. 

Kuundwa kwa Mfuko huu ni hatua mojawapo muhimu sana katika kuiwezesha Serikali kutekeleza kwa ufanisi zaidi matakwa ya Sera ya Ardhi na sheria zake, hususan katika ulipaji wa fidia pindi ardhi inapotwaaliwa kwa manufaa ya umma.

Dkt. Kusiluka alisema; Bodi hii inatarajiwa kufanya kazi kwa karibu sana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi, Mthamini Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Alisema; “Mkitekeleza majukumu yenu kwa ufanisi mtaisadia sana Serikali kukidhi matarajio ya wananchi katika kuwaletea maendeleo na kuwaondolea kero. Hivyo, ni imani yangu kwamba mtatumia weledi wenu katika kutekeleza majukumu yenu”.

Aidha, Dkt. Kusiluka alitoa wito kwa taasisi zote kuhakikisha kuwa mipango yote ya utwaaji wa ardhi inazingatia matakwa ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo. Aliendelea kusema kuwa ni matarajio ya Serikali kuwa taasisi zake zote zitafanya kazi kwa karibu na Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi.

Naye, mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko; Bwn. Martin Madekwe alisema kuwa anashukuru kukabidhiwa nafasi ya uenyekiti katika Bodi hiyo na kuwa anatambua kuwa Bodi anayoiongoza inategemewa kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu Mkuu. Alisema; “ Bodi tumejipanga kufanya kazi kwa ufanisi, uwazi, ueledi na uadilifu na tutajitahidi kuzingatia kuwa wale wote wapaswao kufidiwa, wanafidiwa ipaswavyo”.

Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi, inaoongozwa na Mwenyekiti Madekwe, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Katibu wake ni; Grace Gulinja, ambaye ni Afisa Ardhi Mkuu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akisoma Hotuba ya Waziri wa Ardhi; Mhe. William Lukuvi akiwa amemwakilisha katika Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi. Kulia kwake ni Kaimu Kamishna wa Ardhi Msaidizi ( Mijini), Paul Luge na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo; Bwn. Martin Madekwe.
Wajumbe wa Mkutano wa Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi wakisikiliza Hotuba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Mhe.William Lukuvi katika Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi.
Kanali Mstaafu; Joseph Simbakalia, aliyewahikuwa Mkuu wa Mkoa Kigoma, mmoja wa wajumbe katika Mkutano wa Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi akionekana kwa karibu akifuatilia kwa Makini Hotuba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi katika Uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Fidia ya Ardhi.

Post a Comment

 
Top