Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akitoa maelekezo katika ziara ya kukagua ujenzi wa jengo jipya 'One Stop Centre' la Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) lililopo bandarini leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Eng. Deusdedit Kakoko na Naibu Mkurugenzi wa TPA (Miundombinu), Eng. Karim Mattaka wakimsikiliza.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), kuhakikisha kazi ya kukamilisha ujenzi wa jengo jipya 'One Stop Centre' inakamilika haraka na kuanza kutoa huduma kwa mamlaka hiyo na wadau wake wote.
Akizungumza mara baada ya kukagua jengo hilo leo jijini Dar es Salaam, Prof. Mbarawa amesema ufanisi wa bandari ya Dar es Salaam utafikiwa pale wadau wote wa bandari hiyo watakapofanya kazi saa 24 na katika eneo moja ili kumrahisishia mteja kupata huduma kwa haraka na katika kiwango kinachokubalika kimataifa.
"Natoa miezi sita kuanzia leo kwa TPA msimamieni mkandarasi kikamilifu ili ikifika Juni muwe mmehamia ninyi na wadau wenu wote katika jengo hili," alisititiza Prof. Mbarawa katika ziara hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Eng. Deusdedit Kakoko amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa katika kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati tayari yeye amehamia kwenye jengo hilo, ili kuongeza hamasa kwa mkandarasi kukamilisha ujenzi wake.
"Tumejipanga ifikapo mwezi wa nne ofisi zote zitakazotumiwa na wadau wa bandari ziwe zimekamilika ili kuruhusu baadhi ya ofisi kuanza kuhamia katika jengo hili," amesema Eng. Kakoko.
Jengo hilo la kisasa lenye ghorofa 36 ambalo litawaweka wadau wote wa bandari mahali pamoja ili kurahisisha huduma kwa wateja litagharimu takribani shilingi bilioni 143 litakapokamilika mwezi Juni mwaka huu na kutoa fursa kubwa ya uwekezaji kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua huduma za Kivuko cha Magogoni na kuwataka wasimamizi wa kivuko hicho kuondoa wafanyabiashara na ombaomba ndani ya eneo la kivuko ili kuboresha usalama na kupunguza kero kwa abiria na madereva, na kuwataka abiria kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira waingiapo na watokapo katika eneo la kivuko.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Post a Comment