Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imeuagiza Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kuwafutia hati ya umiliki ardhi wawekezaji walio ndani ya Kiwanja cha Ndege cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere cha jijini Dar es salaam wakiwemo Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy na kampuni ya ukodishaji ndege ndogo ya Tanzania Air, sambamba na kutoa siku 30 kwa Mamlaka hiyo kuwaondoa mara moja wakazi 59 waliojenga ndani ya hifadhi ya Uwanja huo ili kupisha upanuzi wa Uwanja.
Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya ukaguzi katika Kiwanja hicho na kushangazwa na hali ya makampuni hayo na wananchi kuwa na hati ya umuliki ardhi ambayo tayari ni mali ya Kiwanja cha Mwalimu Nyerere, huku akiwagiza TAA kuweka uzio katika viwanja vyote vya ndege nchini ili kuzui uvamizi wa ardhi unaofanywa na wananchi.
Aidha, Naibu Waziri huyo ameagiza TAA kuweka mtu wa kusimamia mafuta ya ndege yanayoingizwa Kiwanjani hapo kutoka Kampuni inayotoa huduma ya mafuta ya Ndege ya Puma Energy baada ya kubaini kuwepo na usimamizi mbovu ambao unaweza kuisababishia hasara Serikali.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TAA Richard Mayongela amekiri kuwepo kwa changamoto ya kuvamiwa kwa mipaka ya Viwanja vya Ndege na wananchi na kuahidi kuifanyia kazi suala hilo haraka.
Post a Comment