SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefanya mazungumzo na uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika mpango wa kuviboresha viwanja vya chama hicho tawala vinavyotumika kwa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jana mjini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema kwamba taarifa rasmi juu ya waliokubaliana katika kikao hicho itatolewa baadaye na wahusika.
“Mimi nilikuwa ninataka nikuambie jitihada zetu katika kuhakikisha tunaboresha Ligi Kuu, tumeanza na suala la viwanja kwa kuzungumza na wamiliki wa viwanja ili kukubaliana tuviboreshe viwe katika kiwango kizuri,”alisema.
Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao amesema wamefanya mazungumzo na uongozi wa CCM katika mpango wa kuviboresha viwanja vinavyotumika kwa Ligi Kuu
Kidao alisema mbali na CCM, pia wamefanya mazungumzo na wamiliki wa viwanja vingine nchini vinavyotumika kwa michezo ya Ligi Kuu, ambo ni Serikali wenye Uwanja wa Taifa na Uhuru na Azam FC wenye Uwanja wa Azam Complex.
Amesema vilikuwa vikao vizuri na walifikia makubaliano mazuri ambayo mara moja yanaanza kufanyiwa kazi katika kuhakikisha Ligi Kuu inachezwa kwenye viwanja bora.
Aidha, Kidao ambaye ni kiungo wa zamani wa Milambo FC ya Tabora na Simba SC na Vijana ‘Kabakayeka’ za Dar es Salam, amesema TFF inaridhishwa na mwenendo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoendelea hivi sasa nchini kutokana na ushindani kuongezeka, hususan baada ya kupanda kwa Singda United
“Kama ambavyo unavyoweza Ligi ni ya ushindani, hata ukiangalia msimamo pale juu, timu tatu zinazofuatana zinalingana kwa pointi. Na hata timu nyingine katika msimamo hazitofautiani sana,”amesema.
Pamoja na hayo, Kidao amesema bado kuna mapungufu madogo ikiwemo uchezeshaji mbovu wa marefa, lakini akasema nayo yanafanyiwa kazi.
Post a Comment