0
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga kuhusu kufanya juhudi ya kukusanya mapato ili azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kikamilifu itimie.Meneja wa Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Shinyanga, Bw. Jumbe Samson (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ikiwemo ukusanyaji wa mapato ya Mkoa wake kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika mkoa huo.Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipokuwa akizungumzia umuhimu wa watumishi wa Mamlaka hayo kote nchini kuzingatia  maadili ya kazi zao, alipofanya ziara ya kikazi katika mkoa huo.
Na. Mwandishi Wetu, Shinyanga
Serikali inatarajia kuajiri wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika Mamlaka hayo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na makusanyo ya kodi.
Ahadi hiyo imetolewa Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji wa Mamlaka hayo mkoani humo.
Dkt. Kijaji amesema kuwa taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.
“Tunatambua changamoto ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ndio maana tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine ili tuweze kuimarisha utendajikazi wa Mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini”alisema Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa pamoja na uhaba wa watumishi, anaamini kuwa lengo la mwaka huu la kukusanya shilingi trilioni 17 ambazo Mamlaka hayo imepangiwa yatafikiwa na ikiwezekana kuzidi kwa kutumia wafanyakazi waliopo.
Dkt. Kijaji alitoa rai kwa wafanyakazi wa TRA kuwa waadilifu na kwamba atakayebainika kukiuka maadili yake ya kazi atachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria.
Awali Meneja wa Mamlaka ya Mapato mkoa wa Shinyanga Bw. Jumbe Samson, alieleza kuwa mkoa wake umepangiwa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 18 na kwamba wanauhakika wa kufikia lengo hilo kutokana na mikakati mbalimbali waliyojipangia ikiwemo kusimamia ukusanyaji kodi kikamilifu katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA Bw. Beatus Nchota alisema kuwa Mamlaka yake imejiwekea mipango ya kufungua ofisi zake kila wilaya hapa nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili lengo walilopewa la kukusanya shilingi trilioni 17 liweze kufikiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Josephine Matiro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, alisema kuwa Serikali mkoani humo itahakikisha kuwa TRA inatimiza malengo yake ya kukusanya kodi na kumhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji kwamba watasimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Post a Comment

 
Top