Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya TEHAMA toka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Baltazar Kibola akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma kuhusu uzinduzi wa mfumo wa kielektroniki wa kuandaa Mipango,Bajeti na kutoa Ripoti za Malaka ya Serikali za Mitaa utakaozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Septemba 5,2017 mjini Dodoma kulia ni Mkuu wa Timu ya Rasilimali Fedha kutoka mradi wa PS3 Dkt. Gemini Mtei na kushoto ni Mtaalamu kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Elisa Rwamiago.
Mkuu wa Timu ya Rasilimali Fedha kutoka mradi wa PS3 Dkt. Gemini Mtei akizungumzia faida za mfumo huo wakati wa mkutano na vyombo vya habari leo mjini Dodoma. Kushoto ni.Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya TEHAMA toka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Baltazar Kibola.
Mmoja wa Wataalamu kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI bw. Elisa Rwamiago akiongea wakati wa mkutano na waandishi wa Habari leo mjini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya TEHAMA toka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Baltazar Kibola.(Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo ,Dodoma
Na Beatrice Lyimo- MAELEZO,DODOMA.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa anatarajiwa kuzindua mfumo wa kielektoniki wa kuandaa Mipango , Bajeti na Ripoti kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa(PlanRep) na Mfumo wa Uhasibu wa Utoaji wa Taarifa za Fedha kwenye Vituo vya Kutolea Taarifa(FFARS).
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma, Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia masuala ya TEHAMA Ofisi ya Rais – TAMISEMI Baltazar Kibola amesema kuwa mifumo hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Septemba 5, 2017 katika ukumbi wa LAPF Mkoani Dodoma.
Akifafanua Bw. Kibola alisema kuwa lengo la mifumo hiyo ni kusaidia kuja na mfumo mmoja wa kitaifa utakaowezesha kuwa na utaratibu wa kuandaa mpango na bajeti ambapo utasaidia Hamlashauri zote nchini kuwa na muundo mmoja wa uandaaji wa mipango na Bajeti za Serikali.
Aidha alisema kuwa lengo la Mradi wa uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ni kushirikiana na Serikali katika kuimarisha mfumo ili kusaidia uandaaji wa Mipango na Bajeti katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika ngazi ya kila kituo husika.
Kwa upande wake Mkuu wa Timu ya Rasilimali Fedha kutoka Mradi wa uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) Dkt. Gemin Mtei alisema kuwa lengo la mradi huo ni kufanya maboresho ya mifumo katika Sekta za Umma ili kuongeza ufanisi.
“Mradi huu unalenga kufanya maboresho katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la Utawala Bora, Rasilimali watu, Rasilimali Fedha na pia katika maeneo ya TEHAMA ambapo utasaidia ni namna gani mifumo inawezeshwa kufanya kazi kwa urahisi” amesema Dkt. Mtei.
Aidha Dkt. Mtei amebainisha baadhi ya maeneo yaliyolengwa kufanyiwa maboresho ikiwemo utoaji wa huduma, kutambua watoa huduma na pia kuwekeza kwa watoa huduma ili kuwezesha wananchi kuweza kunufaika na huduma hizo.
Vile vile Dkt. Meti alisema kuwa Mfumo wa kielektroniki (PlanRep) iliyoboreshwa na Mfumo wa Uhasibu wa Utoaji wa Taarifa za Fedha kwenye Vituo vya Kutolea Taarifa(FFARS) Mradi wa (PS3) ikiwa ni mradi wa miaka mitano (2015 – 2020) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa (USAID) kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania.
Naye Mtaalamu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Elisa Rwamiago amesema kuwa mfumo umeundwa kwa kuzingatia Ubora, Usimamizi wa fedha, ufanisi katika utendaji kazi wa umma, kupunguza gharama za usimamizi na utendaji wa kazi.
“Mfumo uliokuwa ukitumika awali ulitumia gharama nyingi, muda mwingi na pia ulihusisha watu wengi kukaa kusafiri kukaa pamoja sehemu moja, ila mfumo huu ulioboreshwa umerahisisha utendaji kazi na kupunguza gharama iliyokuwa ikitumika awali” amesema Rwamiago
Akibainisha faida za mifumo hiyo kwa Serikali Rwamiago amesema kuwa itawezesha ufuatiliaji kuanzia ngazi za vituo vya Afya, Zahanati na shule hivyo utawezesha upatikanaji wa taarifa kutoka katika kila kituo kwa wakati.
Vilevile amesema kuwa mifumo hiyo ina manufaa katika ngazi zote za utendaji hivyo itasidia uunganishaji wa Taarifa kuhusu fedha za Serikali kutoka katika ngazi ya vituo hadi Halmashauri mpaka ngazi ya Taifa.
“Mifumo hiyo imeandaliwa katika ubora kwa kuzingatia changamoto zilizokuwepo awali kwa lengo la kuleta ufanisi katika utekelezaji wa kazi za Serikali” alifafanua Rwamiago.
Mradi wa uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) ni mradi uliounganisha Mikoa yote ya Tanzania na Halmashauri zake ambapo wataalamu wa masuala ya Mipango, Bajeti,Waganga wakuu wa Wilaya, Makatibu Afya, Mweka Hazina kutoka katika kila Halmashauri wamepatiwa mafunzo kuhusu Mifumo hiyo.
Post a Comment