Wape ng’ombe wako lishe kamili, yenye nguvu, protini, na vitamin pamoja na maji ya kutosha. Kulisha ng’ombe kwa kutumia aina yoyote ya malisho haitoshi kukuhakikishia ng’ombe anakuwa na afya nzuri na kutoa maziwa ya kutosha. Kama ilivyo kwa binadamu, ng’ombe anahitaji mlo kamili. Malisho ni lazima yawe na uwiano sahihi wa viungo.
Mifugo inahitaji chakula kitakachowapa nguvu, protini, madini, na vitamin ili kujenga miili yao, kuzalisha maziwa, na kuzaliana. Wanyama wadogo wanahitaji virutubisho vya kutosha, ili wakuwe na kuongeza uzito. Ng’ombe wa maziwa wanahitaji virutubisho zaidi ili kuweza kuzalisha maziwa kwa wingi hasa katika kipindi cha miezi 3-4 ya mwanzo baada ya kuzaa, wakati ambao uzalishaji wa maziwa unakuwa juu.
Malisho ya kijani ni mlo mkuu kwa mifugo
Mlo muhimu na wenye virutubisho kwa mifugo ni majani. Lakini malisho bora ya kijani ni yale yanayoweza kumpatia ng’ombe wa maziwa virutubisho muhimu vinavyohitajika. Malisho bora yanakuwa na sifa mbili muhimu: ni ya kijani kibichi na machanga hii ina maana kuwa, majani ya malisho ni lazima yakatwe na kuhifadhiwa yakiwa bado machanga na kabla ya kuchanua.
Ni lazima mfugaji afahamu kuwa mimea ambayo imepoteza rangi yake halisi ya kijani inaweza tu kuwasaidia mifugo kuishi lakini haina virutubisho muhimu vya kuwapa mifugo nguvu, madini, protini na haiwezi kusaidia katika uzalishaji wa maziwa. Malisho yenye viwango vya chini vya virutubisho ni lazima yaongezewe kwa chakula cha ziada chenye virutubisho vya kutosha kitakachoziba pengo la virutubisho vilivyokosekana.
Vyakula vya kutia nguvu
Aina zote za majani ni chanzo kizuri cha vyakula vya kutia nguvu kwa mifugo, endapo tu yatalishwa yakiwa bado machanga. Majani yaliyo maarufu kwa malisho ni pamoja na matete, ukoka, majani ya tembo, seteria na Guatemala. Majani ya mahindi au mtama ni chakula kizuri sana kwa kuwapa nguvu mifugo. Vyakula vya kutia nguvu vilishwe kwa kiasi kidogo. Vyakula hivi vinaweza kutokana na aina zote za nafaka, punje za ngano, au molasesi.
Vyanzo vya Protini
Kanuni ya 1:
Mimea michanga ina kiasi kikubwa cha protini kuliko mimea iliyokomaa. Mahindi machanga pamoja na majani ya viazi vitamu ni mahususi kwa protini.
Kanuni ya 2:
Mikunde ina protini nyingi zaidi kuliko nyasi. Mfano, mabaki ya majani ya maharage, njegere, desmodium na lusina. Majani yanayotokana na mimea kama lusina, calliandra au sesbania ina kiwango kikubwa cha protini pia. Ng’ombe wasilishwe kwa kutumia aina zote za jamii ya mikunde kwa zaidi ya asilimia 30 ya uwiano wa mchanganyiko wa malisho ili kuepuka matatizo ya kiafya. Aina nyingine ya vyakula vyenye protini ni mashudu ya pamba, mashudu ya alizeti na soya.
Madini: Mifugo wanahitaji madini ya ziada. Ni lazima yapatikane muda wote, mfano kama jiwe la chumvi. Wanyama wanaokuwa, wenye mimba, na ng’ombe anaenyonyesha wanahitaji kiasi kikubwa cha madini, mfano calcium na phosphorous. Mimea ya jamii ya mikunde na mengineyo isipokuwa nyasi inatoa kiasi kikubwa cha calcium na madini mengineyo.
Pumba
Pumba aina ya Dairy meal ina kiwango kikubwa sana cha madini. Lakini ina madhara kwa mifugo endapo wanyama watalishwa kwa kiwango kikubwa. Malisho yanayotokana na majani au nyasi kavu ni lazima yabakie kuwa chakula kikuu kwa mifugo.
Haishauriwi kulisha zaidi ya kilo 6 za pumba kwa siku kwa ng’ombe mwenye kilo 450. Ni lazima wapewe kwa kiwango kidogo sana, ambacho si zaidi ya Kilo 2 kwa mara moja na kichanganywe na majani. Kuongeza kiwango cha pumba kabla na wakati wa kunyonyesha/kukamuliwa, kisizidi kiasi cha kilo 2 kwa wiki ili tumbo la mnyama lizoee.
Wakulima wazoefu huongeza majani ya malisho na mbaazi kwenye lishe ya mifugo. Wanaweza hata kuacha pumba kwa muda au kupunguza matumzi ya pumba kupitia njia hii. Utafiti unaonesha kuwa kilo 3 za malisho ya majani na chakula jamii ya mikunde kama vile Desmodium au majani ya viazi vitamu hutoa maziwa sawa na kilo 1 ya pumba. Kwa hivyo, mfugaji anaweza kuokoa fedha atalisha ng’ombe wake kwa kutumia chakula cha jamii ya mikunde badala ya kununua aina nyingine ya virutubisho.
Aina ya 1 ya mchanganyiko
Mahitaji
|
Kiwango
|
Mabua ya mahindi yaliyokatwakatwa
|
Debe 2
|
Majani ya viazi vitamu yaliyokatwakatwa
|
Debe 2
|
Matete yaliyokatwakatwa
|
Debe 2
|
Mahindi
|
Sadoline 3
|
Mbengu ya pamba
|
Sadoline 11/2
|
Chumvi ya ng’ombe
|
Vijiko 2
|
Aina ya 2 ya mchanganyiko
Mahitaji
|
Kiwango
|
Mabua ya mahindi yaliyokatwakatwa
|
Debe 2 zilizoshindiliwa
|
Lusina iliyakatwa
|
Debe2
|
Matate yaliyokatwakatwa
|
Debe 2
|
Pumba
|
Sadoline 5
|
Chumvi ya ng’ombe
|
Vijiko 2
|
Post a Comment