0
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva, Jumanne wiki hii ataanza ziara rasmi nchini Tanzania ambapo anategemewa kufanya mikutano na mazungumzo na maofisa waandamizi wa serikali na wadau. 

Bw. Graziano da Silva anategemewa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO amepanga kufanya mikutano na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Tanzania Bara), Dkt. Charles Tizeba, na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed.

Ziara hii ya Mkurugenzi Mkuu inakuta wakati FAO ikiadhimisha miaka 40 toka kuanza shughuli zake hapa Tanzania. Wakati wa ziara hii, Bw. Graziano da Silva atakutana na uongozi na wafanyakazi wa FAO hapa Tanzania kabla ya kuhudhuria hafla maalum hapa Dar es Salaam kusherehekea maadimisho hayo. Hafla hiyo itahudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Samia Suluhu Hassan. 

Mwakilishi Mkazi wa FAO hapa nchini, Bw. Fred Kafeero, amethibitisha kuwa Bw. Graziano da Silva atakuwa hapa nchini kufuatia mwaliko wa Serikali ya Tanzania. “Mkurugenzi Mkuu wa FAO atabadilishana mawazo na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwenye masuala makuu yanayohusiana na uhakika wa chakula na maendeleo ya kilimo, ikijumuisha juhudi za FAO kitaifa na kikanda,” alisema. Bw. Graziano da Silva pia atajadili mambo mengine yanayohusiana na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na FAO, pia masuala mengine ya umuhimu kati ya pande hizo mbili, aliongeza. Mbali ya Maafisa wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu atakutana na wadau wengine wa FAO hapa nchini wakiwa ni pamoja na asasi za kiraia, taasisi za elimu, na taasisi za utafiti. 

Baadae Mkurugenzi Mkuu ataenda Zanzibar ambapo, miongoni mwa mambo mengine, anategemewa kuweka jiwe la msingi katika jingo la Mradi wa Kuzalisha vifaranga vya samaki unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa KOICA. Pia Bw. Graziano da Silva atapata fursa ya kutembelea mradi wa kilimo cha mwani na pia kuona maonesho ya bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa na wanawake wanaojihusisha na kilimo cha mwani. 

Tanzania ilijiunga na FAO mwaka 1962, na mwaka 1977 FAO ilifungua ofisi zake hapa Tanzania. Katika miaka 40 ya uwepo wake, FAO imeisadia Serikali ya Tanzania katika kupanga na kutekeleza sera, mikakati na mipango ya kilimo hapa nchini. Kazi ya FAO imejikita katika kuboresha usalama wa chakula na lishe pamoja na maisha ya wakulima wadogo na hivyo kuwa chachu ya kukua kwa uchumi kupitia sekta ya kilimo.

Post a Comment

 
Top