Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, tarehe 25 mwezi huu lilifanya msako katika pori lililopo Kitongoji cha Nzombo kandokando ya Mto Songwe, Kata ya Bonde la Usongwe, Wilaya ya Mbeya vijijini na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Nelson Tuyanje Mwaigombe (47) Mkazi wa Kijiji cha Mwampalala akiwa na risasi sita (06) za Short Gun aina ya Melior Super GT.
Soma taarifa yake:
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Mafanikio yaliyopatikana kutokana na misako ni kama ifuatavyo:-
Mnamo tarehe 25.07.2017 majira ya saa 21:05 Usiku Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko katika Pori lililopo Kitongoji cha Nzombo kandokando ya Mto Songwe, Kata ya Bonde la Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la NELSON TUYANJE @ MWAIGOMBE [47] Mkazi wa Kijiji cha Mwampalala kilichopo Kata ya Iwindi akiwa na risasi sita (06) za Short Gun aina ya Melior Super GT.
Awali Jeshi la Polisi lilipata taarifa toka kwa raia wema kuwa kuna watu wawili wameonekana katika pori hilo wakiwa na silaha ndani ya mfuko wa salfeti. Aidha silaha hiyo haijapatikana baada ya mtu mmoja ambaye bado anatafutwa kudaiwa kuwa ndiye mmiliki halali wa silaha hiyo kutoonekana mara baada ya mwenzie kukamatwa na yeye kufanikiwa kutokomea porini. Upelelezi unaendelea pamoja na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa aliyekimbia.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na tukio 01 la Ajali ya Moto lililosababisha kifo cha mtu mmoja kama ifuatavyo:-
AJALI YA MOTO NA KUSABABISHA KIFO.
Mnamo tarehe 25.07.2017 majira ya saa 23:45 usiku huko Mnarani Forest Mpya, Kata ya Forest, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya, mama mmoja aliyefahamika kwa jina la MAGRETH KAMBONJA [46] Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkombozi iliyopo Mbalizi, aliuguliwa na nyumba yake yenye vyumba vinne na kuteketeza mali zote zilizokuwa katika nyumba hiyo na kusababisha kifo cha mwenye nyumba hiyo MAGRETH KAMBONJA.
Inadaiwa kuwa chanzo cha kifo chake ni kutokana na kuvuta moshi mwingi hali iliyopelekea kufariki dunia wakati alipokuwa akipelekwa Hospitali kwa matibabu. Chanzo cha moto huo inasemekana ni hitilafu ya umeme iliyosababishwa na jokofu [fridge] iliyokuwa ikigandisha barafu. Moto huo umezimwa kwa ushirikiano wa wananchi, Jeshi la Polisi na Kikosi cha zima moto. Upelelezi unaendelea.
KUMWAGIWA KIMIMINIKA KINACHODHANIWA KUWA TINDIKALI
Mnamo tarehe 19.07.2017 majira ya saa 21:30 usiku huko eneo la Manga lililopo Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya, mama mmoja aliyefahamika kwa jina la VUMILIA SHANGEMA [31] Mfanyabiashara na Mkazi wa Manga akiwa amefuatana na watoto wake wawili 1. LOVENESS JOHN [11] Mwanafunzi wa Darasa la Sita katika Shule ya Msingi Sinde na 2. NANCY PETER [05] walijeruhiwa kwa kumwagiwa usoni, kifuani na mkononi kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni tindikali.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio mhanga ambaye ni VUMILIA SHANGEMA akiwa amefuatana na watoto wake wawili wakitokea dukani kununua bidhaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani wakiwa njiani alitokea mama mmoja ambaye aliweza kufahamika kwa jina la EMMY KYANDO [40] Mkazi wa Sae Jijini Mbeya ambaye inadaiwa kuwa ni mke mwenza na mhanga kutokana na mhanga kudai alizaa mtoto mmoja aitwaye LOVENESS JOHN na mume wake.
Mara baada ya mama huyo kujitokeza maeneo hayo aliwamwagia kimiminika hicho sehemu za usoni, kifuani na mikononi. Wahanga walipata msaada toka kwa wasamaria wema wa kupelekwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu. Aidha mhanga VUMILIA SHANGEMA ameumia vibaya usoni na kwenye macho hali inayosababisha kutoona. Majeruhi mwingine LOVENESS JOHN alijeruhiwa usoni lakini hali yake sio mbaya sana, NANCY PETER alitibiwa na kuruhusiwa.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi. Juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea kwa kushirikiana na mume wake aliyefahamika kwa jina la LAUSI KIDAGILE, Mkazi wa Sae kwani mara baada ya tukio hili mtuhumiwa ametoweka nyumbani kwake.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA ninatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kukamatwa mtuhumiwa azitoe Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake. Aidha ninatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia, kutanzua na kutokomeza vitendo vya kihalifu.
Imesainiwa na:
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
Post a Comment