0
Magufuli
Kundi la mashirika ya Kimataifa 18 yanayotetea haki za binadamu limeitaka Tanzania kuacha kuzinyanyasa asasi za kiraia zinazotetea haki za binadamu hasa zile zinazotetea haki ya wanafunzi waliopata ujauzito kurudi shuleni.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania Mwigulu Nchemba amenukuliwa hivi karibuni akionya kwamba wizara yake haitasita kufutia usajili shirika lolote lile lisilo la kiserikali linalotetea mapenzi ya jinsia moja na wanafunzi kurudi shuleni baada ya kuwa.
Kundi hilo la mashirika yanayotetea haki za binadamu ya kimataifa limeitaka Tanzania kuyaacha mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya shughuli zake pasipo na wasiwasi wa kuadhibiwa.
Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo, iliyotiwa saini na mashirika makubwa ya kimataifa kama vile Human Rights Watch na Amnesty International pia imeunga mkono msimamo wa kundi la asasi za kiraia lenye wanachama 25 ambalo wiki iliyopita kwa pamoja walitoa tamko lao kutaka serikali iwaruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kurudi shuleni baada ya kuwa wamejifungua.
Mwandishi wetu Sammy Awami anasema kundi hili la mashirika ya asasi za kiraia za kimataifa limeita serikali ya Rais Magufuli kuelekeza nguvu zake zaidi katika kuwapatia wananchi wake pasipo ubaguzi wa aina yoyote ile.
Rais Magufuli na viongozi wengine wa ngazi ya juu ndani ya serikali yake wameendelea kutilia mkazo msimamo wao kwamba serikali hii haitaruhusu wanafunzi wanaopata ujauzito kurudi shuleni baada ya kuwa wamejifungua.
Akiongea mkoani Mwanza, Jumanne Rais Magufuli aliyataka Mashrika yasiyo ya Kiserikali ambayo yamekuwa yakipinga uamuzi wa serikali kufungua Shule zao wenyewe ambazo zitawasomesha wanafunzi wanaopata ujauzito.
''Haiwezekani Serikali itoe pesa kuwasomesha wanafunzi halafu wapate mimba waendelee na masomo hilo haiwezekani, hizo NGOs zinazotetea hali hiyo zikitaka zijenge shule kwa ajili ya kuwasomesha wanafunzi watakaopata ujauzito,''alisema.
Wakati msimamo huu unaendana na sheria ya elimu ya nchi, umepingwa vikali na makundi mbalimbali kutoka ndani na hata nje ya nchi.

Post a Comment

 
Top