0
Raia wakisajiliwa kama wapiga kura nchini Kenya mapema mwaka huu
Image captionRaia wakisajiliwa kama wapiga kura nchini Kenya mapema mwaka huu
Mahakama kuu nchini Kenya imefutilia mbali zabuni ya jumla ya $24m (£18m) ya uchapishaji wa karatasi za kura ya urais nchini humo.
Mahakama imechukua hatua hiyo ikitoa uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa na upinzani kupinga utoaji wa zabuni hiyo.
Upinzani ulikuwa umesema kampuni iliyopewa kandarasi hiyo ina uhusiano na Rais Uhuru Kenyatta amabye pia anawania katika uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 8 Agosti.
Jopo la majaji watatu limesema Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC) ilikosa kushauriana na wagombea wote wa uchaguzi huo kabla ya kukabidhi zabuni hiyo kwa Al Ghurair ya Dubai.
Mahakama imeamua kuwa zabuni hiyo itangazwe upya.
Muungano mkuu upinzani National Super Alliance (Nasa), ulikuwa umewasilisha kesi kortini ukisema kampuni hiyo ilipewa zabuni hiyo bila utaratibu ufaao kufuatwa.
Tume ya uchaguzi ilikuwa imesema ilifuata utaratibu ufaao.
Kampuni ya Al Ghurair na Bw Kenyatta wote walikana kuwa na uhusiano wowote.
Mahakama iliamua kwamba kampuni hiyo inaweza kuchapisha karatasi za uchaguzi wa wabunge na maseneta, madiwani na magavana, ambao pia utafanyika tarehe 8 Agosti.
Mgombea urais wa Nasa Raila Odinga anashindana vikali na Rais Kenyatta, katika kinyang'anyiro ambacho ni kama marudio ya uchaguzi wa mwaka 2013.
Bw Odinga anawania urais kwa mara ya nne.

Post a Comment

 
Top