Na. Ahmad Mmow, Nachingwea.
KUTOPELEKWA kwa wakati na kiasi kidogo cha dawa za kuzuia ukungu na kuuwa wadudu (viwatilifu) kinachotarajiwa kutolewa kwa wakulima wa korosho wilayani Nachingwea mkoa wa Lindi, kumetajwa kutasababisha kushusha uzalishaji wa zao hilo msimu wa mwaka 2011/2018.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara, mbele ya mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango, uliofanyika katika kijiji cha Mpiruka A, wakulima hao walisema kiasi kidogo cha dawa viwatilifu kinachotarajiwa kupelekwa na kugawiwa bila malipo kwa wakulima wa zao hilo, na ucheleweshaji uliotokea kunauwezekano mkubwa wa kushuka kiwango cha uzalishaji wa zao hilo katika msimu wa 2017/2018.
Mkulima Alli Mawani alisema uzalishaji wa zao hilo utashuka kutokana na kuchelewa kupelekwa viwatilifu. Kwamadai kuwa katika msimu iliyopita, inapofikia mwezi Mei wanakuwa wameanza kupuliza dawa hizo. Hata hivyo hadi sasa hawajaelekezwa na hawajui lini watapata.
Alisema misimu ya nyuma walikuwa wanapeleka fedha kwenye vyama vyao vya msingi na kupewa viwatilifu vya bei nafuu kwasababu serikali ilikuwa inaweka ruzuku. Hata hivyo msimu huu wamerejeshewa fedha walizopeleka kwenye vyama hivyo. Ikiwamo chama cha msingi cha ushirika cha Ukombozi ambacho yeye ni mwanachama.
“Tulirudishiwa fedha zetu, tuliambiwa serikali italeta dawa na kugawa bure. Hadi sasa hazijaletwa na tunaambiwa hata zikiletwa zitakuwa kidogo kuliko mahitaji. Nasisi baada ya kurudishiwa tulitumia kwa matumizi mengine, uzalishaji lazima utashuka kwasababu wengi hatutapulizia,” alisema Mawani.
Mkulima Joseph Liundi alisema wakulima wengi waliacha kufanya maandalizi ya kununua viwatilifu baada ya kuambiwa na kusikia serikali itagawa bure. Hasa baada ya wakulima ambao ni wanachama wa vyama vya msingi kurejeshewa fedha na kuhakikishiwa watapata dawa hizo bila malipo. Liundi alisema hali hiyo imewachanganya wakulima wa zao hilo. Huku akihoji vyama vya msingi vilipata wapi uwezo na nguvu za kurejesha fedha za wanachama wake iwapo hakukuwa na mawasiliano na serikali. Nae Daudi Mkane alitoa wito kwa serikali kusimamia vizuri bei za viwatilifu kwa mawakala ili wakulima wasishindwe kununua baada ya zoezi la kupewa bure kuyumba.
Akijibu malalamiko na maombi ya wakulima hao ambao dhahiri walionekana kukata tamaa, mkuu huyo wa wilaya ya Nachingwea alisema dhamira ya serikali kwa wakulima ni njema na inatambua thamani na faida ya kazi wanayofanya kwao binafsi na uchumi wa nchi. Kwakuzingatia ukweli huo ndipo ilipoamua kuwasaidia viwatilifu.
Hata hivyo kiasi kitakacholetwa ni kidogo kikilinganishwa na mahitaji. Alibainisha kwamba mahitaji halisi ya dawa ya unga ni tani 20,000. Hata hivyo mgao ulitolewa na bodi ya korosho ni tani 1300 tu.
“Hayo yalikuwa mahitaji ya wilaya hii na tuliyoomba bodi ya korosho, kwa sasa hakuna haja ya kutafuta mchawi bali mnatakiwa kujipanga muweze kupulizia. Alisema awamu ya kwanza zitapelekwa tani 362. Ambapo tayari tani 30 zimeshapelekwa. Kuhusu viongozi wa vyama vya msingi kurejesha fedha za wanachama wake, Muwango alisema halikuwa agizo la serikali. Kwasababu huo ulikuwa uamuzi wa wanachama wenyewe.”
Katika msimu wa 2016/2017 wilaya ya Nachingwea iliongoza kwa uzalishaji wa zao hilo kuliko wilaya zote za mkoa wa Lindi. Ilizalisha takribani tani 20,000.
Post a Comment