Na. Ahmad Mmow, Lindi.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa kijiji cha Kiwawa kilichopo katika
wilaya na mkoa wa Lindi, wameshangazwa na hatua ya halmashauri ya wilaya
ya Lindi ya kuchukua na kuwakabidhi wavunaji mbao 2360 walizovuna
kwenye msitu wa kijiji hicho kinyume cha sheria.
Wakizungumza kijijini hapo, wananchi na viongozi hao walisema hawaelewi ni kigezo
gani vilitumiwa na halmashauri hiyo kuwapa mbao 2360 zilizokamatwa
kwenye msitu wa kijiji chao na kusababisha kijiji hicho kikose ushuru.
Mjumbe wa serikali ya kijiji hicho, Ahmad Koha, alisema tarehe 15 mwezi
Oktoba mwaka 2015 walikamata mbao 1000 walitoa taarifa wilayani hata
hivyo kwa mshangao mkubwa mbao hizo zilichukuliwa na mvunaji.
“Tuliwapigia simu akaja
ofisa misitu akasema anakwenda kuchukua gari, lakini hakurudi tena.
Badala yake huyo mvunaji aliyevuna kinyume cha sheria akaruhusiwa
aondoke na mbao hizo,” alisema Koha.
Mwananchi Ahmad Tendele alisema mwaka jana mwezi wa kwanza tarehe 20
walikamata tena mbao 1360 kwenye msitu huo, hata hivyo halmashauri ya
wilaya hiyo kupitia idara yake ya maliasili ilizuia mbao hizo
zichukuliwe na yeyote hadi itakapo tambulika zilivunwa kwenye msitu wa
kijiji gani Kati ya Mputwa na Kiwawa.
“Tuliambiwa zisiondoke hadi viongozi wa Mputwa na Kiwawa
wakutane. Hata hivyo ofisa aliyekuja hapa hakurudi tena, mbao hizo nazo
ziliondoka bila maelezo yeyote na kwamujibu wa viongozi wetu nikwamba
wamekwenda wilayani mara nyingi kuuliza namna zilivyoondolewa na hatima
ya ushuru wetu. Lakini mpaka sasa hakuna chochote tunachokielewa, “ alisema Tendele.
Maelezo ya Tendele yaliungwa mkono na mjumbe wa iliyokuwa kamati ya
upimaji wa hewa ya ukaa, Shaibu Mkulyungu, ambae alisema wamekwenda
wilayani mara nyingi kuulizia hatima ya malipo ya zao ushuru wa mbao
hizo na jinsi zilivyoondolewa bila kuwashirikisha. Alidai hata hivyo
hawapati ushirikiano. Alisema sababu kubwa ni migogoro ya mipaka ambayo
hadi sasa haijashugulikiwa kikamilifu. Hali ambayo inatumiwa na vijiji
vingine kuwaingiza wavunaji kwenye msitu wa kijiji hicho. Kwa madai
kwamba vijiji vingi vinavyokizunguka kijiji hicho vimeshaharibu na
kumaliza misitu yake.
Hata hivyo mwenyekiti wa kamati ya maliasili ya kijiji hicho, Said
Matata alisema hata serikali ya kijiji hicho inasitahili kubeba lawama
sawa na halmashauri ya wilaya. “Kamati ya maliasili inafuata
miongozo yote, ila serikali ya kijiji inasitahili kubeba lawama kwa
mfano kunamvunaji alikamatwa Litandantama hata hivyo mwenyekiti alisema
aachwe pamoja na vifaa vyake,” alisema Matata.
Mwanahawa Tawile ambae pia ni mjumbe wa serikali ya kijiji alisema
halmashauri ya wilaya hiyo hainabudi iwaeleze sababu ya kuwaruhusu
wavunaji waliovuna kinyume cha sheria waondoe mbao hizo bila
kuwashirikisha, huku ikijua wenye haki na mbao hizo ni kijiji hicho.
“Msitu unakwisha hakuna tunachonufaika, tunawakamata wavunaji
wanatetewa nawakubwa na mbao wanapewa. Tumeanza kuvunjika moyo, huenda
ndio sababu wanashindwa kushugulikia migogoro ya mipaka sababu
wananufaika nayo,” alisema Mwanahawa.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Issa Mtambile, licha
kukanusha kuwa serikali ya kijiji hicho haihusiki na upotevu wa mbao
hizo wala yeye kuamrisha mvunaji aliyekamatwa aachwe na vifaa vyake.
Alisema serikali ya kijiji haikushirikishwa kuziondoa mbao hizo 2360
bali wavunaji walikuwa wanasema walikuwa wanaruhusiwa na halmashauri.
Hata hivyo wanapouliza hawapati ushirikiano na hawajui hatima ya mgogoro
ushuru wa mbao hizo ambazo alidai kuwa anauhakika zilivunwa kwenye
msitu wa kijiji hicho.
Akijibu malalamiko hayo kwaniaba ya mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya wilaya hiyo, kaimu mkuu wa idara ya maliasili, Patrick
Senga alisema halmashauri imekuwa ikishugulikia migogoro ya mipaka.
Ikiwamo mipaka ya Kiwawa na vijiji vilivyokizunguka. Hata hivyo tatizo
kubwa ni vijiji hivyo kutoheshimu mipaka iliyopo kisheria.
Akibainisha kuwa tamaa ya maliasili ndio inayosababisha hali hiyo.
Matokeo yake migogogoro imekuwa ikijirudia mara kwa mara. Kuhusu mbao
zinazodaiwa kukamatwa na kuchukuliwa bila idhini ya kijiji, Senga
alisema mbao hizo zilivunwa katika kijiji cha Namkongo.
“Eneo lililovunwa mbao hizo halipo Kiwawa wala Mputwa
bali Namkongo, zilivunwa kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni.
Zililipiwa ushuru husika katika kijiji husika, “ alisema Senga.
Alikiri kuwa migogoro ya mipaka inaathiri mapato ya vijiji na
halmashauri hiyo. Huku akibainisha kuwa baadhi ya wafanyabishara
wanaitumia kuvamia na kuvuna mazao ya misitu kinyume cha sheria. Hivyo
halmashauri imejipanga kuendelea kupima mipaka kwa kushirikiana na
wakala wa misitu.
Post a Comment