DODOMA:
WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali itikadi
ya vyama vyao, wameungana kwa kauli moja leo Mei 2, 2017 na wamekubali
Mbunge mwenzao, Halima James Mdee wa Kawe (Chadema) asamehewe kutokana
na kosa la kutoa lugha isiyo na staha kwa Spika Job Ndugai.
Mapema
leo asubuhi Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge,
ilitoa uamuzi wake wa kumsimamisha asihudhurie vikao vyote vya Bunge
vilivyobakia kutokana na kosa hilo.
Mdee
na Freeman Mbowe walijitokeza mbele ya Kamati ya Maadili kujibu tuhuma
za kutoa lugha isiyokuwa na staha kwa Spika Job Ndugai bungeni siku ya
uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Aprili 5, mwaka
huu.
Baada
ya Mdee kusimamishwa, huku wabunge wengine na viongozi wa mikoa na
wilaya waliokuwa na makosa kama hayo wakisamehewa, wabunge walianzisha
mjadala wa kumtetea wakitaka asamehewe kwani aliomba msamaha Bungeni
mbele ya wabunge wote wiki iliyopita huku akiahidi kutorudia kosa.
Baada ya mvutano wa muda mrefu, wabunge wote wameridhia Mdee asamehewe na kumuonya asirudie kosa tena.
Akisoma maazimio ya Bunge kuhusu mjadala huo, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu,
Jenista Joakim Mhagama amesema kuwa, Bunge kwa kauli moja limemsamehe
Halima Mdee, hivyo adhabu yake ya kutohudhuria vikao vya bunge
vilivyobaki imefutwa.
Aidha
Bunge limempa sharti moja kuwa asirudie tena kutenda kosa kama hilo la
kudharau kiti cha spika na endapo atarudia, basi atapewa adhabu kubwa
zaidi tena bila kuitisha kikao cha kamati yoyote ya Bunge.
Pia
Kamati hiyo, imemsamehe Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) kutokana
na kosa la kutoa lugha isiyokuwa na staha mitandaoni kwa kuingilia
Haki, Uhuru na Madaraka ya Bunge.
Kamati imefikia hatua hiyo baada ya Mbowe kukiri kosa hilo na kuomba radhi wakati alipohojiwa na kamati hiyo mjini Dodoma.
Mwingine
aliyesamehewa ni Mbunge Ester Bulaya wa Bunda Mjini baada ya kupewa
karipio kali na Kamati hiyo kutokana na kosa la kudharau Mamlaka ya
Bunge.
Kamati pia imemsamehe DC Alexander Mnyeti kutokana na kukiri, kujutia kosa lake na kuliomba radhi Bunge.

Post a Comment