Rais
wa Rwanda Paul Kagame amewataka Wanyarwanda waondokane na kasumba ya
kuwapiga wake zao, ambapo amesisitiza umuhimu wa kumpa kichapo mwanaume
anayempiga mkewe.
Akihutubia
umati wa wanawake wanachama wa RPF-Inkotanyi, wikiendi hii, Rais wa
Rwanda amesema unyanyasaji wa wanawake haufai na wanaume wanaouendekeza
hawana budi kupigwa ili wasirudie.
“Kwa
nini awepo mtu wa kuvumilia unyanyasaji? Unyanyasaji hauvumiliki,
mwanamke ndiye amefanya kazi zote za nyumbani wewe umeshinda baa, halafu
ukirudi usiku unampiga?” Rais Kagame amehoji.
“Wanaume
wanaowapiga wake zao ndio wanatakiwa wapigwe,” Rais Kagame ameongeza,
ambapo amesema kasumba hiyo inatokana na ushauri ambao msichana anapewa
na wanawake kabla ya kuolewa.
Ameukosoa
utamaduni huo ambapo mwanamke mtarajiwa hufundishwa kuvumilia uonevu wa
mumewe, akiambiwa kujikaza kisabuni ndiyo siri ya mwanamke kudumu
kwenye ndoa.
“Msichana
anaambiwa anakokwenda (kuolewa) atakutana na migogoro, kwa nini
umrithishe matatizo? Eti wanaume wanapenda kuwaonea wake zao ikikutokea
vumilia!” amesema Rais.
“Tunataka
kukomesha unyanyasaji unaofanywa dhidi ya wanawake halafu wewe nyuma ya
pazia unamuambia mtoto akipigwa asilalamike?” Rais Kagame ameongeza.
Rais
wa Rwanda amesema ikitokea mwanamke apigwe, anatakiwa awaite
wanafamilia wampe kipigo muonevu, ikishindikana sheria ndipo ifuate
mkondo wake.
Katika
hatua nyingine Rais Kagame amewakemea wanawake walioichukulia vibaya
sera ya usawa wa jinsia, ambapo wapo wanaohisi inawapa haki ya
kuwadharau waume zao.
Biashara ya binadamu
Rais
Kagame amesema chama chake cha RPF Inkotanyi hakitavaalia miwani suala
la biashara ya binadamu, ambapo Wanyarwanda husafirishwa kwenda kuuzwa
katika nchi za nje.
“Naamini
mnakumbuka makumi ya wasichana waliorudishwa kutoka Uchina ambako
walikuwa wamefikishwa kwa ahadi hewa za maisha bora, walikuwa kama
mateka,” Rais Kagame amekumbushia.
Rais
Kagame amewataka wadau wa maendeleo nchini Rwanda walivalie njuga
tatizo hili, na kuwataka wasichana wajihadhari na matapeli wanaowarubuni
na kisha kuyaingiza maisha yao hatarini.
Aidha
Rais Kagame amewataka wazazi wawape malezi mazuri mabinti zao wanafunzi
wa sekondari ambao wamekuwa wakivuka mipaka ya nchi kwenda kufanya
biashara ya ukahaba nje ya Rwanda.
Rwanda ndiyo nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na wanawake wengi bungeni ambapo wamefikia asilimia 64 ya wabunge wote.
Bonyeza hapa kwa picha zaidi
Post a Comment