0

SERIKALI imewasilisha pendekezo la mabadiliko ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ili kuwezesha wanafunzi wanaochukua Stashahada katika vipaumbele vya kitaifa, kupewa mikopo ya kuwawezesha kuchukua elimu husika.
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema mabadiliko hayo, yamelenga kuwezesha kasi katika uchumi wa viwanda.
Profesa Ndalichako alisema mabadiliko katika Sheria Namba 4 ya Mwaka 2016 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), yamelenga kutoa nafasi ya kada ya Stashahada inayohitajika ambao wamekuwa hawapati mikopo.
“Kwa lengo la kupata balance (mizania) na kwa kuwa Diploma nayo iko kwenye elimu ya juu, watoto ni wale wale. Kuna wengine nao wanashindwa kumudu gharama na ili serikali ipate uwiano mzuri tumeona ni vizuri kuwe na marekebisho ya sheria,” alieleza Profesa Ndalichako.
Profesa Ndalichako alisema kuna umuhimu mkubwa wa kada ya Stashahada, hasa wanaokwenda sanjari na vipaumbele vya kitaifa kwenye msukumo wa Serikali ya Awamu ya Tano wa ujenzi wa taifa la vijana, kama ilivyo kwa wenye Shahada.
“Kama taifa tunazungumzia uchumi wa viwanda,wadau wote hata wale wa ngazi ya kati ni muhimu katika kuhakikisha kwamba ajenda hii inafanikiwa kama vile ambavyo wale wa digrii wangelifanya,” aliongeza waziri huyo.
Mwaka 2004, kulikuwepo na mabadiliko katika sheria hiyo iliyowezesha wanaochukua masomo ya sayansi, hisabati na elimu ya msingi (kwenye msisitizo wa sayansi na hisabati), kupata mikopo ya elimu, nafasi iliyoanza kutumika mwaka 2014, lakini hatua hiyo ilisimamishwa wakati wa muhula wa masomo wa mwaka 2016/17.
Hata hivyo, HESLB ilikaririwa ikisema kwamba maamuzi ya kusitisha utoaji wa mikopo, ililenga kutekeleza maagizo ya serikali. Hata hivyo, jana Profesa Ndalichako alisema kwamba uamuzi wa kusimamisha mikopo hiyo,ulitokana na nia ya serikali kufanya mabadiliko katika sheria hiyo ili kuipa wigo mpana zaidi kuliko kujikita katika eneo la sayansi pekee.
“Mwaka 2004 tuliingiza diploma, lakini kwa masomo ya sayansi pekee sasa, tunataka kuwa na kipengele kinachopanua wigo ili tuweze kuhusisha kozi nyingine za diploma ambazo zinaenda sanjari na vipaumbele vya kitaifa,” alifafanua waziri huyo.
Kwa mwaka wa masomo 2016/17, serikali ilipanga bajeti ya Sh bilioni 483 ambazo zitakopeshwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea. Katika mwaka huo, wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo walikuwa ni 25,715.
Wakichangia mjadala huo, Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF) alitahadharisha kuhusu vipaumbele vya kitaifa na kutaka kuwapo na ufafanuzi ili kuondoa utata. “Sijafurahi sana na phrasing of national priority.
Naogopa isije ikajibana au ikatumika katika hali itakayoleta utata. Hivi karibuni tulikuwa na utata mkubwa wa nani apewe mikopo...sasa tunasikia kuwa tunaenda kwenye uchumi wa viwanda isije fedha zote zikapelekwa kule.
“Kutafutwe njia ya kudetermine hizo priority za kitaifa na kujua watakuwa wangapi ili tujue kichumi itagharamu kiasi gani ilitusishindwe huko mbele,” alisema Saleh.
Fikra ya kutanua wigo kwa wanafunzi wa Stashahada ilifafanuliwa na watu wa Bodi ya Mikopo kwamba imezingatia kuwa katika sekta zote kutatakiwa uwiano wa wataalamu wa kada mbalimbali. Aidha, imeelezwa kuwa waziri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wataweza kushauriana na kuona hitaji ya kada mbalimbali zinavyokwenda.
Chanzo-Habarileo

Post a Comment

 
Top