Kati ya jambo mojawapo linaloonekana ni kikwazo kikubwa hadi sasa kwa
watu wengi, hasa kwa wale wanaohitaji kuingia katika biashara na
kujiajiri binafsi ni juu ya namna ya kupata mtaji wa biashara.
Mtaji wa kuanzia kufanya biashara ndio umekuwa chanzo cha vijana
wengi hivi leo kutoa sababu ya wao kushindwa kuingia katika biashara na
kujiajiri binafsi; hasa ukizingatia hali ya sasa ya ukosefu wa ajira
iliyokithiri hapa nchini.
Ukosefu wa ajira pamoja na ukosefu wa mitaji ya kuanzia kufanya
biashara, umesababisha vijana wengi wanaomaliza vyuoni na wale wanaotaka
kujiajiri binafsi kutumia kelele zao nyingi kulalamikia serikali na
taasisi nyinginezo nchini juu ya umaskini na ongezeko la kushuka kwa
kiwango cha uzalishaji.
Nami kupitia makala hii fupi ninayokuandikia leo kupitia katika
mtandao huu wa Ishi Ndoto Yako; ninapenda kukupa habari njema kwako wewe
kijana na mtu yoyote ambaye leo hii umeshindwa kujiajiri binafsi baada
ya kumaliza masomo yako na hatimaye kubaki ukiilalamikia serikali juu ya
hatma yako.
Hakuna serikali yoyote duniani inayoweza kutoa msaada wa kila kitu
kwa watu wake wote ambao ni wahitaji. Ukizingatia kwamba kila
panapokucha kuna ongezeko kubwa la watu hasa vijana wanaohitimu kila
mwaka elimu yao ya masomo ya juu. Huku bado hakuna mahali pa kuwapeleka
na kuwapa ajira.
Hivyo kwa kuliona jambo hili nimependa kukupa mwaga na habari njema
ya namna ya kupata mtaji wa kuanzia biashara unayohitaji kuifanya kwa
muda mrefu; uwe chuoni au nyumbani ni vyema ufahamu inakupasa utambue
jambo hili ninalokwenda kukuambia sasa.
Kama wewe ni kijana au mtu unayehitaji kuanzisha biashara yako
binafsi na unahitaji mtaji kwa muda mrefu; nataka utambue kwamba mtaji
wa kuanzisha biashara yako unayohitaji kuanzisha haupo serikalini wala
kwenye taasisi nyingine zozote zile. Bali upo kwako binafsi.
Nataka uelewe nilichosema hapo juu nikirudia tena ya kwamba; mtaji wa
kuanzia biashara yako uliyo na maono na malengo nayo kwa muda mrefu
tangu ukiwa chuoni hadi sasa bado ukiwa mtaani nk. upo kwako binafsi,
haupo serikalini.
Usisubiri serikali ndio ikupe mtaji wa kuanzia biashara; wala
usisubiri taasisi binafsi na mabenki kukukopa fedha kwa ajili ya kuanzia
biashara unayoitaka. Bali badilika kwa kufahamu kuwa mtaji ni wewe
binafsi na kile ulichonacho wewe binafsi.
Kwa nini nasema mtaji ni wewe binafsi? Ni kivipi wewe unaweza kuwa mtaji wa biashara unayohitaji kufanya?
Nataka utambue kuwa wewe ni mtaji wa kwanza kwa sababu kuu kubwa
ambayo nimeithibitisha kwa muda mrefu na nina uhakika nayo; na hii si
sababu nyingine bali ni akili, nguvu, kipaji, uwezo na ubunifu wako
ulionao ndio mtaji wa kwanza wa dhidi ya kile unachotaka kukifanya.
Mambo hayo yote manne ndio mtaji wako tosha wa kwanza unaoweza
kuutumia kuboresha na kuinua maisha yako; na kujua ni namna gani ya
kufanya ili uweze kuwa miongoni mwa watu matajiri duniani sawa na
wengine waliofanikiwa.
Jambo moja muhimu unalopaswa kufahamu ni kujua ni namna gani ya
kutumia akili na maarifa yako yote, nguvu zako, kugundua na kukitumia
kipaji ulichonacho, na kubuni njia na wazo bora la kukupeleka katika
kilele cha mafanikio yako.
Kwa msaada wa kukujenga katika jambo hilo ninakutaka uambatanishe
mambo hayo na ngunzo tatu muhimu za kukuwezesha kutimiza maono yako
ambazo ni imani, uhusiaano mzuri na wengine pamoja na kutokukata tamaa juu ya kufikia maono na malengo mazuri uliyonayo.
Hadi kufikia hapo nikutakie mwanzo mzuri wa kuanza kufikiri upya juu
ya maono yako uliyoyaacha kwa kuisubiri serikali na taasisi binafsi
zikusaidie kuyatimiza. Usiogope! songa mbele.
Post a Comment