Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma linamshikilia Patrick Malindisa (29)
mkazi wa Mtaa wa Namanyigu Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumuua baba
yake mzazi Athanasi Malindisa (70) kwa kumpiga na kitu chenye ncha kali
kichwani na kidevuni na kisha kutaka kuufukia kwenye shimo alilochimba
ndani ya nyumba yao.
Mmoja wa wanafamilia ambaye ni mdogo wa marehemu Pius Malindisa jana
alisema walipata taarifa ya kifo cha ndugu yao Januari Mosi mwaka huu
saa 1:30 jioni kutoka kwa mtoto wa marehemu Patrick Malindisa.
Alisema marehemu alikuwa akiishi na mtoto wake huyo ambapo baada ya
kufanya mauji hayo alianza kuwaarifu ndugu kuwa amefariki kwa ugonjwa wa
tumbo.
Kutokana na taarifa hizo ndugu walikusanyika nyumbani kwa marehemu
ambapo baada ya kuingia ndani walikuta akiwa amelala ndipo walipowaita
viongozi wa mtaa na baada ya kufunua walibaini marehemu ameuawa kwa
kupinga na kitu chenye ncha kali kichwani na kidevuni.
“Baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa awali tulitoa taarifa polisi ambapo
walifika na kuuchukua mwili kwa uchunguzi zaidi. Na mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma huku mtoto wake
akishikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
“Tulipofika hapa tulikuta shimo limechimbwa ndani ya nyumba na inaelekea
lilimshinda na kuamua kuanza kutoa taarifa kwetu ambapo alidai alikuwa
anaumwa ugonjwa wa tumbo,” alisema Pius
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji amethibitisha kutokea
kwa mauaji hayo ambapo kwa sasa wanamshikilia mtoto wa marehemu, Patrick
Malindisa kwa uchunguzi zaidi.
Post a Comment