JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linawashikilia watu 12, wakiwemo viongozi
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Arusha.
Viongozi hao walikamatwa kwa amri ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo wakituhumiwa kuhusika kuchoma moto mashine za kuvuta maji kutoka
kwenye chanzo cha Kangdet wilayani Karatu kwa madai kwamba wanatekeleza
agizo la Serikali, hatua ambayo imeelezwa kuwa haikufuata utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Arusha, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, aliwataja waliokamatwa kuwa ni pamoja na
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Karatu, Moshi Darabe ambaye pia ni
Diwani wa Kata ya Barai, anayedaiwa kuhamasisha wananchi kuchoma moto
mashine hizo zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 16.
Wengine waliokamatwa ni Diwani wa Kata ya Mang’ola, Lazaro Emanuel,
viongozi wa vijiji vya kata hizo pamoja na baadhi ya wananchi.
Kamanda Mkumbo alisema kuwa msako wa kuwakamata watuhumiwa wengine
waliohusika na tukio hilo bado unaendelea na uchunguzi utakapokamilika
watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.
Desemba 27, mwaka huu, kundi la wananchi wa vijiji vinne vya kata hizo
waliandamana, wakang’oa na kuchoma moto mashine za kuvuta maji katika
chanzo cha maji cha Kangdet, kinachotegemewa na vijiji vingine vya
Kata ya Barai.
Kutokana na tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa
na mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Gambo, walitembelea
eneo la tukio na baada ya viongozi kueleza kilichotokea, aliagiza
kukamatwa kwa watu wote waliohusika na uharibifu huo.
“Sheria lazima ichukue mkondo wake kwani agizo la Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa lilikuwa wazi na halikusema wananchi wachukue sheria mkononi,
jambo hili ni kinyume cha sheria,” alisema Gambo katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubilate Mnyenye
(Chadema), amesema kuwa yeye, mbunge wa jimbo hilo, Willy Qambalo na
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’ola, Jacob Pius, wametakiwa kuripoti Kituo
Kikuu cha Polisi jijini Arusha leo asubuhi kwa mahojiano kuhusu tukio
hilo.
Post a Comment