![]() | |
|
MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Arusha, imetupilia mbali rufaa ya Mbunge wa Arusha Mjini,
Godbless Lema (Chadema) ya kuomba dhamana yake na hatimaye kurudishwa
katika Gereza la Kisongo jijini hapa.
Atakuwa
katika mahabusu ya gereza hilo hadi Februari 2 mwakani atakaporejeshwa
mahakamani kusikiliza kesi yake ya msingi. Hii ina maana kwamba, sikukuu
zote za mwisho wa mwaka, yaani Krismasi na Mwaka Mpya zitamkuta mbunge
huyo akiwa mahabusu.
Mbunge
huyo anashikiliwa kwa mwezi mmoja sasa katika Gereza Kuu Kisongo, baada
ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufutilia mbali rufaa yake.
Akisoma
uamuzi mdogo wa Jaji Fatuma Masengi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha, Angelo Rumisha, alisema Mahakama imeifuta rufaa hiyo
kutokana na wakata rufaa kufanya hivyo nje ya muda.
Rumisha
alisema waomba rufaa walitakiwa kuonesha kusudio la kukata rufaa ndani
ya siku 10 tangu maamuzi ya maombi ya marejeo kutupwa na Mahakama Kuu,
yaliyokuwa mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha,
Sekela Moshi, Novemba 11 mwaka huu.
“Hivyo
Mwomba rufaa hii (Lema) kupitia Mawakili wake alitakiwa kuonesha kusudio
au kutoa notisi kuonesha Mahakama sababu ya kukata rufaa na Novemba 21
walipaswa kukata rufaa, lakini wao walikata Novemba 22 nje ya muda wa
kukata rufaa,” alisema.
Alisema
kutokana na hali hiyo, Mahakama imekubaliana na upande wa pingamizi
lililowekwa na upande wa Serikali kupitia Wakili Paul Kadushi
akishirikiana na Martenus Marandu kuwa rufaa hiyo haikufuata misingi ya
kisheria kuikata sababu hakuna kusudio la kukata rufaa na kuiomba
Mahakama hiyo itupilie mbali rufaa hiyo.
Rumisha
alisema baada ya pingamizi hilo kutolewa na upande wa Lema kuomba
Mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo, kwani rufaa yao ipo ndani ya
muda na imewasilishwa kwa hati ya dharura, Mahakama ilivyopitia hoja za
pande zote mbili imeona rufaa hiyo imeletwa Mahakamani hapo nje ya muda
unaotakiwa.Kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa Februari 2, mwakani.
Aidha
alisema mbali na nje ya muda pia wakata rufaa hawakuzingatia sheria
inavyotaka kuwa ukikata rufaa lazima uanze na kutoa siku 10 za kusudio
la kukata rufaa, na hivyo kuifutilia mbali rufaa hiyo.
Baada ya
uamuzi huo wa Msajili Rumisha, Wakili wa Lema Adam Jabir, aliomba
Mahakama hiyo itoe angalizo kwa askari wanaokwenda Mahakamani hapo
kuweka ulinzi, kwani wanawazuia lakini pia raia wanawake wanapekuliwa na
askari wanaume.
Alisema
mteja wao (Lema) anasikitika kuona hali hiyo ikijitokeza wakati yeye ni
Mbunge na kesi inasikilizwa chumba cha wazi ili kila mmoja asikilize na
kufahamu kinachoendelea.
Akijibu
hoja hiyo, Msajili Rumisha alisema Mahakama ikiruhusu watu wote
wanaokuja katika kesi hiyo kuingia kutakuwa na uhaba wa sehemu za kukaa,
kwa vile chumba ni kidogo na ndio sababu watu wanadhibitiwa.
Nje ya
chumba cha Mahakama Wakili wa Lema, John Mallya aliwaambia waandishi wa
habari, kuwa baada ya kuzungumza naye, Mbunge huyo aliwaomba
kutojishughulisha na suala lolote la kukata rufaa, ingawa wao kama
mawakili wanaona bado kuna njia za kufanya hivyo katika Mahakama za juu.

Post a Comment