0

WIMBI la watumishi hewa limechukua sura mpya mkoani Arusha baada ya kubainika kuwa kuna majina ya wafanyakazi waliokwenda masomoni lakini hawajaonekana kwenye vyuo walivyodaiwa kusajiliwa na wala hawapo kwenye sehemu zao za kazi ingawa wanaendelea kupokea mishahara yao ya kila mwezi.

Hii ni kutokana na mishahara yao kuendelea kuingia kwenye akaunti zao benki pamoja na malipo ya kuhudhuria mafunzo kwenye vyuo ambavyo ingawa vimepokea fedha za ada na huduma nyingine, hazijapokea wafanyakazi hao ambao walitakiwa kujiunga na masomo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, tayari kuna wafanyakazi 71 wa halmashauri za Meru na Arusha Vijijini, walioaga kwenda masomoni katika vyuo tofauti nchini, lakini imebainika kuwa hawapo kwenye vyuo hivyo.

Mnyeti akizungumza na gazeti hili jana alisema kati yao, 15 ni wale waliotakiwa kujiunga na vyuo mbalimbali na idadi yao kwenye mabano, Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (1), Chuo Kikuu cha Mount Meru (6), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (6), Chuo Kikuu cha Mwenge (6); Chuo cha Eckinford Tanga (5) na Chuo cha Tiba cha KCMC Moshi (4).

Wengine Chuo Kikuu cha Arusha (3), Chuo cha Ualimu cha Patandi (3), Chuo Kikuu cha Ruaha (3), Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere Memorial (3) na Chuo Kikuu cha Kampala (3).

Wapo pia waliotakiwa kuwepo katika Chuo cha Tanzania Institute of Accountancy (1), Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (2), Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa (2), Chuo Kikuu cha SAUT-Mbeya (1), Chuo Kikuu cha Jordan (1), na Chuo Kikuu cha Stephano Memorial Moshi (1), hivyo kufanya jumla yao wote ifikie wafanyakazi 71.

Alisema walioomba kwenda kusoma kutoka wilaya ya Arumeru ni wafanyakazi 306, lakini kati yao 71 hawajaonekana kwenye vyuo hivyo na kwamba inasadikiwa walisingizia kwenda kusoma tangu mwaka 2011 lakini wako kwenye shughuli nyingine ikiwemo kuajiriwa kwenye kampuni nyingine binafsi pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Alisema kwa kitendo hicho wafanyakazi hao wameiingizia serikali hasara ya Sh 837,545,280/- (karibu Sh milioni 840) kupitia mishahara ambayo ilikuwa ikiendelea kuingia kwenye akaunti za benki za wafanyakazi huku wakiwa katika ajira sehemu nyingine kwa kisingizio cha kwenda kusoma.

Kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkuu huyo wa Wilaya, Alexander Mnyeti alitoa siku 30 kwa wafanyakazi wote 71, warudishe fedha zote za mishahara waliyokuwa wakipokea wakidai kuwepo masomoni kumbe wapo katika ajira nyingine za nje.

Pia aliwataka wafanyakazi wengine wote ambao wako masomoni warudi kutoa taarifa za maendeleo ya masomo huko waliko kwa waajiri wao ili serikali ijiridhishe kuwa kweli wanasoma na wanaendelea vizuri.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru Christopher Kazeri alisema kuna haja ya uongozi kufuatilia watumishi wanaoomba ruhusa kwenda masomoni maana wengi ni waongo, wanaitapeli serikali wakijua wazi wanakwenda kufanya shughuli zao, na hasa kipindi hiki ambapo kuna upungufu wa watumishi wa umma.

Post a Comment

 
Top