Siku
moja baada ya Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo kudaiwa
kumfanyia fujo jirani yake, mchungaji huyo maarufu kwa jina la Mzee wa
Upako ameibuka kanisani kwake na kusema msemo wake wa kawaida kuwa,
‘watashindana lakini hawatashinda.’
Pia alisema kuwa alitaka kusema jambo, lakini hatazungumza kama wengi walivyodhani.
Lusekelo
aliyasema hayo jana jioni katika ibada ya Ijumaa kanisani kwake, Ubungo
Kibangu ambako mwandishi wa Mwananchi alihudhuria.
“Nimeyaona
magazeti hapa, ooh Mzee wa Upako, ooh Mzee wa Upako, sisemi. Sasa leo
yupo hapa, na kwa taarifa yao watashindana sana, lakini hawatashinda.
Hii ni kama kumpiga chura teke,” alisema huku akishangiliwa na waumini
wake.
Kabla ya kuzungumza, Lusekelo aliingia kanisani akiimba wimbo wa kuabudu ‘Niguse Tena’ huku waumini wote wakiwa wamesimama.
Akiwa
amevalia shati jeupe la kitenge na suruali nyeusi huku kanisa likiwa
limezingirwa na walinzi kila kona, mchungaji huyo aliingia na kusimama
madhabahuni kisha kuwasalimu waumini: “Nawasalimu katika jina la Bwana.”
Baada
ya salamu hiyo, alianza kuimba wimbo mwingine na waumini hao wakaanza
kuimba pamoja naye huku wakipita mmoja mmoja mbele kumtuza fedha.
Wimbo ulipoisha, waumini waliketi na Lusekelo alianza kuhubiri kwa kufungua Biblia katika kitabu cha 2 Timotheo 4.
Katikati
ya mahubiri hayo, alidokeza na kusema kuna watu walikuwa wanasubiri
kuona Mzee wa Upako hayupo na wanataka aseme, lakini hatasema chochote.
“Kuna
kitu nilikuwa nataka nikiseme, lakini sitakisema ili waendelee kusema
haohao waliokuwa wanasema. Sisemi chochote. Hao waliosema wakawaulize
wenyewe,” alisema bila kufafanua zaidi.
Ingawa alisema hatasema chochote, mahubiri yake yalionekana kama kujibu mapigo.
“Imani
yangu ndiyo ilikuwa mwisho, kwa sababu maadui watakuwa wengi lakini
watajikuta wanapiga risasi kule, kumbe adui yupo huku… vita ni kutulia,”
alisema.
“Adui
yako hataacha kuwa adui yako. Jiepushe sana na watu hao. Lakini mimi
ninaamini Mungu atawalipa sawa na amri yake wakati ukifika.”
Aliendelea na kusema wanadamu wamekengeuka na kuziacha njia za uzima na kuzigeukia njia zao wenyewe.
“Wakati
wote watu watakataa kusikia ule ukweli, Ogopa sana anayekataa
kukusikiliza, watakapozigeukia njia zao wenyewe, wakiacha kusikia
ukweli, jua kuna tatizo, akiacha kukusikiliza ni hatari sana jua kuna
rushwa. Ukiona anaacha kukusikiliza kaa tayari” alisema.
Mchungaji huyo aliendelea kuhubiri na kusema ni marufuku kumuhukumu mtu kabla ya kumsikiliza.
“Hao
ndiyo marafiki wanafiki.Nao wakajiepusha wasisikie yaliyo kweli na
watageukia hadithi za uongo. Uongo ukisemwa sana hubadilika na kuwa ni
kweli.
“Wale
wazee wa Israel walitunga uongo, na wakatoa fedha uongo usambazwe, ule
uongo mpaka leo bado unaitafuna Israel.” alisema Mzee wa Upako.
Kabla
ya Lusekelo kuingia kanisani, mchungaji mmoja ambaye jina lake
halikuweza kupatikana alisimama madhabahuni na kusema mwaka huu mwanzoni
Mchungaji aliziombea bahasha na kuubariki kuwa mwaka wa kucheka. “Kuna
watu wanaotaka kuuharibu, lakini hawatafanikiwa.”
“Zimebaki
siku 40 kabla ya kumaliza mwaka wa kucheka, lakini kuna watu lazima
muwe nao makini wanaweza kusababisha mwaka wa kucheka usiishe vizuri.”
alisema
Mahojiano ya Mwananchi na Mzee wa Upako Jumanne wiki hii
Awali
katika mahojiano yaliyofanyika nyumbani kwake Kawe Jumanne wiki hii,
Lusekelo alisifu uamuzi wa Serikali ya Rais John Magufuli kwa kuzuia
shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni kwa
kuwa hali ya kisiasa Zanzibar si nzuri na kwamba uamuzi huo unanusuru
amani ya nchi.
Mzee
wa Upako alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi
yaliyofanyika Jumanne kabla ya taarifa zake za hivi karibuni kuwa
amegombana na jirani yake.
Hata
hivyo, Lusekelo amesema shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria ni
muhimu kurushwa moja kwa moja, lakini ni hatari kwa usalama iwapo
kitatumiwa vibaya.
Serikali
ilitangaza Januari mwaka huu kuwa kituo cha televisheni cha Shirika la
Utangaza la Taifa (TBC) hakitakuwa kikirusha shughuli zote za Bunge
kutokana na gharama za matangazo hayo kuwa kubwa.
Waziri
wa Habari, Nape Nnauye alisema wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo
bungeni kuwa badala yake shughuli hizo zitarekodiwa na kurushwa usiku na
kwamba vituo vingine binafsi vinaruhusiwa kurusha moja kwa moja.
Hata
hivyo, vituo binafsi pia vilizuiwa na sasa hata wapigapicha za
televisheni hawaruhusiwi kuingia na kamera ndani ya ukumbi wa Bunge.
Sababu
ya Waziri Nape aliyotoa wakati huo, ilipishana na kauli ya Waziri Mkuu
Kassimu Majaliwa aliyoitoa wakati akizungumza na Watanzania waishio
nchini Uingereza ambako alisema kurusha Bunge moja kwa moja ni kwenda
kinyume na kaulimbiu ya Rais Magufuli ya “Hapa Kazi Tu” kwa kuwa anataka
watu wafanye kazi badala ya kuangalia matangazo ya televisheni wakati
wote.
Katika
mahojiano hayo, Mzee wa Upako alisema ni muhimu kuwa na Bunge Live,
lakini kutokana na hali ya kisaiasa ya Zanzibar na sababu za kiusalama
ni bora lisionyeshwe.
“Hali
ya Zanzibar kisiasa si nzuri kwa hiyo ukiacha uhuru wa kila mtu aseme
anachojisikia, ni hatari kwa taifa hili. Mali kubwa tuliyonayo katika
nchi hii ni amani na utulivu. Wanasiasa si watu wazuri sana (kwa kuwa)
wapo tayari kufanya lolote ili wapate madaraka au wasalie madarakani,”
alisema.
Alisema
si vyema ukawaacha watu kuzungumza kuhusu maandamano na mikutano ya
kisiasa bungeni na Bunge lipo ‘live’ wakati unajua hali iliyopo
Zanzibar. Na unapozungumzia uongozi wa Rais, lazima ujue kwamba ana
dhamana ya kusimamia ulinzi na usalama.
“Ukisema
uanze kusemasema tu kila kitu, utahatarisha amani ya Taifa hili kwa
kuwa mtu anaweza kusema neno dogo tu nchi ikalipuka. Hivyo Serikali
kuchukua uamuzi wa kuchuja nini kinasemwa ni muhimu sana kiusalama,”
alisema Mzee wa upako.
Alisema
katika uchaguzi wa mwaka jana kwa mara ya kwanza wapinzani walipata
kura nyingi, hivyo ni dhahiri kwamba hao watu wanakubalika.
Alisema kwa maana hiyo endapo wapinzani wakiruhusiwa kuingia barabarani kuandamana inawezekana wakasababisha maafa.
“Endapo
wataingia (wataandamana) wapinzani 20,000 tu halafu wakakataa kutoka
unafanyeje? Ukisema uue watu 300 inakuwa ni nchi tena? Tayari vita,”
alisema mchungaji huyo.
Kuhusu
hali ya kisiasa Zanzibar, Mchungaji Lusekelo alisema kinachomkwamisha
katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kupata uongozi wa Zanzibar
ni hoja yake ya Serikali tatu kwa kuwa inaiweka nchi njia panda katika
masuala ya amani na usalama.
“Kwa
mfano kama kweli Sharif alishinda, tatizo si kushinda, tatizo ni
usalama wa nchi. Unapozungumza Serikali tatu unatuhakikishiaje kuwa nchi
yetu itakuwa salama? Au unatuhakikishiaje kwamba tutakuwa wamoja?”
alihoji.
“Hakutakuwa
na Tanganyika na Zanzibar? Akishindwa kutuhakikishia, bora mambo yabaki
hivi hivi kwa kuwa amani ni muhimu kuliko madaraka.”
Alisema amani ya nchi si kitu cha kuchezea wala kujaribisha kwa kuwa nguvu ya ngumi haipimwi kwenye mwili wa mtu.
Kadhalika
alisema siasa za Zanzibar zimetawaliwa na ubaguzi baina ya wakazi wa
Unguja na Pemba tofauti na hali ilivyo Tanzania Bara.
“Ni kama Kenya ambako ukabila umetawala,” alisema.
“Ni
vigumu sana Mpemba akawa CCM na hata akienda CCM ujue kanunuliwa tu na
ukimchunguza vizuri utakuta si Mpemba, na ndiyo maana siku zote, CCM
itashinda Unguja na CUF itashinda Pemba, piga ua.”
Kuhusu suala la Katiba Mpya
Mzee
wa Upako alisema tatizo la Watanzania si Katiba Mpya, bali maisha
mazuri, huduma nzuri za afya, ulinzi na usalama na kuona rasilimali za
nchi zinawanufaisha.
“Suala
la Katiba Mpya ni hitaji la kisiasa si la wananchi. Wapinzani wanadhani
ikipatikana Katiba Mpya, wataweza kushika dola na chama tawala
wanadhani watapokonywa dola, lakini wananchi wao wanataka maendeleo,”
alisema mchungaji huyo.
Chanzo: Mwnanchi