0

KATIKA kile kinachodhihirisha nia ya dhati ya kupiga vita na kukabili jitihada za kueneza vitendo vya ushoga nchini, serikali imefanikiwa kuidhibiti Asasi ya Kimataifa ya UPR Info iliyoandaa mpango wa kuwashawishi maofisa wa serikali na wabunge kuunga mkono harakati za ushoga nchini.

Serikali imeidhibiti asasi hiyo wakati ikiwa katika jitihada za kuwashawishi maofisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria na wabunge ili waunge mkono kuishawishi Tanzania kuridhia utekelezaji wa mapendekezo ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu ikiwemo suala la ushoga yaliyoasisiwa na mataifa ya Marekani na Ulaya.

Moja ya ushawishi uliolengwa na asasi hiyo ili kuwalainisha watunga sera (wabunge) na watekelezaji wa sera hizo (watendaji wa serikali) kuunga mkono vitendo hivyo vya ushoga ilikuwa ni kuandaa mpango wa kuendesha semina kwa viongozi hao, jaribio ambalo hata hivyo limezimwa na Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe.

Msimamo wa Dk Mwakyembe Dk Mwakyembe akizungumzia tukio hilo jana alisema,

“Nilikataa na niliwaambia wazi kwamba serikali haihitaji ushauri wala ushawishi wa chombo chochote cha ndani au nje ya nchi kuhusu masuala ya ushoga na ndoa za jinsia moja kwani ni batili kisheria, kiimani na kiutamaduni.”

Waziri huyo alisema maombi ya asasi hiyo kutaka kuendesha semina hiyo yaliwasilishwa kwake Jumatano wiki hii, ambapo asasi hiyo ya UPR Info ilisema lengo ni kuwapa ufahamu viongozi wa serikali na wabunge kuhusu utekelezaji wa mapendekezo mbalimbali kuhusu haki za binadamu yaliyotolewa na Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.

Alisema baada ya kushauriana na maofisa wake waliamua kuyakataa maombi hayo kutokana na sababu mbalimbali lakini kubwa ikiwa ni uchunguzi wa wizara hiyo kubaini kuwa asasi hiyo ni miongoni mwa asasi za kimataifa zinazoshawishi mataifa mbalimbali kuchukulia masuala ya ushoga kama sehemu ya haki za binadamu.

"Hatuhitaji semina zao kufahamu msimamo wa Tanzania kama nchi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu. Mapema mwaka huu tulijiandaa bila msaada wao na kuweza kuwasilisha kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi taarifa ya pili ya nchi yetu kuhusu haki za binadamu chini ya mfumo wa mapitio kwa kipindi maalumu,” alisema Waziri Mwakyembe.

Alisema katika mkutano huo, Serikali ya Tanzania ilifanya kazi nzuri na sasa wameanza maandalizi kwa ajili ya kikao kijacho kitakachojadili masuala hayo mwaka 2021 chini ya uratibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hivyo hawahitaji msaada wa ziada au kitaalamu kuhusu suala hilo kwa vile wanajitosheleza.

Maombi ya Asasi ya UPR Info kwa serikali yaliwasilishwa na Mwakilishi wa ukanda wa Afrika wa asasi hiyo, Gilbert Onyango na jana Waziri Mwakyembe alimuonya mwakilishi huyo kuwa kama lengo ni kuishawishi Tanzania itambue ushoga na ndoa za jinsia moja kama sehemu ya haki za binadamu kama ilivyo katika baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani, atakuwa anapoteza muda wake bure kwani masuala hayo ni batili kidini, kisheria na kiutamaduni na kamwe hayajadiliki.

Utekelezaji wa mapendekezo Katika kikao cha 25 cha Baraza la Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa kilichofanyika mwaka huu, mapendekezo 227 yaliwekwa mezani lakini serikali iliridhia kutekeleza mapendekezo 131, lakini iliyakataa mapendekezo 94 na mengine 2 imeyakubali kwa kiasi fulani.

Wataalamu kutoka Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria walisema mapendekezo yaliyokubaliwa ni yale ambayo yanaendana na misingi ya Katiba, Sheria, Sera, programu mbalimbali, mila na desturi za Watanzania.

Mapendekezo yaliyokubaliwa yanahusu ukamilishaji wa mchakato wa kuunda Katiba, kuijengea uwezo wa kifedha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kutekeleza Malengo endelevu ya Dunia na uandaaji wa taarifa za nchi za utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu.

Mengine ni utekelezaji wa Mpango Kazi wa Haki za Binadamu, haki za wanawake na watoto, watu wenye ulemavu, wazee, haki ya elimu, afya, maji, mazingira na mengineyo.

Yaliyokataliwa yanahusu ndoa za jinsia moja, haki za mashoga, ubakaji ndani ya ndoa, kuongeza wigo wa uhalalishaji wa kutoa mimba, adhabu ya kifo, kuweka sera ya kutonyonga wanaokutwa na adhabu ya kifo, ndoa za wake wengi na kuridhia Mikataba ya Kimataifa ambayo haiendani na Katiba na sheria za nchi.

Wadau watoa maoni Wakitoa salamu zao kwa mataifa hayo yanayochochea ushoga, na kuunga mkono hatua ya serikali kuendelea kuonesha kutokuwa na mchezo katika kudhibiti viashiria vya ushoga nchini, Mdhamini wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Askofu David Mwasota alisema anaridhishwa na mwenendo wa serikali katika hilo.

Katika kauli yake alisema; “masuala hayo ni laana na ndiyo maana hata Rais Mteule wa Marekani (Donald Trump) aliungwa mkono na wengi kwa vile alikataa usodoma na gomora (ushoga) katika nchi hiyo.

“Tunapongeza serikali kwa msimamo huo, na mambo mengine kama misaada Mungu atatupigania kwani hakuna haki za binadamu katika dini zote zinazohamasisha matendo kinyume na maadili na imani kwa Mungu,” alisema.

Alisema matendo hayo licha ya kupingwa na imani zote lakini pia si mila na desturi kwa nchi. Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Bashir Ally, alisema Watanzania wana uwezo wa kusimamia mambo yao bila kuingiliwa au kufundishwa na mataifa ya nje.

Alisema serikali na wananchi wake wanafanya maamuzi kwa manufaa ya nchi na si kuyumbishwa hivyo uamuzi wa kukataa ushauri ni wa busara kwani katika suala hilo hata nchi za Magharibi walipoweka wazi bado kuna misuguano inaendelea kuonesha wapo wasiokubaliana nayo.

Mwanasheria mmoja maarufu aliyekataa kutajwa jina lake ili maoni yake kutoingiliana na utetezi wa baadhi ya kesi anazosimamia alisema Waziri (Mwakyembe) alifanya vyema kutosikiliza mawazo ya asasi hiyo na kuonesha msimamo wa nchi katika jambo hilo na kwamba hiyo ni salamu tosha kwa wahamasishaji wa vitendo hivyo.

Post a Comment

 
Top