0

Watanzania wengi hawaijui Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), majukumu yake na miongozo inayoongoza uchaguzi, hali inayosababisha manung’uniko mengi na upotoshaji kwa umma juu ya tume hiyo.
 
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani (pichani) wakati akitoa tathmini ya elimu ya mpiga iliyotolewa hivi karibuni kwenye Mkutano Mkuu wa 32 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) uliofanyika wiki mbili zilizopita mjini Musoma.
 
Bw. Kailima alisema kutokana na hali hiyo, NEC imeanza kutekeleza mkakati kabambe wa kutoa elimu ya mpiga kura kupitia njia mbalimbali ikiwemo kushiriki kwenye maonesho na mikutano inayojumuisha wadau muhimu wa uchaguzi.
 
Alisema kutokana na utekelezaji huo wa mkakati wa elimu ya mpiga kura anaamini baada ya miaka mitano au kumi ijayo Watanzania wataifahamu tume hiyo na kufanikisha chaguzi zijazo bila ya manung’uniko na kwa mafanikio makubwa zaidi.
 
“Baada ya miaka 5 au 10 ijayo, tunategemea kwanza watu wataijua Tume ya  Taifa ya Uchaguzi kwa sababu bila kumung’unya maneno watu hawaijui Tume ndio maana wanauliza “hivi baada ya uchaguzi nyinyi tume mnafanya nini” alisema Bw. Kailima na kuongeza kuwa:
 
“Sasa wakiijuia Tume na ule uhalali wake, uiaminifu wa wananchi kwa NEC utaongezeka kwa kiwango kikubwa sana, manung’uniko kwamba tume haitimizi wajibu wake yatapungua kwa kiwango kikubwa ”
 
“Pili ule upotoshaji itapungua kwa sababu wananchi watakuwa wameelewa kwa kiwango fulani kuhusu Tume, taratibu za uchaguzi na wakishaelewa wewe ukienda na jambo lako watakushangaa.”
 
Alisema iwapo Watanzania watapata elimu ya mpiga kura na kuizingatia hata uchaguzi wa mwaka 2020 utakuwa mzuri kwa sababu kila atakayeshiriki atakuwa na uelewa wa kiwango cha juu kuhusu uchaguzi na maswali kawaida yatakwisha kabisa.
 
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, anaamini watu wakielimika pia mvurugano zitapungua katika mchakato wa  kupiga kura, kuhesabu kura, kujumlisha kura na kutangaza matokeo kwani kila mtu atakuwa anajua taratibu zinazoongoza mchakato huo.
 
“Hata zile kelele za kusema tunakaa mita 200 au mita 300 hazitakuwepo kwa sababu kila mtu atakuwa amefahamu kumbe hata kama nisipokaa huu ni utaratibu kwa hiyo mambo yatakwenda vizuri”alisisitoza Bw. Kailima.
Akitoa tathmini ya mkutano wa ALAT, Bw. Kailima alisema washiriki wengi wa mkutano huo wanahitaji kueleweshwa mambo mbalimbali kuhusu uchaguzi na tume inayosimamia na kuratibu uchaguzi huo.
“Kuna maswali ambayo yaliulizwa pale ambayo kwa mtendaji ambaye ni mzoefu asingeweza kuuliza maswali ya namna ile, ni maswali ambayo yako wazi ikiwemo kuhusu fomu ya kutoa matokeo namba 21 (a) na (b)” alisema Bw. Kailima.
 
Hivyo alionesha kuwa kunahitajika kiwango cha juu cha elimu ya mpiga kura kwa watendaji na wenyeviti wa halmashauri na wagombea kwa ujumla.
Aliongeza kuwa amegundua pia kwamba watu wana shauku kubwa ya kujua mambo mbalimbali kuhusu uchaguzi na tume huku akikiri baadhi yao kudhani kama Tume inachelewa kutoa elimu na wengine wakistaajabishwa na Tume kuwepo kwenye mkutano huo.
Bw. Kailima alisema jambo lilionesha sura tofauti na aliyoizoea ni kuona washiriki wa mkutano huo kuwa na umoja bila ya kuonesha kwa tofauti za vyama.
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na kutoa elimu ya mpiga kura katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye shule za sekondari na maonesho na hivi karibuni inategemea kushiriki kwenye utoaji elimu katika maeneo mengine nchini.Na Hussein Makame, NEC

Post a Comment

 
Top