0

Jana, tulihitimisha mfululizo wa ripoti ya uchunguzi maalumu kuhusu waganga wa jadi uliobainisha jinsi wanavyowafilisi wananchi hasa wale wenye tamaa ya kupata utajiri na kutafuta bahati.

Katika ripoti hiyo iliyochapishwa kwa siku sita mfululizo, mwandishi wetu alionyesha kinagaubaga jinsi baadhi ya waganga wa kienyeji wanavyotumia matatizo ya wananchi kuwatapeli.

Lakini pia alibainisha jinsi waganga wengine wanavyotumia matatizo ya watu kuwadhalilisha kijinsia. Kimsingi ameweka bayana uhalifu unaofanywa na baadhi ya waganga wa kienyeji.

Kwa kuwa huu ni uhalifu, gazeti hili lilitaka kujua maoni ya polisi, chombo cha dola kilichopewa dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao ambacho kilipongeza kazi iliyofanywa na kisha kuomba msaada ili kuhakikisha mganga Nguvumali aliyehusika kwa kiasi kikubwa katika ripoti hiyo ya uchunguzi anatiwa nguvuni. Na hapo ndipo ilipo hoja yetu.

Kwanza kabisa ni jambo jema kwa wananchi kutoa taarifa polisi au kushirikiana na jeshi hilo katika mapambano dhidi ya uhalifu. Pale wanapopata tatizo lolote kuhusu usalama wao au mali zao huko ndiko kwa kukimbilia.

Hata hivyo, jambo la kustaajabisha ni kwamba licha ya kuwapo kwa chombo hicho, matukio hayo na mengine mengi yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku. Tunajiuliza. Je, tatizo ni wananchi kutotumia vyema chombo hiki kwa maana ya kukipa taarifa za uhalifu au taarifa hizo zinapotolewa hazifanyiwi kazi inavyopaswa hivyo watoaji kukata tamaa?

Tunasema hayo kwa sababu matapeli hawa wanajitangaza sehemu mbalimbali na wanafanya kazi zao kwa bayana. Mathalani, mwandishi wetu anasimulia alivyopata wazo la kufanya uchunguzi huu baada ya kuona bango la mganga huyo na kazi anazofanya.

Mabango yanayoelezea tiba au dawa za mambo ya ajabuajabu yapo kibao mitaani, tunayapita, polisi wanayapita, wanaonaswa wanawatafuta kwa simu kama alivyofanya mwandishi wetu na wengi wao wanaishia kuumizwa kimyakimya, hatujajipa muda wa kuhoji. Haya ni moja ya mambo ambayo yanaumiza idadi kubwa ya watu katika jamii na ni kielelezo mojawapo cha uelewa katika masuala yanayohusu maisha yao. Tuchukue hatua.

Mosi, asasi za kiraia na wadau wengine vikiwamo vyombo vya habari, vibebe jukumu la kutoa elimu ili wananchi waepukane na dhana kwamba kuna mganga anayeweza kumpatia utajiri zaidi ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Pili, Jeshi la Polisi, halmashauri za jiji, manispaa na miji zisimamie na kuchukua hatua dhidi ya matapeli hawa wanaotumia shida za kimaisha ya watu kujinufaisha.

Halmashauri zote ndizo zinazosimamia uwekaji mabango na matangazo katika maeneo mbalimbali hivyo, kwa kushirikiana na polisi ziendeshe operesheni maalumu ya kufuatilia yaliyoandikwa yanaakisi misingi ya sheria za nchi au vinginevyo na kuchukua hatua. Udhibiti huo ni hatua ya mwanzo ya kupambana na uhalifu huu kwani wananchi wanaposoma taarifa hizo ndipo huwafuata au kuwatafuta kama alivyofanya mchunguzi wetu.

Tunasema hili la waganga matapeli ni chuya katika mchele, matapeli wanaojitangaza hadharani ni wengi, tuwaelimishe wananchi wawaepuke, lakini tuwaibue ili sheria ichukue mkondo wake kwani wanachokifanya ni uhalifu.

Post a Comment

 
Top