0
Siku chache baada ya kutoa taarifa kwamba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeanza ukaguzi wa makontena Bandarini, Waziri mwenye dhamana Charles Mwijage ameahidi kuliunda upya shirika la viwango Tanzania (TBS) huku akieleza kuwa tayari wizara imeanza kutafuta vijana 136 watakaoajiriwa katika shirika hilo kwa lengo la kudhibiti bidhaa zinazoingizwa nchini chini ya viwango.
Waziri Mwijage amesema kuwa wataweka kitengo maalumu kwa vijana hao, watakaokuwa na uwezo wa kuchunguza mipaka ya nchi, kukamata, kuwasiliana na polisi na kutoa ushahidi mahakamani.
Mwijage amesema lengo la kuiunda upya TBS ni kuhakikisha kwamba kazi zinafanyika ipasavyo ili kulinda viwanda vya ndani, vinavyozalisha bidhaa mbalimbali. Hatua hiyo nakuja siku chache tu, baada ya makontena 100 kutoroshwa katika bandari kavu za Dar es Salaam bila ya kukaguliwa na hivyo kuikosesha mapato serikali na pia kuwa na hatari ya kuingiza bidhaa zilizo chini ya kiwango.
Taarifa ya Kaimu mkurugenzi mkuu wa TBS, Egid Mubofu imesema kuwa wameongeza siku za utekelezaji wa agizo la kuwataka wafanyabiashara waliochukua makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na TBS, watoe taarifa.
October 13, 2016 Waziri Mwijage alitoa siku nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila kukaguliwa na TBS, wakatoe taarifa katika shirika hilo.
Mwijage alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika kwa siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya asilimia 15.

Post a Comment

 
Top