0

BAADHI ya majengo kama shule, hospitali na mengineyo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera yameanza kujengwa na kufanyiwa ukarabati.

Aidha, fedha zote za misaada zinazotolewa na watu mbalimbali wakiwemo wafadhili kutoka nchi za nje zinawekwa katika akaunti moja na kutumika baada ya kamati maalumu kupitisha matumizi yake kwa lengo la kuhakikisha zinatumika vizuri.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya aliyasema hayo hivi karibuni alipozungumza na gazeti hili na kueleza kuwa uharibifu uliofanywa na tetemeko hilo ni mkubwa sana na misaada inayotolewa haiwezi kutosheleza mahitaji.

Brigedia Jenerali Msuya alisema ukarabati wa majengo kama sekondari ya Ihungo na Nyakato pamoja na nyumba za walimu, umeanza pamoja na kujenga nyumba za muda za walimu hao wakati ukarabati ukiendelea.

Alisema kinachofanyika ni fedha zote kuwekwa kwenye akaunti moja ya Maafa Kagera na kuna kamati maalumu inayozitoa na kuzigawa kulingana na mahitaji ya matumizi.

Alisema kwa wafadhili waliojitokeza kujenga shule kama Ihungo na nyinginezo ambao ni wawili au watatu wanapeleka maombi katika Kamati ya Maafa mkoani humo ili kuruhusu fedha hizo nyingine kutumika katika sehemu nyingine iliyoathirika.

“Uharibifu uliotokea ni mkubwa sana na serikali haina uwezo wa kumpatia kila mwananchi msaada, bali ni kufanya mambo yanayomgusa kila mmoja kama ujenzi wa shule, hospitali na zahanati na kuwapatia misaada mingine ya jumla,” alieleza Mkuu huyo wa Maafa nchini.

Post a Comment

 
Top