UTANGULIZI
Napenda kumshukuru mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kwa namna moja au nyingine kutoa mchango wangu kwa mtindo huu. Huu ni kama mwongozo tu wa nini utakabiliana nacho au unatakiwa kufanya katika zoezi zima la ufugaji wa kuku wa kienyeji. Nimeamua kuuleta kwenu ili kwa mtu mwenye malengo ya kufanikiwa kupitia ufugaji wa kuku ajue mlolongo mzima na changamoto ambazo atakabiliana nazo.
A.KWA NINI KUKU WA KIENYEJI?
1. Wastahimilivu wa magonjwa lakini ni muhimu wakikingwa na magonjwa ya kuku kama mdondo, ndui ya kuku n.k ili kuweza kuwaendeleza.
2. Wana uwezo wa kujitafutia chakula ardhini.
3. Wana uwezo wa kuatamia mayai, kutotoa na kulea vifaranga na ustahimilivu wa mazingira magumu kama ukame, baridi n.k
4.Nyama na mayai yake vina ladha nzuri kuliko kuku wa kisasa.(PATA SUPU YA KUKU WA KIENYEJI ILI UTHIBITISHE)
5. Wana uwezo wa kujilinda na maadui kama mwewe n.k . Pamoja na sifa hizi ni muhimu muhimu kuku hao wakapewa matunzo mazuri, wakawekwa kwenye mabanda mazuri, wakapewa maji na chakula cha kutosha.
B.FAIDA ZA KUKU WA KIENYEJI.
Faida ni nyingi na zinafahamika lakini nitaeleza zile ambazo kwa wengine huenda zikawa ni ngeni kwao.
- - Mayai huweza kutumika kwa tiba. (Pata maelezo jinsi yai la kuku wa kienyeji linavyoweza kutumika kwa tiba kutoka kwa wataalam wa tiba mbadala)
- - Kiini cha njano cha yai kinaweza kutumika kutengenezea mafuta ya nywele (shampoo)
- - Manyoya yake yanaweza kutumika kama mapambo.
- Fuga kuku upate faida kwa kuzingatia:
- Chanjo ya mdondo kila baada ya miezi mitatu na chanjo ya ndui mara mbili kwa mwaka
- Zuia viroboto, utitiri na minyoo.
- Chagua mayai bora kwa ajili ya kuatamiza
- Panga kuuza kuku kwa makundi uongeze kipato
- Kula mayai na kuku kadri uzalishaji unavyoongezeka.
- Kipato unachokipata utenge pia na kiasi kwa ajili ya uendelezaji wa kuku
C:MAPUNGUFU
Yako mapungufu mengi yanayofahamika lakini hapa naomba niweke lile la muhimu zaidi. MAGONJWA kama mdondo na ndui huathiri ufugaji wa kuku kutokana na kutokuzingatia kuchanja kuku kwa wakati.
D: KABILA ZA KUKU WA KIENYEJI
Kuna maelezo ya kusisimua sana kuhusu makabila ya kuku wa kienyeji, hata hivyo kuna ugumu kidogo kuweza kuyachanganua makabila hayo kutokana na muingiliano mkubwa wa vizazi kati ya aina mbalimbali za kuku hao.
Hata hivyo kuku hawa wana tofauti za kimaumbile zinazosaidia kwa kiasi fulani kutambua uwepo wa baadhi ya makabila ya kuku. Kabila hizi pia zinahusishwa kwa kiasi kikubwa na eneo kuku wanakotoka.
Baadhi ya kuku wa kienyeji wanaweza kutambuliwa kwa maumbile yao Mfano:
a. Kishingo - kuku wasio na manyoya shingoni
b. Njachama au Nungunungu - Hawa ni wale wenye manyoya yaliyosimama.
c. Kibwenzi - Ni wale wenye manyoya mengi kichwani.
d. Kibutu- Hawa hawana manyoya mkiani
Mwingiliano wa vizazi unaweza ukasababisha kuku kuwa na aina ya maumbile mchanganyiko. Mfano kuku aina ya kuchi anaweza kuwa na alama ya kishingo, Njachama, Kibwenzi au Kibutu.
Hivyo kabila za kuku zifuatazo zinaweza kutambuliwa kama ndiyo kabila za kuku wa kienyeji kulingana na maumbile yao na maeneo wanakotoka.
(i) KUCHI
Ni kuku warefu kwa umbo na wenye kusimama mgongo ukiwa wima. Wana manyoya machache mwilini na hasa kifuani, vilemba vyao ni vidogo. Majogoo huwa na wastani wa uzito wa Kg. 2.5 na mitetea kg 1.5 mayai ya kuchi yana uzito wa wastani wa gm 45. Kuku hawa hupatikana kwa wingi maeneo ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Zanzibar.
(ii) CHING'WEKWE
Kuku hawa ambao jina lao ni gumu kidogo kwa mtu asiyekuwa na meno kulitamka wana sifa zifuatazo.
Majogoo wana wastani wa kg 1.6, Mitetea wastani kg 1.2, mayai wastani wa gm 37. Kuku hawa wenye umbo dogo hupatikana zaidi maeneo ya CHAKWALE mkoani Morogoro na pia sehemu za umasaini. Kuku hawa hutaga mayai mengi sana kuliko aina nyingine ya kuku wa kienyeji waliopo Tanzania, kwa hiyo wanafaa sana kwa biashara ya mayai.
(iii)UMBO LA KATI
Majogoo wana uzito wa wastani wa kg. 1.9, Mitetea kg. 1.1, Kuku hawa ndio hasa wanaoitwa wa kienyeji(wa kawaida) Wana rangi tofauti. Utafiti umeonyesha kuwa kuku hawa hukua upesi na hupata kinga upesi baada ya kuwachanja dhidi ya ugonjwa wa mdondo (Castle desease)
Muhimu - Mfugaji akifanya uchaguzi kutoka kwenye aina hii ya kuku na kutoa matunzo mazuri kwa hao kuku waliochaguliwa, Hakika anaweza kupata kuku walio bora na wenye uzito wa kutosha pia kutaga mayai mengi na makubwa.
(iv) SINGAMAGAZI
Ni aina ya kuku wakubwa wa kienyeji wanaopatikana zaidi TABORA, kuku hawa wana utambulisho maalum kutokana na rangi zao. Majogoo huwa na rangi ya moto na mitetea huwa na rangi ya nyuki. Uzito - Majogoo uzito wa wastani wa kg 2.9, mitetea wastani wa kilo 2 mayai gramu 56.
(iiv) MBEYA
Kuku hawa wanapatikana Ileje mkoani mbeya. Asili hasa ya kuku hawa ni kutoka nchi ya jirani ya Malawi na si wa kienyeji asilia bali wana damu ya kuku wa Kizungu "Black Australop". Majogoo Kg 3 mitetea kg 2 mayai gram 49
(iiiv)PEMBA
Hupatikana zaidi Pemba. Majogoo Kg.1.5 Mitetea Kg 1 mayai wastani gm 42
(xi) UNGUJA.
Majogoo Kg 1.6,mitetea kg 1.2 mayai gm 42. Kuku hawa wa Unguja na Pemba wanashabihiana sana na Kuchi isipokuwa hawa ni wadogo.
SEHEMU YA PILI
1. MIFUMO YA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI.
A. MFUMO HURIA
Katika mfumo huu kuku huachiwa wakitembea toka asubuhi wakijitafutia chakula na maji na kufungiwa kwenye vibanda visivyo rasmi wakati wa usiku. Huu ni mfumo rahisi lakini si nzuri kwa mfugaji wa kuku wengi kwani atahitaji eneo kubwa la ardhi.
FAIDA.
Mfumo huu una faida za gharama ndogo za uendeshaji kiujumla.
HASARA
- Uwezekano mkubwa wa kuku kuliwa na vicheche, kuibiwa mitaani n.k
- Kuku huweza kutaga popote na kusababisha upotevu mkubwa wa mayai.
- Ni rahisi kuku kuambukizwa magonjwa
- Utagaji unakuwa si nzuri kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.
- Uwekaji kumbukumbu si nzuri.
- Ni vigumu kugundua kuku wagonjwa hivyo kusababisha ugumu katika utoaji wa tiba.
UTUMIAJI NZURI WA MFUMO HUU
- Kuku wajengewe banda kwa ajili ya kulala nyakati za usiku na liwasaidie wakati mwingine wowote hali ya hewa inapokuwa si nzuri.
- Kuku wapatiwe chakula cha ziada na maji.
- Kuku waandaliwe kwa viota vya kutagia.
- Kuku 100 ni vizuri wakitumia eneo la ardhi la ekari 1.
B.MFUMO NUSU HURIA
Huu ni mfumo ambao kuku hujengewa banda rasmi na banda hilo huzungushiwa uzio/ wigo. Mfumo huu ni ghari kiasi ukilinganisha na mfumo huria lakini huweza kumpatia mfugaji faida haraka sana.
FAIDA
Sehemu ndogo ya kufugia hutumika kuliko ufugaji huria, utunzaji wa kuku ni rahisi ukilinganisha na mfumo huria, Ni rahisi kutibu magonjwa ya mlipuka kama mdondo (Newcastle desease), Upotevu wa kuku na mayai ni mdogo sana ukilinganisha na mfumo huria.
C. MFUMO WA NDANI
Kuku hujengewa banda rasmi na hufugwa wakiwa ndani. Mfumo huu kuku huwekwa kwenye mabanda ambayo sakafu hufunikwa kwa matandiko ya makapi ya mpunga, takataka za mbao(randa), maganda ya karanga au majani makavu yaliyokatwa katwa.
FAIDA
Mfumo huu unahitaji eneo dogo la kufugia, uangalizi mzuri na rahisi wa kuku, Joto litokanalo na matandiko lina uwezo wa kuua vimelea vya maradhi, kuku wanakingwa na hali ya hewa mbaya na maadui wengine.
HASARA
Uwezekano wa kuku kudonoana ni mkubwa na pia Gharama za ujenzi wa mabanda
UTUMIAJI MZURI WA MFUMO HUU.
1. Matandiko yageuzwe kila siku
2. Kila mara matandiko yawe makavu kwa kuwa na madirisha yanayopitisha hewa ya kutosha, ambayo yatatoa unyevunyevu hewa chafu ikiwemo ammonia.
4. Mita mraba moja hutosha kuku 5 hadi 8.
UTATUZI WA KUKABILIANA NA VIKWAZO KATIKA UFUGAJI.
Mambo ya kuzingatia:
Mabanda bora - Fuatilia kwa wataalamu wa mifugo walio karibu nawe.
Sifa za banda bora (Waone wataalam wa mifugo)
Kuchagua kuku wa kuendeleza kizazi
Kuwa makini na aina ya mitetea na majogoo unatakiwa kuchagua ili kuwa na kizazi bora.
UTAGAJI WA MAYAI
Kwa kawaida kuku huanza kutetea(Kutoa mlio wa ishara ya kutaga) anapofikisha miezi sita hadi minane. Hivyo ni vyema viota viandaliwe mapema wakiwa na umri wa miezi mitano. Kuku anapoanza kutaga akifikisha mayai matatu mfugaji anashauriwa kuondoa kila yai linalozidi hayo matatu kila siku linapotagwa na kuliweka alama ya tarehe au namba kwa kutumia penseli ili kumfanya kuku aendelee kutaga kwa lengo la kufikisha mayai 15 mpaka 20.
Mayai yanayoondolewa yawekwe kwenye chombo kikavu kinachopitisha hewa ni vizuri pia kuweka mchanga ndani ya chombo hicho.
Hakikisha ya fuatayo.
- Sehemu iliyochongoka iwe chini na pana iwe juu.
- Hifadhi sehemu yenye hewa ya kutosha na isiyohifadhi joto
- Mayai yasikae kwenye hifadhi hiyo zaidi ya wiki mbili toka siku ya kuanza kutagwa.
UATAMIAJI WA MAYAI NA UANGUAJI WA VIFARANGA
Uatamiaji na uanguaji wa kubuni - Mfumo huu hutumia mashine za kutotoleshea vifaranga (Incubators) hutumika kuangua mayai mengi kati ya 50 hadi 500 kwa wakati mmoja Mashine zinazotumika kutotoleshea vifaranga wa kisasa zinaweza kutumika pia kutotoleshea wa kienyeji.
Uatamiaji na uanguaji wa asili
KUCHAGUA MAYAI YA KUANGUA.
Hili nalo ni muhimu kuzingatia. Ni vizuri kuchagua mayai ya kuatamia ili mayai yasiyofaa yaweze kuuzwa au kutumiwa nyumbani kwa chakula. Mayai ya kuatamia yawe na sifa zifuatazo
- Yasiwe na uchafu yawe masafi
- Yasiwe na nyufa
- Yatokane na kuku aliyepandwa na jogoo
- Yasiwe madogo wala makubwa bali yawe na ukubwa wa wastani kulingana na umbile la kuku.
- Yasiwe mviringo kama mpira pia yasiwe na ncha kali sana.
- Yasiwe yamekaa muda mrefu zaidi ya wiki mbili toka yalipotagwa
- Yasiwe yaliyohifadhiwa kwenye sehemu yenye joto.
KUMTAYARISHA KUKU WA KUATAMIA
Pamoja na matayarisho hayo zingatia kumuwekea mayai yasiyozidi 15 pia ni vizuri yasipungue 12. Kuku wanaotazamiwa kuatamia ni lazima wachunguzwe kwa makini kabla ya kuatamia ili kuhakikisha kwamba hawana chawa, utitiri n.k.
Kuwepo kwa wadudu hao huwafanya kuku wakose raha na kutotulia kwenye viota vyao. Hali hii husababisha kuanguliwa kwa Vifaranga wachache.
Sasa unatakiwa kufanya yafuatayo:-
- Nyunyiza dawa ya kuua wadudu ndani ya kiota
- Pia mnyunyuzie dawa kuku anayetarajia kuatamia
- Weka mayai kwenye kiota huku mikono yako ikiwa imepakwa jivu ili kuepuka kuwa na harufu kwani kuku anaweza kuyasusa.
Ni vizuri kuifanya kazi hii ya kumuandaa kuku anayetaka kuatamia wakati wa usiku. Pia ifahamike kuwa kwa kawaida kuku huatamia mayai yake siku 21.
PIA JIFUNZE MBINU ZA KUATAMIA MAYAI MENGI KWA NJIA ZA ASILI
Iwapo una kuku wengi wanaotaga kwa wakati mmoja ni vema ukawafanya wakaatamia na kutotoa pamoja.
Unachotakiwa kufanya ni kuchagua mayai ya kuatamia ukianzia na yai la mwisho kutaga.
Unaweza kuwaandaa kuku wako zaidi ya mmoja ili waanze kuatamia kwa pamoja na kupata vifaranga vingi kwa mara moja kuku wa kwanza anapoanza kuatamia.
Mwekee mayai viza au ya kuku wa kisasa kwani kuku huatamia hadi mayai yanapoanguliwa hivyo ukimuwekea mayai yasiyo na mbegu atakaa hapo muda mrefu hadi vifaranga watoke.
UTEKELEZAJI WAKE
Kuku anapotaga kila siku weka alama ya namba au tarehe kulinganisha na siku anayotaga
Yanapofika mayai matatu yaondoe na muwekee mayai viza au ya kisasa huku ukiendelea kuweka alama mayai yanayotagwa kila siku.
Mara kuku anapoanza kuatamia muongezee mayai ya uongo yafikie 8 hadi 10
Fanya hivyo kwa kila kuku anayetaga hadi utakapoweza kupata idadi itakayoweza kukupatia vifaranga wengi kwa wakati mmoja.
Wawekee kuku wote mayai siku moja kwa kuondoa mayai ya uongo na kuwawekea mayai ya ukweli wakati wa usiku.
MUHIMU
Mayai ya kuatamia yasishikwe kwa mkono ulio wazi na wala yasipate harufu za mafuta ya taa, manukato n.k.
JIFUNZE PIA KUTAMBUA MAYAI YALIYO NA MBEGU NA YALE YASUYO NA MBEGU.
Mfugaji anaweza kutambua mayai yaliyo na mbegu na yale yasiyo na mbegu siku ya saba baada ya kuanza kuatamia iwapo atapima mayai kwa kutumia box lililotengenezwa maalum pamoja na tochi yenye mwanga mkali ndani ya chumba chenye kiza. Hii itamuwezesha mfugaji ayatumie mayai yasiyo na mbegu kwa chakula cha familia au kuyauza.
TAMBUA VYAKULA NA UZALISHAJI WA KUKU -
Sitalielezea hili naomba ufuatilie mwenyewe.
JIFUNZE MBINU ZA KUZALISHA KUKU WENGI KWA MUDA MFUPI
Zoezi hili linawezekana iwapo uleaji wa vifaranga kwa njia ya kubuni utatumika. Kuku mmoja anaweza kutotoa zaidi ya mara saba kwa mwaka.
Hesabu ya uzalishaji wa kuku wengi kwa mwaka kwa kutumia mtetea mmoja tu.
Mpaka mwisho wa mwaka unaweza kuwa na idadi ya vifaranga 252 kwa kadirio la vifaranga 8 kila mzao. Hivyo kama una kuku 10 wanaotunzwa vizuri utakuwa umezalisha jumla ya vifaranga 2520.
Fuatilia kwa wataalamu wa mifugo ili ufundishwe zaidi kuhusu mbinu hiyo ya kuzalisha kuku wengi.
ULEAJI WA VIFARANGA
- NJIA YA KUBUNI
- NJIA YA ASILI
Njia zote mbili zinafahamika kama huzifahamu tafadhali fuatilia kwa mtaalamu aliye karibu nawe.
MAGONJWA NA WADUDU WANAOSHAMBULIA KUKU WA KIENYEJI NA JINSI YA KUKINGA.
A. MAGONJWA.
Ugonjwa hatari - Mdondo/ Kideri (Newcastle desease) Hapo nyuma dawa ya kukinga ugonjwa huu ilikuwepo lakini ilikuwa inahitaji kuhifadhiwa kwenye hali ya ubaridi (Friji) Hali hiyo ilisababisha iwe ngumu kutumika vijijini kwa dawa hiyo. Hivi sasa kumepatikana chanjoa ambayo inastahimili joto ambayo inaweza kutumika hata vijijini.
Pamoja na mdondo yapo pia magonjwa yanayoshambulia kuku hapa nchini
- Ndui ya kuku(Fowl pox)
- Mafua ya kuku(Infectious coryza)
- Homa ya matumbo (Cocciodiosis)
- Minyoo na wadudu kama viroboto, chawa, utitiri na kupe wa kuku.
DALILI ZA KUKU MGONJWA.
- Huzubaa
- Hali chakula/maji vizuri
- Hujitenga na wenzake
- Hujikunyata au kuinama
- Hutetemeka
- Hutembea kwa shida
- Utagaji wa mayai hupungua au hukoma kabisa
MAGONJWA YA KUKU HUSABABISHWA NA NINI?
Yako mambo mengi yanayosababisha lakini matunzo hafifu pia huchangia.
ATHARI ZA MAGONJWA.
Hili liko wazi
Maelezo haya ya magonjwa ni mengi hivyo tuwe wafuatiliaji kwa wataalam.
MATIBABU
KIDERI - Sifahamu tiba ya kitaalam ya ugonjwa huu kama kuna ambaye anafahamu tunaomba atufahamishe lakini ziko dawa za asili na za kitaalam ambazo zinafaa zaidi kwa chanjo.
Ugonjwa huu unaweza kuukinga kwa kuwapa kuku chanjo ya Mdondo. Pia usichanganye kuku wako na kuku ambao huna taarifa zao za chanjo.
KUMBUKA
Mdondo au kideri ni ugonjwa tishio ambao huweza kuua kuku wote
Mdondo ukitokea vifo huwa vingi pia kuku hupumua kwa taabu, hupooza na wengine huzunguka na huzungusha vichwa.
Mdondo unaweza kuzuilika kwa chanjo kila baada ya miezi 3
- NDUI YA KUKU
- HOMA YA MATUMBO (Fowly typhoid)
- MAFUA YA KUKU(Infectious coryzya)
- KUHARISHA DAMU(Coccidiosis)
- Minyoo na wadudu wanaoshambulia kuku kama viroboto n.k
Kwa magonjwa na wadudu tuliowataja hapo juu please wasiliana na mtaalamu wa mifugo aliye karibu nawe Kwani siwezi kueleza kila kitu hapa wataalamu tunao naamini watatusaidia.
TIBA ZA ASILI
Kuna madawa ya asili ambayo hutokana na mimea ambayo hukinga kuku.
BAADHI YA MIMEA INAYOTIBU NA KUKINGA MARADHI YA KUKU.
MWAROBAINI - Typhoid, kuhara, kideri, kifua na vidonda
ALOEVERA - Typhoid, kuhara, kideri, kifua na vidonda,ngozi na Cholera. Tutaelekezana zaidi namna ya kuandaa dawa hii.
Hapa nataka niorodheshe baadhi ya madawa ya asili ambayo yanasaidia kutibu na kukinga kuku.
Mwarobaini, Aloevera, Mtakalang'onyo(Euphorbia),Mbarika, mlonge, Ndulele/dungurusi/tura/ndura, Majani ya mpapai, Mwembe, Minyaa na Pilipili kichaa.
Post a Comment