0


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho Jumamosi na Jumapili kwa michezo mitano ya mzunguko wa nne lakini kuna mabadiliko yamefanyika ambapo sasa Jumatatu pia kutakuwa na mchezo wa ligi hiyo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko hayo katika mchezo wa African Lyon na Mbao FC uliokuwa uchezwe kesho Jumamosi, sasa ndiyo ambao utachezwa Jumatatu Septemba 12, 2016.

Mabadiliko hayo ni mwendelezo wa mabadiliko kadhaa ya ligi hiyo ambayo imeanza hivi karibuni.

Mchezo huo utafanyika kwenye Uwanja wa Uhuru baada ya African Lyon kubadili uwanja kutoka Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Michezo ya Jumamosi mingine itaendelea kama kawaida ukiwemo ule wa wapinzani wa jadi kati ya JKT Ruvu itakayokaribishwa na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati Mwadui FC itakuwa mwenyeji wa Stand United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Mbali ya michezo hiyo, pia Yanga itakuwa mwenyeji wa Majimaji ya Songea kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, wakati Azam FC ambayo itakuwa mgeni tena kwenye Uwanja wa Sokoine ikicheza na Mbeya City na kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Ndanda itaikaribisha Kagera Sugar ya Kagera.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili, Septemba 11, 2016 kwa Simba kuikaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Post a Comment

 
Top