0
Mbegu za kiume zikitungisha yaiWanasayansi wanasema huenda ikawezekana wanaume wawili kupata mtoto
Wanasayansi wanasema kuwa majaribio ya awali yanaonyesha kuwa siku za usoni itawezekana kuwatengeneza watoto bila ya kutumia mayai ya mama.
Wanasayansi hao wamefaulu kutengeneza watoto wa panya kwa kutumia mbegu za kiume na kuziunganisha na seli za kawaida kwa kuzidanganya kudhani kwamba zitatungisha mayai ya kawaida ya uzazi wa panya hao.
Uchunguzi huu unamaanisha kuwa siku za usoni huenda wanawake wasishirikishwe katika utengenezaji wa watoto kabisa, watafiti wanasema kwenye matokeo ya utafiti huo ambayo yamechapishwa kwenye jarida la kimatibabu la Nature Communications.
Wanasayansi hao kutoka Chuo Kikuu cha Bath walianza majaribio hayo kwa kutumia mayai ya uzazi ambayo hayajatungishwa mbegu za kiume.
Walitumia kemikali kufanya ujanja fulani ambao ulielekeza mayai hayo ya uzazi kuwa makamilifu.
Mayai haya ya bandia yanafanana au yana sifa nyingi zilizo sawa sana seli za kawaida kama vile seli za ngozi, katika njia ambayo zinajigawanya na pia kudhibiti chembe zinazoamua maumbile ya viumbe au DNA.
Watafiti wanasema kuwa iwapo kwa kutungisha mbegu za kiume kwenye mayai bandia kunaweza kuzalisha watoto wenye afya kwa panya, basi inamaanisha kuwa siku za usoni mpango huo unaweza ukatumiwa kwa mwanadamu na kwa kutumia seli ambazo ambazo hazitoki kwenye mayai ya uzazi.
Katika majaribio ya panya, uwezekano wa upachikaji mimba uliweza kufaulu mara moja kwa kila mara nne. Hii ni sawa na asilimia 25.
Dkt Tony Perry, mmoja wa watafiti hao aliambia BBC kuwa: "Hi ni mara ya kwanza kwa mtu yeyote kuweza kuthibitisha kwamba kitu kingine chochote, isipokuwa mayai ya uzazi, kinaweza kuungana na mbegu za kiume ili kuzalisha mtoto. Hali hii inafutilia mbali dhana ambayo imekuwepo kwa zaidi ya miaka 200."
 Panya wachanga waliozaliwa na wazazi wao
Panya wachanga waliozaliwa na wazazi wao walikuwa na afya nzuri
Panya waliozaliwa kwa njia hiyo walikuwa na afya, walikuwa na maisha marefu kama panya wengine wa kawaida na waliweza kuzaa baadaye watoto wa kawaida.
Iwapo haja ya kuwa na yai ili kuzalisha itaondolewa kutakuwepo na mabadiliko mengi katika jamii.

Wanaume wawili kuzaa

Dkt Perry alisema: "Kuna uwezekano mkubwa kuwa siku za usoni seli za kawaida mwilini zitachanganywa na mbegu za kiume ili kuunda yai lililotungishwa mbegu."
Hii inamaanisha kuwa, wanaume wawili wanaweza kuzaa mtoto, ambapo mmoja wao atatoa seli na mwingine achangie mbegu za kiume.
Katika hali nyingine mwanamume anaweza kumzaa mtoto wake yeye mwenyewe kwa kuwa ataweza kutumia seli zake na mbegu zake yake kwa shughuli hiyo muhimu.
Hapa mtoto anayezaliwa atakuwa kama pacha wa babake badala ya kuwa kiumbe kinachofanana naye.
Hata hivyo Dkt Perry anasema kuwa dhana hizi, kwa wakati huu, ni za matumaini tu.
Mapema mwaka huu nchini Uchina, wanasayansi waliweza kutengeneza mbgeu za kiume kutoka seli tete na kisha kutumia mbegu hizo kuzalisha panya wenye afya.
Dkt Perry alipendekeza kuwa utafiti huo unavyoendelea sambamba, unaweza ukafikia mahali ambapo mayai ya mama na mbegu za wanaume visihitajike kabisa katika uzalishaji au utengenezaji wa watoto.

Post a Comment

 
Top