0

 Mkuu wa wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza Emmanuel Kipole ameamuru Jeshi la polisi wilayani humo kumkamata Afisa Mtendaji wa kata ya Chifunfu Lucas Mashinge na kumuweka mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na upotevu wa kokoro lililokuwa limekamatwa na vijana saba wa kitongoji cha kijiweni katika operesheni ya kusaka zana haramu za uvuvi zinazoendelea kutumika ndani ya ziwa Victoria.

Uamuzi wa Mkuu wa wilaya hiyo Emmanuel Kipole kuamuru Afisa Mtendaji wa kata ya Chifunfu Lucas Mashinge akamatwe na kuswekwa mahabusu ya kituo cha polisi wilayani Sengerema unatokana na kupotea kwa kokoro hilo maarufu kama dunia katika mazingira ya kutatanisha likiwa limehifadhiwa katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa kata hiyo baada ya kukamatwa na vijana hao likiwa limefukiwa ardhini.

Baadhi ya wavuvi katika mialo ambako zoezi hilo la kuyakamata makokoro ya Sangara pamoja na nyavu za timba na kumbakumba limefanyika,wamewalalamikia baadhi ya viongozi kuwalinda vigogo wanaomiliki zana haramu za uvuvi,ilihali nyavu na makokoro yanayochomwa yakiwa ni yale yanayomilikiwa na wananchi maskini.

Kaimu mkuu wa idara ya mifugo na uvuvi wilayani Sengerema Nestory Mmbare akitoa taarifa ya zoezi la uteketezaji wa zana haramu za uvuvi,amesema zaidi ya nyavu 500 zenye thamani ya shilingi milioni 66,zilizokamatwa katika vijiji vinane vilivyopo mwambao wa ziwa Victoria wilayani humo zimeteketezwa na mkuu wa wilaya hiyo.

Zana haramu za uvuvi katika ziwa Victoria zimepigwa marufuku kwa mujibu wa sheria ya uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 kutokana na kuharibu ikolojia ya ziwa na mazalia ya samaki,hali inayosababisha zana hizo kukamata samaki wachanga.

Post a Comment

 
Top