
Kama unahitaji kufikia ndoto yako hauna budi kufahamu siri baadhi na kubwa za mafanikio ya watu waliokutangulia mbele yako, ili uweze kujifunza kila siku kulingana na wao walivyofanya na wewe uweze kuchukua hatua kadhaa kutokana na baadhi ya mambo waliyofanya wao kisha kuwa msaada mkubwa kwako kwa ajili ya kukufanikisha kwenye safari yako ya kutimiza ndoto uliyonayo. Na huu ndio ukweli na siri kubwa ya kufanikisha ndoto yako katika maisha, jifunze kwa waliokutangulia na waliofanikiwa.
Kijana Sandile shezi alizaliwa na kukulia katika mji wa Durban, South Afrika. Ni kijana aliyekulia katika mazingira magumu ya kiuchumi yaliyokuwa yakiisumbua familia yake, hii ilisababisha Sandile kuamua kujishugulisha na biashara ndogo ndogo tangu akiwa na miaka 12 hasa biashara ya kuuza mikate wakati akiwa bado anasoma shuleni (high school), na badae akiwa bado yupo shule aliendelea na biashara nyingine ya kutembeza nguo kwa kupita kwenye kila nyumba (door to door business), ambapo anasema biashara hii aliifanya katika mazingira magumu kutokana na kukataliwa kila alipokuwa akiingia nyumba hadi nyumba kuuza.
Akiwa ana ndoto ya kuwa mfanyabishara mkubwa wakati bado anapitia katika mazingira magumu na changamoto kubwa huku pamoja anasoma, ndipo sendile alipoamua kuacha chuo (Drop out of university) ambacho ni kitu kilichokuwa si kizuri kwa wazazi wake badae walipokuja kugundua na ukizingatia walikuwa wakimsomesha kwa shida. Na hii ilitokana na shauku aliyokuwa nayo sendile ya kuwa mfanyabiashara mkubwa kama Sandile Zungu ambaye ni bilionea na tajiri mkubwa wa South Afrika, ambaye Sandile shezi alipenda kumtumia kama mfano (Role model) wa maisha yake.
Alipoulizwa na chombo cha habari cha CCTV baada ya mafanikio yake kutokea, kwa nini aliamua kumtumia Sandile Zungu kama mfano katika maisha yake? Sandile alisema, “if he could do it, why can’t I?” Akimaanisha kama Sandile Zungu anayemtumia kama mfano kwenye maisha yake ameweza kufanya na kufanikiwa, kwa nini hasiwe yeye? Huo ndio uamuzi alioumua kuufanya Sandile shezi kwenye maisha yake, kwanza kwa kuacha chuo na kuamua kufanya kitu chochote hata kama ni cha hatari kwenye maisha yake ilimradi kufanikisha ndoto yake.
Baada ya kuacha chuo akiwa mwaka wa tatu kwa siri pasipo wazazi wake kujua chochote na kutumia hela za malipo ya ada ya chuo kama mtaji wa kuanzisha biashara yake mpya ya kuuza na kununua fedha za kigeni (foreign exchange market) iliyokuja kuwa biashara kubwa na kumfanya kuwa milionea hadi hivi sasa ninavyoandika hapa. Sandile shezi aliacha chuo kwa siri pasipo wazazi wake kufahamu hadi pale alipokuja kuwataarifu na kuwa mshangao kwao, lakini anasema alifanya hayo yote kwa ajili ya kutimiza ndoto yake aliyokuwa nayo, na sasa amebaki kuwa tegemeo kubwa kwa wazazi na familia yake.
Sandile Shezi anasema jambo pekee lililomfanya akaacha chuo ni baada ya kuona fursa ndani ya soko la kubadilisha fedha, haikuwa kitu rahisi kwake kama anavyosema kuingia katika biashara kubwa na yenye kiwango cha juu cha hatari (risk) hasa bado akiwa hana uzoefu wowote wa kuhusu biashara hiyo. Anasema kilichomsaidia sana kufanya biashara ya soko la fedha ni hatua aliyoichukua ya kuamua kujifunza kuhusu biashara hiyo kwa kupitia video za youtube pamoja na vitabu mbalimbali alivyosoma na majarida ya fedha.
Sasa Sendile ana miaka 23 ni mmiliki na mkurugenzi mkuu wa taasisi kubwa ya Global Forex Institute nchini South afrika inayojishughulisha na biashara ya fedha pamoja na utoaji wa elimu na mafunzo kwa vijana na watu wote kuhusu uwekezaji katika soko la fedha, na zaidi akiwa amelenga vijana kama yeye ili kuweza kufikia ndoto zao. Na inasemekana taasisi yake ni mojawapo ya taasisi inayotoa mafunzo na elimu hiyo bure (free of charge) katika nchi ya south afrika kwenye masuala ya fedha na namna ya kufanya uwekezaji. Shezi anasema kwa nchi kama yake, ina kiwango cha juu sana cha watu ambao hawana ajira lakini huu ni wakati wake wa kuwapatia vijana elimu kuhusu ujasiriamali na kujua namna ya kufuata fursa zilizo mbele yao hata kama kuna hatari kubwa kiasi gani. Shezi anaamini uwekezaji wowote upo kwenye hatari (risk) kubwa lakini kwa njia ya kuwekeza katika kujifunza na kulisha akili yako kwanza kwa ajili ya kile unachotegemea kufanya, basi kila mmoja anaweza kufanya.

Hadi hivi sasa Sandile shezi anamiliki kiasi cha utajiri unaofikia $1.5 Milioni na taasisi yake inakadiriwa kuajili watu wapatao zaidi ya ishirini na zaidi, pamoja na hilo pia taasisi yake inahudumia wateja wengi zaidi ya taasisi nyingine za kifedha kwa kuwapa mafunzo kuhusu uwekezaji na ujasiriamali. Sandile shezi pia hajaishia hapo kwani amekuwa ni mtu anaetoa misaada mbalimbali kwa jamii yake kwa kupitia Sandile Shezi Foundation na hasa misaada hiyo anatoa akilenga hasa kwenda kwenye sekta ya elimu na afya.
Je, Umejifunza nini kutokana na maisha ya Sendile Shezi?
1: Haijalishi unatokea familia yenye uwezo wa chini kiuchumi ukiamua kuishi ndoto yako utafanikiwa.
Kwa kupitia Sandile shezi hii imedhihilika wazi kuwa suala la kutokea familia isiyojiweza kiuchumi sio kigezo hata kidogo cha mtu yoyote kutokufanikiwa katika ndoto yake aliyonayo. Unachopaswa kutambua ni muhimu sana uelewe kile unachokitaka kisha amua kukishikilia hadi pale utakapoona kimefanikiwa. Usichokee njiani wala kukata tamaa mapema kwa sababu ya kuangalia mazingira na hali ya familia unayotokea. Jiamini na amini unaweza. Ishi ndoto yako.
2: Umri wako mdogo si kigezo cha kufikia mafanikio unayoyataka.
Wapo watu kila unapojaribu kuwaambia kuhusu habari ya kutimiza ndoto zao au mikakati yao fulani waliyonayo, watakuambia bado wanasoma au umri wao bado hauwaruhusu kufanya hivyo, wanabaki kusema nitafanya tu huko mbele, au anasema kwani bado mimi ni mdogo sana watu watanishangaa kwa nini najishughulisha na biashara badala ya kusoma. Nataka kukuambia umri wako husiwe kigezo cha wewe kutimiza ndoto yako nzuri uliyonayo kwa muda mrefu, amua sasa kuishi katika ndoto yako pasipo kuona aibu juu ya umri ulionao.
3: Unapaswa kukubali changamoto na hatari zilizo mbele yako kama unataka kufanikiwa.
Kuna msemo ninaopenda unaosema, “if you do what is easy your life will be hard, but if you do what is hard your life will be easy.” Msemo huo ukiwa na maana kwamba, kama unapendelea kufanya mambo marahisi uwe tayari kuishi maisha magumu hapo badae, lakini kama utapenda kuishi maisha magumu (yenye kupitia changamoto na hatari nyingi) basi maisha yako yatakuwa marahisi hapo badae. Sandile shezi aliamua kuingia kwenye biashara ya soko la fedha ingawa biashara hiyo imejaa hatari nyingi (risk), lakini pamoja na hilo bado hakuona hatari hizo kama kizuizi kwake hasa cha kumfanya hasitimize ndoto yake ya kuwa mfanyabishara mkubwa. Amini na wewe unaweza kama sandile shezi, usiogope changamoto bali chukua hatua leo hii katika kufuata na kuishi ndoto yako.
4: Usikimbilie kufanya kitu chochote kabla hujachukua hatua ya kujifunza.
Kama Sandile shezi anasema alianza kujifunza kuhusu masuala ya soko la fedha kabla ya kuingia moja kwa moja kwenye biashara hiyo, tena alijifunza kwa kupitia video za youtube na kwa kusoma vitabu. Jiulize ni mara ngapi na wewe ulitoa muda na kuchukua hatua ya kujifunza kuhusu jambo fulani ulilokuwa ukitaka kulifanya? Mara nyingi sana watu wengi tunapenda kukimbilia kufanya mambo fulani pasipo kufanya utafiti na mwisho wa siku tukikosea katika kile tunachokifanya tunaamua kukata tamaa mapema na kuacha kufanya kabisa. Usikimbilie kufanya biashara yoyote kama hujafanya utafiti, tafiti kwanza kisha uamue kuingia katika biashara hiyo. Acha uvivu wa kupenda kusoma, kumbuka kama unahitaji mafanikio makubwa hauna budi ujitoe kujifunza kila siku.

Huo ndio ukweli kuhusu maisha ya Sandile shezi milionea kijana mwenye umri wa miaka 23, ambaye pamoja na kuwa milionea pekee anatufundisha pia kupenda kurudisha kile tunachokipata kwa jamii zetu ili tuweze kufanikiwa zaidi. Lakini pia unapaswa kuwa na mtu unayeweza kumtumia kama mfano kwako (role model) wa maisha yako au juu ya kile kitu unachotaka kufanya.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Post a Comment