0

Dar/Arusha. Hatua ya kuondolewa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Felix Ntibenda na nafasi yake kuchukuliwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo imepokewa kwa hisia tofauti huku baadhi ya wachambuzi wakisema ni mikakati ya kisiasa.

Ntibenda aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu, alipandishwa mwaka 2014 kuwa mkuu wa mkoa, na kubakizwa katika nafasi hiyo katika uteuzi uliofanywa mwaka huu na Rais John Magufuli.

Hakuna sababu zilizoelezwa kuhusiana na mabadiliko hayo ya juzi asubuhi wakati Ntibenda akijiandaa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Amref na baadaye wa Tasaf.

Ntibenda ambaye alifurahiwa na vyama vya upinzani, amekuwa katika ugomvi na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambao wamekuwa wakimlalamikia kutokana na kuwaingilia katika majukumu yao.

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, Lengai ole Sabaya aliwaambia waandishi wa habari wiki iliyopita wakati akisoma maazimio ya utendaji kwamba mkuu huyo wa mkoa alikuwa anakwamisha utendaji wao.

Alipoulizwa jana wamepokeaje uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa mkuu huyo wa mkoa, Ole Sabaya alisema UVCCM Arusha wamefurahi kuondolewa kwake kwa kuwa walikuwa na migogoro naye. Mgogoro mkubwa ni madai ya UVCCM kwamba Ntibenda aliingilia kati mikataba ya maduka ya jumuiya hiyo na pia Serikali mkoa Arusha kudai kushindwa kudhibiti matukio ya shule kuchomwa moto. “Hatuwezi kuendelea kuona watoto wa shule wakipata shida kutokana na shule kuchomwa moto na hatua kali hazichukuliwi kwa wahusika,” alisema Sabaya

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu ilisema Ntibenda anahamishiwa kwenye ofisi hiyo na kupangiwa majukumu mengine.

Wananchi

Wakizungumza katika mahojiano na Mwananchi jana, wananchi, watendaji wa Serikali na wanasiasa walisema Ntibenda atakumbukwa kwa kurejesha mahusiano ya kisiasa baina ya vyama vya Chadema na CCM katika Jiji la Arusha.

Diwani wa Kata ya Ngarenaro (Chadema), Isaya Doita alisema Ntibenda kama binadamu anaweza kuwa na upungufu, lakini Arusha itamkumbuka kwa uvumilivu wa kisiasa aliokuwa nao.

Godi Mallya, ambaye ni fundi magari, mkazi wa Sakina alisema atamkumbuka Ntibenda kutokana na jitihada zake za kushirikiana vyema na vyombo vya dola kudhibiti matukio ya uhalifu yaliyohusisha ugaidi ambayo yaliukumba mji wa Arusha. “Arusha amani ilitoweka kwa matukio ya ugaidi, maandamano ya vyama na migogoro, lakini huyu Ntibenda aliweza kudhibiti,” alisema Mallya.

Mwenyekiti wa mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali Arusha (Anginet), Petro Ahham alisema watamkumbuka Ntibenda kama mtu aliyekuwa anasikiliza watu. Alisema Ntibenda mara nyingi katika maamuzi yake hakutumia nguvu tofauti na viongozi wengine hivyo licha ya kuwa na vyombo vya dola, lakini alipenda majadiliano.

Katibu wa umoja wa vyama vya waongoza watalii, Loshiye Mollel alisema watamkumbuka Ntibenda kwani alikuwa kiongozi msikivu na aliahidi kushughulikia matatizo ya wapagazi kulipwa malipo stahili ingawa hadi anaondolewa yalikuwa hayajapatiwa ufumbuzi.

Wachambuzi

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema mabadiliko hayo yanaweza kuwa ya kimkakati kisiasa.

“Ni kweli mimi nimesoma kwenye vyombo vya habari, japo sijajua hasa sababu iliyosababisha Ntibenda aondolewe, lakini naona kuna hofu kubwa kwenye utawala huu. Ni kweli wanaangalia kigezo cha utendaji kazi ‘Hapa Kazi Tu’ lakini kuna mikakati ya kisiasa zaidi kuelekea uchaguzi wa 2020,” alisema Mbunda na kuongeza: “Kama Ntibenda aliweka mazingira sawa kati ya wapinzani na CCM atakuwa amejiharibia kwa sababu huo mkoa una ushindani mkubwa wa kisiasa na viongozi wanawekwa pale kimkakati.

“Hakuna aliyefikiria kuwa Magufuli atakuwa Rais, hata mwenyewe amekiri kuwa ni Mungu tu aliyemsaidia, sasa asingependa tena 2020 iwe hivyo, lazima apange safu yake mapema.”

Mhadhiri wa Sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha Iringa, Profesa Gaudence Mpangala alisema kuna dalili za mikakati za siasa kugubika mabadiliko hayo.

“Sababu za kutolewa Ntibenda kwa kweli sizijui hata taarifa haikusema. Lakini nimesoma vyombo vya habari zimegusia sababu za kisiasa.

“Arusha ni ngome ya Chadema huo ndiyo ukweli. Mtu aliteuliwa Machi leo Agosti ameondolewa? Lazima kuna sababu. Pengine alionekana kuwa ‘liberal’, aliheshimu zaidi demokrasia, ndiyo maana Rais akaona hafai kupambana,” alisema Mpangala.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Fordia, Bubelwa Kaiza alisema mabadiliko hayo hayana mikakati ya kisiasa bali ni utendaji mpya wa Rais Magufuli ambao aliuahidi tangu anaingia madarakani.

“Rais Magufuli alisema tangu anaingia madarakani kuwa hataki mambo ya kazi kama kawaida, kwamba unaingia ofisini kwako unajipangia ratiba zako tu. Akiona mahali pana legalega anafanya mabadiliko haraka,” alisema na kuongeza.

“Unakumbuka alipowaambia viongozi wa kuteuliwa kuwa wasifanye sherehe hadi siku wanapoondoka? Maana yake ni kwamba hampi mtu nafasi ili ale na kunywa, akitaka anamwondoa wakati wowote.”

Alisema mabadiliko kama hayo yamefanyika katika mikoa ya Ruvuma, Shinyanga na Singida hivyo hoja ya upinzani haina mashiko.

“Ni kweli mkoa wa Arusha ni ngome ya upinzani kwa muda mrefu, lakini nasita kuhusisha mabadiliko haya na siasa hizo. Yameshafanyika Ruvuma, Singida, Shinyanga. Mbona hapa Dar es Salaam na kule Kagera kuna upinzani mkali, lakini hawabadilishwi?” alihoji Bubelwa.

Post a Comment

 
Top