0


Dar es Salaam. Kuna dalili kuwa wabunge wa vyama vya upinzani wanaweza kuachana na msimamo wao wa kususia vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia Ackson baada ya Spika Job Ndugai kusema anataka kumaliza suala hilo, huku kiongozi wa upinzani bungeni, Freeman Mbowe akiwa tayari kwa maridhiano.

Ndugai ambaye hakuwepo wakati wabunge wa upinzani walipoamua kususia vikao wakati wa Bunge la Bajeti, amesema atatafuta mbinu ya kuweka mambo sawa.

Wapinzani walianza kususia vikao vya Bunge mwishoni mwa Mei baada ya Dk Tulia kukataa chombo hicho kujadili kwa dharura sakata la wanafunzi 7,802 wa kozi maalumu ya ualimu wa masomo ya sayansi kutimuliwa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Hoja hiyo ilianzishwa na mbunge wa CCM wa Chemba, Juma Nkamia lakini alikosea kunukuu kanuni na hivyo kudakwa na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari aliyesahihisha makosa hayo. Hata hivyo, Dk Tulia amesema hakuona kama hoja hiyo inakidhi vigezo vya uendeshaji bora wa shughuli za Bunge na pia hakuona kama ina udharura unaozungumzwa.

Jibu lake lilisababisha wabunge wa CCM na upinzani kusimama kuonyesha wanamuunga mkono Nasari na jitihada za kutaka wakae zilishindikana, ndipo akaagiza askari kuingia ukumbini kuwatoa waliosimama.

Wakati wakiingia ukumbini, Dk Tulia aliahirisha kikao kabla ya muda, lakini askari walienda kumzonga Nasari, jambo lililoudhi wabunge hao wa upinzani.

Hadi Bunge linapitisha Bajeti ya mwaka 2016/17 na kuahirisha vikao vyake mapema Julai, wabunge hao wa upinzani hawakulegeza msimamo wao.

Mwezi ujao, Bunge la 11 linatarajia kuanza tena vikao vyake mjini Dodoma, wakati bado wapinzani hawajalegeza msimamo.

Lakini kauli ya Spika Ndugai, ambaye kwa muda mrefu wa vikao hivyo alikuwa nchini India kwa uchunguzi wa afya, inaweza kubadilisha hali hiyo.

“Kwa kweli hata mimi, hivi sasa (suala la kususia vikao) ni kitu ambacho kinanisumbua kichwani; kwamba tufanye vipi kufikia hali fulani ya maridhiano,” alisema Ndugai kwenye mahojiano katika kipindi cha Funguka kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Azam TV kila Jumapili saa 3.00 asubuhi.

Ndugai amesema atatumia uzoefu wa Bunge la Katiba kupata suluhu ya jambo hilo kwa kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano halina chombo cha maridhiano.

Alibainisha kuwa kanuni za Bunge la Katiba zilimpa Spika au mwenyekiti fursa ya kuunda kamati maalumu ya muda kwa ajili ya maridhiano na kwamba kamati hiyo huundwa kutegemea na aina ya jambo lililopo.

“Kwenye kanuni zangu mimi za kuendesha Bunge la kawaida, hatuna kitu chochote, ukiacha zile kamati ambazo ni rasmi. Na mambo haya ambayo yanatokea bungeni yanataka kitu cha aina hiyo,” alisema Ndugai, ambaye kabla ya kuwa Spika alishika nafasi ya unaibu. “Nafikiria itabidi tuazime uzoefu huo wa Bunge la Katiba. Tunaweza tukawapata baadhi ya watu hata kama ni maspika wastaafu au na watu wengine wakaja kusaidiana na Spika tukaitisha pande ambazo zina tofauti ili kuona tatizo kubwa ni nini,” alisema Ndugai.

Msimamo huo wa Spika umepokewa kwa mikono miwili na Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai, aliyesema wanamheshimu Ndugai pamoja na kiti chake hivyo wapo tayari kumsikiliza kwa hilo.

“Kama ameona kuna tatizo na kuna umuhimu wa kukaa mezani na kuzungumza hilo ni jambo la busara. Kuzungumza ni ujasiri na kunaonyesha ukomavu wa kisiasa,” amesema.

Mbowe alisema siku zote Ukawa wamekuwa wakiamini siasa ni mazungumzo, lakini ulipotokea mvutano uliosababisha wasusie vikao, upande wa pili wa Spika haukuwa tayari kujadili suala hilo na maamuzi yalikuwa yanatolewa kibabe.

Post a Comment

 
Top